“First off, don’t let the force of the impression carry you away. Say to it, ‘hold up a bit and let me see who you are and where you are from—let me put you to the test’ . . .”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 2.18.24
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari AMINI LAKINI DHIBITISHA…
Huwa tunaangushwa na wale watu ambao tunawaamini sana,
Watu ambao hatukutegemea watufanyie kile ambacho wamefanya,
Tunaishia kuwalaumu kwa kutumia vibaya uaminifu wetu.
Lakini mtu pekee unayepaswa kumlaumu ni wewe mwenyewe.
Hupaswi kumwamini mtu yeyote yule bila ya kudhibitisha,
Hupaswi kukubaliana na kile ambacho mtu anakuambia bila ya kudhibitisha wewe mwenyewe.
Hata kama ni mtu ambaye mnaaminiana na kuheshimiana, usikubali tu kitu bila ya kudhibitisha wewe mwenyewe.
Ni kwa kuamini bila ya kudhibitisha wengi wamekuwa wanadanganywa na hata kutapeliwa.
Unashirikiana na mtu kwenye biashara au mradi fulani, anakuambua usiwe na shaka, mambo yanaenda vizuri, kwa kuwa unamwamini unapokea kauli yake.
Ni mpaka wiku unakuja kustuka mradi umeshakufa ndiyo unajiuliza mbona uliambiwa mambo yanaenda vizuri.
Kosa limekuwa lako kwa kuamini mambo yanaenda vizuri bila ya kudhibitisha mwenyewe.
Dhibitisha kila kitu, hata kama ni mtu unayemwamini kiasi gani.
Kutaka kwako kudhibitisha kunaweza hata kumsaidia yule unayemwamini, kwa sababu mara nyingi mtu huwa hajui kama anakosea, anaona kila kitu kinaenda sawa, mpaka pale mambo yanapoharibika.
Dhibitisha kila unachojihusisha nacho, na utapunguza sana migogoro baina yako na wengine, hasa wale ambao unawaamini sana.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuamini na kudhibitisha wewe mwenyewe.
#AminiLakiniDhibitisha, #HojiKilaUnachokutanaNacho, #TafutaUkweliKwenyeKilaJambo
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha