Kila mtu anashindwa kwenye maisha, hakuna ubishi kwenye hilo, haijalishi umefanikiwa kiasi gani, kuna baadhi ya mambo utajaribu na kushindwa. Hata makampuni makubwa duniani, yamekuwa yanakuja na mawazo ya bidhaa au huduma mpya ambazo zinashindwa vibaya mno na kuanguka kwenye soko.
Tatizo kwenye kushindwa linakuja pale ambapo kushindwa kwako unataka kuwe ni kushindwa kwa kila mtu. Kwa sababu wewe umeshindwa basi unaamini hakuna mwingine anayeweza. Au kwa kushindwa kwako unakuwa balozi wa kuwakatisha tamaa wengine wasijaribu kile ulichojaribu, tena ukijiona unawasaidia wasiumie kama ulivyoumia wewe.
Hii siyo sahihi kabisa, usitake kushindwa kwako kuwe maumivu kwa wengine, usitake kushindwa kwako kuwe kuwakatisha tamaa wengine wanaotaka kujaribu ulichoshindwa wewe.
Shindwa, lakini shindwa mwenyewe, usishindwe na kila mtu. Kama unaweza kushindwa kimya kimya ni bora kuliko kushindwa kwa makelele ambayo yatawatishia wengine. Na kama mtu atapenda kujifunza kupitia kushindwa kwako, eleza makosa uliyofanya ukashindwa ili yeye ayaepuke na siyo kuonesha kwamba ni vigumu kufanikiwa.
Na muhimu zaidi, upande wa pili pia unahusika, usikubali kushindwa kwa wengine kuwa maumivu kwako. Kwa sababu wengine wamejaribu wakashindwa haimaanishi kwamba na wewe ukijaribu utashindwa. Hata kama walioshindwa wana uwezo na nguvu kuliko wewe, kama ni kitu unachokitaka kweli kiendee. Unaweza kushinda, na hata ukishindwa, utajifunza mengi kuliko kutokujaribu kabisa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,