Kuna nguvu kubwa mbili zinazohusika kwenye kila hatua ambayo tunachukua kwenye maisha yetu. Nguvu hizo ni maumivu na uchoshi.

Tunapokuwa hatuna kitu fulani tunachokitaka sana, huwa tunapata maumivu. Maumivu haya yanatusukuma kupata kile ambacho tunakitaka, na kadiri maumivu yanavyokuwa makubwa, ndivyo tunavyosukumwa kupata kitu hicho.

Tunapopata kile tunachotaka, huwa tunakizoea haraka na kukichosha, hii huleta hali ya uchoshi. Huwa tuna matarajio makubwa sana kwa kile tunachotaka au kufanyia kazi, lakini tunapopata kitu hicho, tunagundua hakiwezi kutimiza matarajio yetu, hivyo tunaishia kuchoka.

Kama unataka kuyadhibiti maisha yako, uwe na uhuru na hata mafanikio, lazima ujifunze kudhibiti nguvu hizo mbili. Kwa sababu kama hutazitumia wewe mwenyewe, wengine watazitumia na kunufaika na wewe.

Kwanza kabisa unapaswa kuelewa kwamba hali hizo mbili hazitaondoka kabisa kwenye maisha yako, hata upate nini, kuna wakati utakuwa na maumivu ya kutaka kupata kitu fulani, na kuna wakati utakuwa umekichoka kile ambacho tayari unacho.

Elewa kwamba maisha ni mwendelezo wa maumivu na uchoshi, unakuwa na maumivu unapokosa kitu fulani, lakini ukishakipata unakuwa na uchoshi kwa kuwa nacho, na kutaka kupata zaidi.

Kitu kingine muhimu ni kuelewa kwamba maisha yako yamekamilika hapo ulipo, hata kama hujapata kile ambacho unatamani sana kuwa nacho. Tambua kwamba hakuna chochote unachohitaji ili kukamilisha maisha yako, hata kile unachojiambia kwamba ukishakuwa nacho utafurahia, furaha haidumu muda mrefu baada ya kukipata, na baadaye hufuata mazoea.

Usiweke furaha yako kwenye vitu vya nje, kwa sababu vitu hivi ndiyo vinaleta maumivu na uchoshi, furaha yako inapaswa kuanzia ndani yako. Kama huna furaha kabla hujapata kitu, usifikiri utakuwa nayo baada ya kupata kile unachotafuta.

Unapojikuta kwenye maumivu au uchoshi, jitofautishe wewe kama nafsi na hisia hizo. Ziangalie kama vile unavyomwangalia mtu mwingine, zielewe na kisha usiziruhusu ziharibu utulivu wako wa ndani.

Hakuna wakati ambao utaweza kuondokana kabisa na hali hizi mbili, hivyo zipokee na jikubali wewe mwenyewe na endesha maisha yako bila ya kusukumwa sana na hisia hizo mbili.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha