“For there are two rules to keep at the ready—that there is nothing good or bad outside my own reasoned choice, and that we shouldn’t try to lead events but to follow them.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 3.10.18
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KANUNI KUU MBILI ZA HEKIMA…
Zipo kanuni kuu mbili za hekima ambazo unapaswa kuzijua na kuziishi wakati wote.
Moja; hakuna kitu kizuri wala kibaya, bali fikra zako ndiyo zinafanya kitu kiwe kizuri au kibaya.
Mbili; hupaswi kutaka mambo yaende kama unavyotaka wewe, bali unapaswa kuyafuata mambo yanavyokwenda.
Kanuni hizi mbili ambazo zinaonekana rahisi sana, zina nguvu kubwa ya kuyafanya maisha yako kuwa bora na tulivu zaidi.
Matatizo mengi unayotengeneza kwenye maisha yako yanaanzia kwenye fikra zako, pale unapochagua kipi kizuri na kipi kibaya.
Na pale unapotaka kula kitu kiende kama unavyotaka wewe, halafu vitu visiende hivyo, unajiona kama huna bahati au dunia haina usawa.
Vitu vinatokea kama ambavyo vinatokea, siyo vizuri wala vibaya, bali namna wewe unavyotafsiri kinachotokea ndiyo kunaleta uzuri au ubaya.
Kadhalika vitu vinatokea kwa namna ambavyo vinatokea na siyo kww namna ambavyo umepanga wewe vitokee.
Hivyo kama unataka maisha yako yawe bora na tulivu, ona uzuri kwenye kila linalotokea kwenye maisha yako, kwa sababu nsiyo upo uzuri. Na mambo yanapokwenda tofauti na ulivyopanga, badala ya kuumia na kutaka yaende ulivyopanga, yatumie kwa namna yalivyoenda.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi kwa kanuni hizi mbili za hekima, hakuna uzuri wala ubaya balo fikra zako na usitake kila kitu kiende kama ulivyopanga wewe.
#UzuriAuUbayaNiFikraZako, #DuniaHaifuatiMipangoYako, #OnaUzuriKwenyeKilaHali
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha