“Diogenes of Sinope said we sell things of great value for things of very little, and vice versa.”
—DIOGENES LAERTIUS, LIVES OF THE EMINENT PHILOSOPHERS, 6.2.35b

Ni siki nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari LIPIA KITU KULINGANA NA THAMANI YAKE…
Tumekuwa tunalipa gharama kubwa sana kwa vitu ambavyo havina umuhimu mkubwa kwenye maisha yetu.
Tumekuwa tunajitoa mhanga kwa vitu ambavyo haviongezi thamani yoyote kwenye maisha yetu.
Na hii hutokea pale tunapojaribu kushindana na wengine, pale tunapojilinganisha na wengine na kuona kuna kitu tunakosa.

Tunapaswa kupima thamani ya kitu kwenye maisha yetu kabla hayujalipa gharama yake.
Tusikazane tu kuwa na kitu kwa sababu kila mtu anacho au kila mtu anategemea uwe nacho.
Bali tukazane kuwa na kitu kwa sababu ni muhimu kwetu, kwa sababu kinaongeza thamani kwenye maisha yetu.

Tunapaswa kukumbuka kwamba kila kitu tunachotafuta kwenye maisha yetu kina gharama kubwa sana, ambayo ni maisha yetu.
Unapoweka muda na nguvu ili kupata kitu unachotaka, jua kwamba muda na nguvu hizo huwezi kutumia kwenye kitu kingine.
Je kila unachokifanya kinastahili kweli kupoteza sehemu ya maisha yako?
Je kila unachohangaika nacho, kinastahili kulipiwa gharama ambazo unalipa, ukilinganisha na thamani yake?
Ukijiuliza maswali hayo kwenye kila unachofanya, utagundua vitu vingi vinavyokusumbua havistahili kabisa kukusumbua, maana havina thamani kubwa kwako.

Kama kila unachofanya kinaiba sehemu ya maisha yako, ni vyema kufanya vile ambavyo ni muhimu zaidi kwako na vyenye thamani kubwa.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kulipa gharama zinazoendana na thamani ya kitu kwenye maisha yako.
#HangaikaNaMuhimu, #MudaWakoNiAdimu, #UsipotezeMaishaKwaYasiyoMuhimu

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha