“If you should ever turn your will to things outside your control in order to impress someone, be sure that you have wrecked your whole purpose in life. Be content, then, to be a philosopher in all that you do, and if you wish also to be seen as one, show yourself first that you are and you will succeed.”
—EPICTETUS, ENCHIRIDION, 23

Tumeiona siku nyingine nzuri sana leo rafiki,
Ni jambo kubwa na la kushukuru sana, kwa sababu siyo wote waliolala jana wameamka leo.
Wapo ambao walilala wakiwa na mipango mizuri na mikubwa, lakini leo hawajaamka kabisa au wameamkia hospitalini.
Lakini wewe umeamka na nguvu za kuweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako. Ni jambo la kushukuru, na njia pekee ya kuonesha shukrani hizi ni kutumia vizuri siku hii ya leo, kwa kutokupoteza muda wala nguvu kwa mambo yasiyo muhimu.

Tukaitumie vizuri siku hii ya leo kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KWA NINI UNATAKA KUMRIDHISHA KILA MTU?
Pale unapoanza kufanya vitu ili uonekana na wengine, ndiyo unaacha kuwa wewe na kuanza kuwa maigizo.
Unakuwa umeacha kuishi kusudi la maisha yako na kuanza kuhangaika kuishi kusudi la wengine, ambao hata hawajui kusudi lao ni nini.
Kwa kifupi unapofikia hatua ya kufanya kitu ili uonekane, unakuwa umechagua kupoteza mwenyewe maisha yako.

Chagua kuishi maisha yako kwa uhalisia wako, lijue kusudi lako na liishi kila siku. Fanya kitu kwa sababu ni muhimu kwako na kinakupeleka kwenye kusudi lako na siyo kwa sababu kila mtu anafanya au anategemea ufanye.

Maisha yana uhuru mkubwa sana kama mtu utachagua kuyaishi maisha yako na kuacha wengine waishi maisha yao.
Lakini maisha yanakuwa utumwa mkubwa pale unapofanya mambo ili kuwaridhisha au kuwafurahisha wengine.
Kwa sababu, kwanza hutaweza kumridhisha na kumfurahisha kila mtu na pili, hata kama hilo lingewezekana, bado ndani yako hutaridhika.

Unaridhika pale unapoishi kusudi lako, hivyo funga macho na weka pamba masikioni ili uweze kuachana na wanayofanya wengine na kufanya yale ambayo ni muhimu kwako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi kusudi la maisha yako na kuacha kutaka kumridhisha kila mtu.
#IshiMaishaYako, #MaishaSiyoMashindano, #FanyaYaliyoMuhimuKwako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha