#TANO ZA JUMA #12 2019; Wewe Siyo Wa Kawaida, Sheria Kumi Za Kuishi Maisha Ya Mafanikio, Maeneo 12 Ya Kuzingatia Ili Ufanikiwe Kwenye Maisha, Jamii Inavyokuzuia Usiwe Tajiri Na Usiweke Furaha Yako Kwenye Malengo.

Karibu sana rafiki yangu mpendwa kwenye makala hii ya tano za juma.

Makala ambayo ina mkusanyiko wa mambo matano makubwa ya kujifunza kutoka kwenye kitabu nilichokisoma kwenye juma husika.

Juma hili la 12 la mwaka huu 2019 nimepata nafasi ya kusoma kwa kina kitabu kinachoitwa The Code of the Extraordinary Mind: 10 Unconventional Laws to Redefine Your Life and Succeed On Your Own Terms ambacho kimeandikwa na Vishen Lakhiani.

CODE OF EXTRAORDINARY MIND

Hiki ni kitabu ambacho kinakwenda kutupa mtazamo wa tofauti kabisa wa namna tunavyoyachukulia maisha yetu. Katika kitabu hiki tunajifunza kwa nini sheria na kanuni nyingi tunazoziishi siyo sahihi au zimepitwa na wakati. Na muhimu zaidi, kitabu kinatufundisha jinsi ya kuwa na maisha yasiyo ya kawaida, yaani kuwa na maisha ya kipekee kwetu, kwa namna tunavyotaka sisi wenyewe.

Hivi unajua kwamba mambo mengi ambayo umekuwa unaaminishwa ndiyo sahihi kwenye maisha siyo kweli? Kuanzia elimu, dini, mahusiano na hata kazi, imani nyingi ambazo tumebebeshwa siyo sahihi. Na mbaya zaidi, imani hizo zinakuwa kikwazo kwetu kupiga hatua zaidi. Katika kitabu hiki tunakwenda kujifunza jinsi ya kuvunja imani hizo na kujenga imani mpya ambazo zitatuwezesha kuwa na mafanikio makubwa.

Karibu kwenye tano hizi za juma tujifunze jinsi ya kuwa watu wa tofauti na wenye mafanikio makubwa sana.

#1 NENO LA JUMA; WEWE SIYO WA KAWAIDA.

Neno ‘WATU WA KAWAIDA’ limekuwa linatumika sana kwenye maisha ya kila siku. Watu wengi wamekuwa wanawekwa kwenye kundi la watu wa kawaida, kwa kuwa wanaishi maisha yao kama ambavyo wengine wanaishi. Wanaamini na kupokea kile ambacho jamii inawaambia ni sahihi na hawathubutu kuhoji kwa nini waamini au kufanya kile ambacho wengine wanaamini na kufanya.

Ukiishi kwa kupokea na kukubali kile ambacho jamii inataka ukubali, jamii itakupenda na utaitwa mtu wa kawaida. Lakini hili linakuja na gharama yake, huwezi kuwa na maisha ya uhuru, wala mafanikio makubwa kama utaenda kama jamii inavyotaka uende. Ukifanya kile ambacho kila mtu anafanya, utapata matokeo ambayo kila mtu anapata.

Hii ina maana kwamba, kama unataka kupata matokeo ya tofauti, kama unataka kufanikiwa kuliko pale ulipo sasa, lazima kwanza ukatae kuwa ‘MTU WA KAWAIDA’. Lazima uchague kuwa mtu ambaye siyo wa kawaida, lazima uanze kuhoji imani na kanuni nyingi ambazo umezipokea na kuziishi. Lazima uchague kusimama mwenyewe hata kama jamii nzima inapingana na wewe. Hili linakuja na manufaa ya kuwa na maisha yako, na kufanikiwa sana, lakini pia linakuja na gharama ya kusumbuliwa na jamii.

Jamii itahakikisha unajisikia vibaya pale unapokataa kuwa wa kawaida. Itatishia kukutenga, itakupa vitisho vya maisha kuwa magumu na ukose wa kukusaidia. Yote hiyo ni katika kuhakikisha hutoki kwenye kifungo cha ‘MTU WA KAWAIDA’.

Lakini mimi nakuambia kitu kimoja rafiki yangu, WEWE SIYO MTU WA KAWAIDA, hivyo kataa kifungo cha jamii cha kukufanya kuwa wa kawaida. Amua sasa kuishi uwezo mkubwa uliopo ndani yako, amua sasa kutumia akili uliyopewa, ambayo ina uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi. Anza kuhoji kila unachoamini na kukubaliana nacho, je ni sahihi, je ndiyo njia pekee na je hakuna namna nyingine ya kufanya kwa ubora zaidi.

Utakapoanza kutumia akili yako kufikiri na kuhoji, utaanza kuona njia mbadala na bora zaidi za kufanya kila kitu kwenye maisha yako, na hapo utakuwa na maisha yako, maisha ambayo siyo ya kawaida.

Wewe siyo mtu wa kawaida, kataa ulaghai wa jamii wa kukulazimisha uwe mtu wa kawaida. Ishi maisha yako, hiyo ndiyo njia pekee ya kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.

#2 KITABU CHA JUMA; SHERIA KUMI ZA KUISHI MAISHA YA MAFANIKIO.

Rafiki, kwenye kitabu chetu cha juma hili la 12, The Code of the Extraordinary Mind: 10 Unconventional Laws to Redefine Your Life and Succeed On Your Own Terms ambacho kimeandikwa na Vishen Lakhiani, mwandishi ametushirikisha sheria kumi za kuishi maisha ambayo SIYO YA KAWAIDA yatakayotuwezesha tuwe na mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Katika uchambuzi huu, nakwenda kukushirikisha sheria hizi kumi na jinsi ya kuziishi kila siku ya maisha yako ili uweze kupiga hatua zaidi. Karibu sana tujifunze kanuni hizi muhimu za kuondoka kwenye UKAWAIDA na kwenda kwenye MAFANIKIO.

CODE OF EXTRAORDINARY MIND 2

SHERIA YA KWANZA; ONDOKA KWENYE UKAWAIDA.

Watu waliofanikiwa sana wako vizuri kwenye kuona yale ambayo jamii inayaita maisha ya kawaida na wapo tayari kuchagua sheria na hali za kukubaliana nazo na kujua zipi za kuhoji au kupuuza. Watu hawa huwa wanachukua njia ambayo haipendelewi na wengi na hili linawawezesha kuja na uvumbuzi wa kipekee.

Tunaishi kwenye dunia za aina mbili. Kuna dunia ya ukweli halisi, vitu ambavyo ni kweli duniani kote, mfano moto unaunguza. Na kuna dunia ya ukweli ambao siyo halisi, huu ni ukweli ambao unaweza kuwa sahihi eneo moja, lakini siyo sahihi eneo jingine. Mfano dini, fedha, mahusiano, elimu zote hizi ni kweli ambazo siyo halisi. Dini moja inaiweza kuwa sahihi kwa kikundi fulani cha watu na isiwe sahihi kwa kikundi kingine.

Jukumu lako wewe ni kuweza kutofautisha ukweli halisi na usio halisi, ukweli halisi upokee kama ulivyo, lakini ukweli usiohalisi uhoji na wakati mwingine upuuze, kwa sababu umekuwa kikwazo kwako kuwa na maisha ya mafanikio.

SHERIA YA PILI; HOJI SHERIA ZA HOVYO.

Watu wasio wa kawaida, huwa wanahoji sheria za hovyo, sheria ambazo zinatokana na ukweli usio halisi. Wanajua kwamba sheria hizo haziendani na ndoto na matakwa yao. Wanatambua kwamba jinsi dunia inavyoenda ni matokeo ya watu kupokea sheria na kuziishi bila ya kuzihoji. Na sheria hizi zinakuwa siyo sahihi au zinakuwa zimeshapitwa na wakati.

Zipo sheria nyingi ambazo tumebebeshwa na kuaminishwa na jamii kama ndiyo ukweli halisi lakini siyo. Lazima uweze kuzitambua sheria hizi na kuzihoji au kuzipuuza. Kuna sheria nne ambazo zimepokea kama ukweli wakati siyo;

Moja; kwamba lazima uwe na elimu ya juu ndiyo utafanikiwa, siyo tu kwamba sheria hii siyo sahihi, lakini kwa zama hizi imepitwa na wakati.

Mbili; kwamba lazima ufanye yale ambayo kabila lako linafanya ndiyo uonekane mwaminifu kwa kabila hilo, kudumisha mila. Mila nyingi zimeshapitwa na wakati kwa zama tunazoishi sasa.

Tatu; kwamba lazima ukae kwenye dini ambayo wazazi wako walikukuza nayo, na lazima uwe kwenye dini fulani ndiyo utakuwa sahihi. Dini nyingi zimepoteza yale mamlaka ambayo zilikuwa nazo kutokana na kutokubadilika, huku mazingira na teknolojia ikibadilika kwa kasi.

Nne; kwamba lazima ufanye kazi kwa mateso ndiyo ufanikiwe, ni kweli kazi inahitajika, lakini mateso hayapaswi kuwa sehemu ya kazi, bali unapaswa kufanya kile unachopenda, na hapo haiwi tena kazi.

Swali ni je unawezaje kugundua kama sheria ni ya hovyo na hivyo kuihoji au kuipuuza? Kuna maswali matano ya kuuliza kwenye kila sheria ili kujua kama ni ukweli halisi au uzushi tu;

  1. Je sheria hiyo ni kweli kwa kila eneo duniani? Kama ni kweli kwa sehemu fulani na siyo kweli kwenye eneo jingine basi jua ni uzushi.
  2. Je sheria hiyo inaendana na kanuni ya Dhahabu, kwamba mfanyie mwingine kile ambacho ungependa kufanyiwa, kama ndiyo basi ni sahihi.
  3. Je sheria hiyo imetokana na utamaduni fulani au dini fulani? Kama ndiyo basi ni uzushi.
  4. Je sheria hiyo inakupa wewe nafasi ya kufikiri au inabidi uipokee tu kwa imani? Kama ni kupokea kwa imani basi ni uzushi.
  5. Je sheria hiyo inakuwezesha kuwa na furaha au inakuzuia usiwe na furaha? Kama haichangii wewe kuwa na furaha basi siyo sahihi.

Usikubali kupokea sheria au utaratibu wowote bila ya kuhoji na kuona kama ni sheria sahihi au ni uzushi.

SHERIA YA TATU; TENGENEZA UPYA UFAHAMU WAKO.

Watu wasio wa kawaida wanatambua kwamba ukuaji wao unategemea vitu viwili. Cha kwanza ni muundo wao wa uhalisia na cha pili ni mfumo wao wa maisha. Wanatengeneza muundo bora wa uhalisia na mfumo mzuri wa maisha na mara kwa mara wanaboresha mifumo hiyo ili kwenda na wakati.

Unaweza kuyachukulia maisha yako mama kompyuta, ambayo inaundwa na vitu viwili, mashine (hardware) na programu zinazoiendesha kompyuta hiyo (software). Kwenye maisha yako hardware ni muundo wako wa uhalisia ambao unajumuisha imani uliyonayo juu yako na dunia kwa ujumla. Sofrware ni mfumo wako wa maisha ambao unahusisha tabia zako, mahusiano yako, ufanyaji wako wa kazi na hata jinsi unavyopumzika na kujiburudisha.

Ili kompyuta ifanye kazi vizuri, lazima kila wakati iwe inaboreshwa zaidi upande wa hardware kwa kupata vifaa bora zaidi na upande wa software kwa kupata programu nzuri zaidi. Kadhalika, ili maisha yako yawe mazuri, lazima uboreshe muundo wako wa uhalisia, yaani imani zako na mfumo wako wa maisha yaani tabia zako za kila siku.

Unapotumia kompyuta au hata simu, mara kwa mara unaboresha zaidi, kwa kununua zilizo bora au kuweka programu za juu zaidi. Fanya hili kwenye maisha yako pia, kwa kuboresha imani zako na tabia zako za kila siku.

Yapo maeneo 12 ya kufanyia kazi kwenye maisha yako ili kuboresha imani zako na tabia zako, utayasoma kwa kina kwenye kipengele namba tatu cha makala ya juma.

SHERIA YA NNE; TENGENEZA UPYA MUUNDO WAKO WA UHALISIA.

Watu wasio wa kawaida wanatengeneza upya muundo wao wa uhalisia, ambao unawapa nguvu ya kujisikia vizuri na kuweza kuigeuza dunia iendane na maono waliyonayo kwenye akili zao. Watu hawa wanatengeneza upya imani zao badala ya kupokea kile ambacho kila mtu anaamini.

Ni juu yako kuchagua uamini nini juu yako mwenyewe na maisha yako, ili kuwa na maisha ya mafanikio, lazima utengeneze imani inayoendana na kile unachotaka.

Katika kujijenga vizuri kiimani, ili kuweza kutambua uwezo mkubwa ulionao wa kupata chochote unachotaka, kuna mazoezi mawili muhimu sana ya kufanya kila siku.

Moja ni zoezi la shukrani, kila siku fikiria vitu vitatu mpaka vitano ambavyo unashukuru kuwa navyo kwenye maisha yako. Inaweza kuwa kitu chochote, haijalishi kikubwa au kidogo. Unaposhukuru, unakuwa umeamini kwamba unaweza kupata zaidi.

Mbili ni zoezi la kujipenda mwenyewe. Hili ni zoezi la kujiuliza ni nini unapenda kwako mwenyewe. Kila siku orodhesha vitu vitatu mpaka vitano ambavyo unavipenda sana kuhusu wewe. Zoezi hili linakufanya ujithamini zaidi.

Kuna imani kuu nne unazopaswa kujijengea kwenye maisha yako ili uweze kupiga hatua zaidi.

Moja; amini kwamba kila mtu nguvu kubwa ndani yake, inayomwezesha kujua vingi na kuweza kufanya vingi.

Mbili; amini kwamba kuna nguvu kubwa kwenye akili na mwili ya kuweza kujitibu mwenyewe.

Tatu; amini kwamba furaha kwenye kazi ndiyo msingi wa uzalishaji mkubwa.

Nne; amini inawezekana kuwa mwamini asiye na dini, yaani kukua kiimani na kiroho bila kuwa chini ya dini yoyote.

Ukiweza kujijengea imani hizi mpya nne, hakuna kitakachokushinda kwenye maisha.

SHERIA YA TANO; BORESHA MFUMO WAKO WA MAISHA.

Watu wasio wa kawaida wanatumia muda mwingi kutafuta, kuboresha na kupima mifumo mipya ya maisha na kuitumia kwenye maisha yao, kazi zao, mioyo yao na hata imani zao. Watu hawa muda wote wapo kwenye hali ya ukuaji na kujigundua zaidi wao wenyewe.

Ni rahisi sana kujikuta unafanya kitu leo kwa sababu jana ulifanya, au kufanya kesho kwa sababu leo umefanya. Lakini hii ni njia ya uhakika ya kubaki kawaida. Ili kutokuwa wa kawaida, unapaswa kujipa muda wa kujihoji kwa nini unafanya unachofanya na kama njia unayotumia kufanya ndiyo sahihi. Kwa njia hii unaweza kuboresha zaidi mifumo yako ya maisha.

Njia ya kuboresha mfumo wako wa maisha ni kujifunza na kujaribu vitu vipya, kujijengea tabia mpya na kupata ujuzi mpya kwenye maeneo 12 muhimu ya maisha yako.

Katika maeneo 12 ya maisha yako, jiwekee viwango ambavyo hupaswi kushuka chini ya hapo, hii itakusukuma kuendelea kupiga hatua kila siku.

Pia unapaswa kujijengea mfumo wa kuyafanya maisha yako kuwa bora kila siku, ambao unahusisha kuwa na shukrani, kufanya tahajudi, na kuwa na utulivu wa hali ya juu.

SHERIA YA SITA; PINDISHA UHALISIA.

Watu wasio wa kawaida wana uwezo wa kupindisha uhalisia. Wana malengo na maono makubwa na yanayosisimua na kwa watu wa kawaida malengo hayo yanaonekana hayawezekani. Furaha yao haipo kwenye kuyafikia malengo hayo, bali kwenye kila hatua wanayochukua. Wana furaha kabla hata hawajafikia malengo yao makubwa, ambayo inawasukuma zaidi kufikia malengo yao makubwa. Kwa nje watu hawa wanaonekana kuwa na bahati, lakini kwa ndani wanaupindisha uhalisia, uende kama wanavyotaka wao.

Katika kuupindisha uhalisia kuna vitu viwili muhimu unavyohitaji;

Moja ni kuwa na maono makubwa na yanayosisimua, ambayo yanakuvuta kwenda mbele zaidi. Maono ambayo mtu wa kawaida akiyasikia anaona hayawezekani.

Mbili ni kuwa na furaha SASA, pale ulipo, kabla hata ya kupata unachotaka, unakuwa katika hali ya furaha, furaha hii ndiyo inakupa nguvu ya kuendelea zaidi hata pale unapokutana na magumu.

Kwa kuwa na vitu hivi viwili, chochote unachofanya hakiwi kazi kwako, bali unakuwa kama mchezo ambao unaufurahia.

SHERIA YA SABA; ISHI KWENYE NIDHAMU YA FURAHA.

Watu wasio wa kawaida wanaelewa kwamba furaha inaanzia ndani ya mtu. Wanaanza kuwa na furaha kabla hata hawajapata kile wanachotaka na furaha hiyo inakuwa nishati ya kuwasukuma kufikia maono yao makubwa.

Ili kuweza kuishi kwenye nidhamu hii ya furaha kila siku, unapaswa kufanya vitu vitatu;

Moja; SHUKRANI.

Unapaswa kuwa na shukrani kwa kila kinachoendelea kwenye maisha yako. Kila siku asubuhi na jioni tenga muda wa kutafakari na andika mambo matatu mpaka matano ambayo unashukuru kuwa  nayo kwenye maisha yako, na pia mambo matatu mpaka matano unayoshukuru kuwa nayo kwenye kazi au biashara yako. Kwa kuangalia mazuri uliyonayo, unaikaribisha furaha.

Mbili; MSAMAHA.

Msamehe kila ambaye amewahi kufanya chochote cha kukukwaza. Unaposamehe unajiondoa kwenye kifungo cha vinyongo na visasi, kitu ambacho kinakuweka huru na hivyo kuwa na furaha. Usiposamehe kila wakati utakuwa unajikumbusha kuhusu alichofanya mtu na kuendelea kujiumiza. Na unaposamehe, samehe kwa upendo, kwa kuwa na huruma kwa yule aliyekukosea, ukijua huenda ana matatizo fulani kwenye maisha yake yaliyompelekea akufanyie alichofanya.

Tatu; UTOAJI.

Unapaswa kutoa kwa wengine, kupitia kazi yako, biashara yako, mali zako na hata maisha yako kwa ujumla. Kila mmoja wetu ana kitu anaweza kutoa, na unakuwa na furaha zaidi unapotoa kuliko unavyopokea. Hivyo tafakari kwenye maisha yako vitu gani unaweza kutoa, angalia wenye uhitaji kisha wapatie. Utoaji unaleta furaha kubwa kwenye maisha.

SHERIA YA NANE; TENGENEZA MAONO YA BAADAYE.

Watu wasio wa kawaida huwa wanatengeneza maono makubwa ya baadaye ambayo ni yao na hayatokani na sheria zisizo halisi za kijamii. Maono yao yanawapeleka kwenye matokeo makubwa wanayotaka kupata na hali wanayotaka kujisikia kuliko kushindana na wengine.

Uwekaji wa malengo ni changamoto kwa wengi. Wengi wamefundishwa kuweka malengo yanayowapa vile vitu ambavyo kila mtu anavyo. Lakini hayo siyo malengo makubwa wala yanayomsukuma mtu.

Malengo sahihi kuweka ni yale ambayo yanatumia uwezo mkubwa wa ndani yako, kukufikisha kwenye hatua za juu zaidi za kile cha kipekee unachofanya. Malengo haya yanakupa maono makubwa na ya kipekee kwako, ambayo hakuna mwingine unayeshindana naye, unafanya kwa sababu ni muhimu kwako na siyo kwa sababu kila mtu anafanya au wengine wanategemea ufanye.

Maono unayojiwekea yanapaswa kugusa vipengele vitatu vya maisha yako, ambavyo ni hisia zako, ukuaji wako na mchango wako kwa wengine. Katika hisia yanaingia mahusiano yetu na hata mazingira, katika ukuaji inaingia afya, akili, ujuzi na imani na katika utoaji kwa wengine inaingia kazi, ubunifu, familia na jamii kwa ujumla.

SHERIA YA TISA; USIYUMBISHWE NA CHOCHOTE.

Watu wasio wa kawaida hawahitaji udhibitisho au hamasa ya nje ili kufanyia kazi malengo yao. Badala yake wana utulivu mkubwa ndani yao na wanajiamini kutoka ndani yao, wana msukumo wa ndani wa kupata chochote wanachotaka. Hawajali wengine wanasema au kufanya nini, wao wanafanyia kazi kile wanachotaka. Watu hawa wanaishi bila ya hofu, wana kinga dhidi ya ukosoaji au sifa za wengine. Kinachowasukuma ni furaha iliyo ndani yao na kujipenda wao wenyewe.

Kama unataka kufikia maono yako makubwa, lazima uvuke kila aina ya hofu, uwe tayari kusimamia kile unachoamini hata kama dunia nzima inakupinga. Unapaswa kuwa imara na usiyetetereshwa wala kuyumbishwa na chochote. Ili kufikia hali hii, unahitaji vitu viwili;

Moja; malengo ambayo yanajichochea yenyewe, haya ni malengo ambayo yanatoka ndani yako na siyo yale ya nje ya kushindana.

Mbili; kujiona kwamba umekamilika na hivyo kutohitaji hamasa ya wengine. Lazima uweze kujiona kwamba umekamilika kwa namna ulivyo, ujiamini na kuwa tayari kuchukua hatua mwenyewe na siyo kutegemea hamasa za wengine. Unapokuwa mkamilifu unaona jinsi ulivyo na vitu vingi vya kutoa kwako mwenyewe na kwa wengine pia.

Zipo njia tatu za kufikia hali ya kujiamini na kutokuyumbishwa, kujiambia najipenda, kujipa sababu kwa nini unajipenda na kuishi katika wakati uliopo kwa mawazo yako kuwa kwenye kile unachofanya.

SHERIA YA KUMI; POKEA WITO WAKO.

Watu wasio wa kawaida wanapokea, kukubali na kusukumwa na wito ambao upo ndani yao, kitu kinachowasukuma kuleta mabadiliko chanya duniani. Wito huo unawasukuma kupiga hatua kwenye maisha na pia kupata maana ya maisha yao na hivyo kuwa tayari kujisukuma zaidi, hata pale safari inapokuwa ngumu.

Wale wenye mafanikio makubwa sana duniani huwa hawana kazi wala biashara, bali wana wito. Chochote wanachofanya hawakichukulii kama sehemu tu ya kuingiza kipato, bali wanachukulia kama sehemu ya wao kutoa mchango mkubwa na kuifanya dunia kuwa sehemu bora ya kuishi.

Lazima na wewe utafute na kupokea wito wako ambao utakusukuma kuweka juhudi zaidi kuifanya dunia kuwa sehemu bora na wewe mwenyewe kufanikiwa zaidi.

Ili kujua wito wako, kuna maswali matatu muhimu unayopaswa kujiuliza na kujipa majibu sahihi;

Swali la kwanza; kumbuka wakati ambao umewahi kujisikia hali ya furaha sana katika maisha yako, hali ambayo unaweza kusema dunia ilikuwa kama mbingu. Je ulikuwa unafanya nini wakati huo?

Swali la pili; fikiria kama ungekuwa na uwezo wa miujiza wa kutengeneza mbingu hapa duniani. Je mbingu hiyo ingekuwa na nini, yaani nini unakiona kama mbingu hapa duniani?

Swali la tatu; ni hatua zipi ndogo na rahisi unazoweza kuchukua ndani ya masaa 24 yajayo na ukaweza kutengeneza mbingu hapa duniani.

Kumbuka tunaposema mbingu duniani ni ile hali unayojisikia pale ambapo kila kitu kipo kamili kwako. Kuna vitu ambavyo ukivifanya unakuwa na utulivu mkubwa, unajisikia vizuri, huchoki na wala husumbuki kwamba unamaliza saa ngapi. Vitu hivyo ndivyo vimebeba wito wako ndani yake, pokea wito wako na weka maisha yako katika kuutimiza, na hilo litakufanya usiwe wa kawaida na ufanikiwe sana.

#3 MAKALA YA JUMA; MAENEO 12 YA KUZINGATIA ILI UFANIKIWE KWENYE MAISHA.

Rafiki yangu, watu wengi wanaposikia mafanikio huwa wanafikiria eneo moja tu, fedha na mali. Ndiyo maana ukiwaambia watu kwamba umefanikiwa, swali la kwanza kukuuliza ni una nini? Watu wanataka waone vitu ndiyo waseme umefanikiwa. Na hakuna ubaya wowote kwenye kutumia mali kama kipimo cha mafanikio.

Ila tunapokwama ni pale tunapotumia mali kaka kipimo pekee cha mafanikio. Tunasahau maisha ya mafanikio yana vipengele vingi ambavyo lazima vifanye kazi kwa pamoja ndiyo mtu aweze kusema kweli amefanikiwa.

Kwa kutokuelewa, wengi wamekuwa wanaweka juhudi zao kwenye mali pekee, na wanazipata kweli, lakini licha ya kuwa na mali nyingi, bado maisha yao yanakuwa hayana furaha. Hii ni kwa sababu wanakuwa wameyatenga maeneo mengine muhimu sana kwa mafanikio yao.

Rafiki, kama unataka mali na mafanikio makubwa yenye mlinganyo sahihi kwenye maisha yako, basi yapo maeneo kumi na mbili ambayo unapaswa kuyafanyia kazi kwenye maisha yako. Kwenye makala ya juma hili, nimekushirikisha maeneo hayo 12 kama nilivyojifunza kwenye kitabu cha juma.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo ya maeneo 12, unaweza kuisoma sasa hapa; Maeneo Kumi Na Mbili (12) Muhimu Sana Kwa Mafanikio Ya Maisha Yako, Malengo Ya Kujiwekea Kila Eneo Na Vitabu Vya Kusoma Ili Kufikia Mafanikio Makubwa.  Usiache kusoma makala hii, kwa sababu wengi walioisoma wamesema imewapa msingi muhimu sana. Bonyeza hayo maandishi au kiungo kufungua na usome.

#4 TUONGEE PESA; JAMII INAVYOKUZUIA USIWE TAJIRI.

Rafiki, kama ulikuwa hujui, jamii inafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba huwi tajiri. Na kama unabisha wewe angalia tu jinsi watu wa kawaida wanavyofanya inapokuja upande wa fedha.

Watafanya kazi kwa nguvu kubwa ili wapate fedha, wakishapata fedha hiyo wataitumia yote mpaka iishe. Ikiisha hawatasubiri mpaka wapate nyingine, badala yake watakopa fedha ili kuendelea na matumizi. Hapo sasa wanakuwa na deni, hivyo kipato ambacho hakikuwatosha awali walipokuwa hawana deni, sasa wana deni, hivyo kipato kinazidi kutokuwatosha, na hapo inawabidi wakope tena.

Mtu anakuwa ameingia kwenye mtego ambao atazunguka nao maisha yake yote, anafanya kazi akipata fedha analipa madeni, halafu anaanza kukopa tena, anafanya kazi, analipa madeni, anakopa tena. Wengi wanakwama hapa maisha yao yote.

Sasa utaniuliza jamii inahusikaje hapa? Na mimi nitakujibu kwa kauli moja ambayo amewahi kuisema mtu mwenye busara ‘watu wengi, wanatumia fedha ambazo hawana, kununua vitu ambavyo hawavihitaji, kuwaridhisha watu ambao hawajali’.

Na pia nitakuongezea kauli ya Mwanafalsafa wa Ustoa Seneca, ambaye anasema ‘mahitaji ya msingi ya maisha ni machache sana, na yapo ndani ya uwezo wa kila mtu, ni yale ya anasa ndiyo yanawasumbua wengi’.

Naamini utakuwa umeanza kupata mwanga namna gani jamii inawazuia wengi kuwa matajiri. Ni kwa sababu jamii inawaaminisha wengi kwamba lazima uwe na hiki au kile ndiyo uonekane una maisha mazuri au umefanikiwa. Hivyo mtu ambaye hana uwezo wa kupata kile ambacho jamii inahesabu kama mafanikio, inambidi akope kukipata. Na hapo ndipo wengi wanaingia kwenye gereza.

Kila mtu ana nguo nyingi kuliko anavyoweza kuzivaa, lakini bado watu wanaendelea kununua nguo. Kila mwenye nyumba ana vyumba vingi kuliko anavyohitaji. Na hata kwenye magari, mtu ana gari kubwa kuliko uhitaji wake, au ana gari ambalo hahitaji kuwa nalo. Ila kwa kuwa jamii inapima kama mafanikio, basi mtu anaingia kwenye madeni kuwa na vitu hivyo.

Na sisemi kwamba watu wasivae nguo nzuri, wasiwe na majumba makubwa au kuwa na magari ya kifahari, hakuna ubaya wowote kwenye hilo. Ila ninachosema ni hiki, kama unaingia kwenye madeni ili kupata vitu hivyo basi jua jamii imeshashinda, imeshafanikiwa kukuweka kwenye gereza ambalo hutaweza kufikia utajiri na mafanikio ya kweli kwenye maisha.

Chagua kuishi misingi ya mafanikio ambayo haitakuweka kwenye gereza wala kukufanya kuwa mtumwa wa fedha za watu. Ishi ndani ya uwezo wako na kila wakati kazana kukuza kipato chako zaidi. Kama kitu huwezi kukimudu kuwa na subira na weka kazi kupata fedha ya kukimudu, usiingie kwenye madeni ili tu kumudu kitu ili kuonekana na wewe una uwezo kama wengine. Kumbuka maisha ni yako, hivyo chagua kuyaishi ilivyo sahihi kwako. USIWE MTU WA KAWAIDA, KUWA WEWE.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA;USIWEKE FURAHA YAKO KWENYE MALENGO.

“Have big goals—but don’t tie your happiness to your goals. You must be happy before you attain them.” ― Vishen Lakhiani

Jinsi ambavyo watu wengi wamekuwa wanaweka malengo yao, iwe ni makubwa au madogo wamekuwa wanakosea. Hii ni kwa sababu huwa wanaahirisha maisha mpaka wafikie malengo hayo. Mtu anajiambia nikishapata kitu fulani basi nitakuwa na furaha. Hivyo mtu anatumia furaha ya baadaye kama msukumo wa kufanyia kazi lengo.

Lakini wote tunajua, ukifikia lengo moja unaona malengo mengine mengi zaidi ya kufikia, hivyo furaha inaendelea kuahirishwa. Kwa namna hii, wengi wanaishi maisha yao bila ya kuwa na furaha, kwa sababu wakipata wanachotaka, wanaona vitu vingi zaidi ambavyo bado hawajapata.

Ili kuwa na maisha bora, hupaswi kuweka furaha yako kwenye malengo yako. Badala ya kusubiri mpaka ufikie lengo fulani ndiyo uwe na furaha, anza kuwa na furaha kwanza na hilo litakuwezesha kufikia lengo hilo na kuwa na maisha pia.

Furaha kwenye maisha yako haipaswi kuambatanishwa na kitu chochote, unapaswa kuwa na furaha hata kama huna chochote. Kwa sababu kama huna furaha ukiwa huna kitu, basi hata ukikipata hakitakuletea furaha, badala yake kitazidisha ile hali ya kutokuwa na furaha.

Maisha ya furaha ni kuchagua wewe mwenyewe, lakini sivyo jamii inavyokuaminisha, hivyo kuwa na furaha ya kweli kwenye maisha yako, lazima uache kuwa mtu wa kawaida. Anza na furaha na utaweza kufikia lengo lolote. Achana na jamii inayokuambia uanze na lengo ili likuletee furaha, utakimbiza furaha kama kukimbiza upepo maisha yako yote.

Hizi ndizo tano za juma hili la 12, tumejifunza kwa kina umuhimu na jinsi ya KUWA WA TOFAUTI, hivyo chukua hatua ili uwe wa tofauti na maisha yako yaweze kuwa na mafanikio makubwa zaidi.

Katika mafunzo ya ziada, nitakayoshirikisha kwenye channel ya TANO ZA JUMA, nitakushirikisha aina ya tofauti ya TAHAJUDI ambayo Vishen ametufundisha kupitia kitabu chake. Kwa wale wote ambao wanasumbuka kufanya tahajudi ya kawaida ya pumzi, tahajudi hii ya tofauti ni rahisi zaidi, ina mtiririko mzuri na unaweza kuifanya kwa dakika 15 pekee. Lakini matokeo yake ni makubwa sana kwenye maisha yako. ili usikose maarifa haya na mengine mengi, jiunge sasa na CHANNEL YA TAZO ZA JUMA, maelekezo ya kujiunga yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpendwa, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu