Rafiki yangu mpendwa,

Inapokuja kwenye kuingiza kipato, kuna watu wanaojiambia kwamba wapo tayari kufanya chochote ili tu wapate fedha. Na wanapokuwa na uhitaji mkubwa wa fedha, wanafanya chochote kupata fedha. Wanajituma sana, na wanazipata fedha kweli, lakini baada ya kupata fedha, badala ya maisha kuwa mazuri, yanakuwa hovyo kwao.

Hapa ndipo unakutana na mtu mwenye fedha nyingi, ana kila anachotaka, lakini hana amani ndani yake. Licha ya kuonekana ana mafanikio makubwa kwa nje, ndani yake kunakuwa na utupu mkubwa.

Wengi wamekuwa wanajaribu kuziba utupu huo kwa kununua vitu vya kifahari zaidi, lakini utupu huo umekuwa haujai. Na kadiri mtu anavyokazana kuuziba kwa kununua vitu, ndivyo utupu huo unakuwa mkubwa zaidi.

Tatizo hili kubwa ambalo linawasumbua wengi waliofanikiwa, linaanzia kwenye kushindwa kutofautisha kazi, taaluma na wito. Na ndiyo maana tunaona watu wenye kazi na taaluma zinazoheshimika sana wanakosa furaha kwenye maisha yao. Wakati watu wengine wanaofanya viti vya chini wanaonekana kuwa na furaha kubwa kwenye maisha yako.

kazi, taaluma na wito

Kwenye makala hii, tunakwenda kujifunza tofauti ya kazi, taaluma na wito na unachohitaji ili kuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha yako, mafanikio ambayo yamekamilika.

KAZI.

Kazi ni kitu chochote unachofanya ili kuingiza kipato. Lengo kuu la kazi ni kupata kipato cha kuendesha maisha, bila ya kujali kama kazi hiyo unaipenda au la. Kinachokufanya uwe kwenye kazi hiyo ni kipato unachopata, na ukiacha kulipwa unaacha kufanya. Hakuna tofauti ya jana na leo kwenye kazi, unafanya kitu kile kile, ili kupata kipato.

Kazi ni ngazi ya chini kabisa na ambayo haina kuridhika ndani yake. Na wengi ambao walichonacho kwenye maisha ni kazi tu, huishia kuharibu maisha yao, kwa sababu wakati ambao hawafanyi kazi, wanaishia kwenye ulevi au tabia nyingine ambazo zinawaharibu kabisa, lengo likiwa kuukimbia uhalisia. Uhalisia kwamba wapo kwenye kazi isiyokuwa na maana kwao, ila wanahitaji fedha, hivyo inawabidi wafanya.

Kazi yoyote unayofanya ambayo huhitaji kuwa na utaalamu nayo ipo kwenye kundi hili. Iwe ni kubeba mizigo, kulima shamba, kusafisha, na vibarua mbalimbali, ni sehemu tu ya kuingiza kipato, ambapo ukuaji ni mdogo au haupo kabisa na hakuna utofauti mkubwa unaoweza kuweka kwenye kile unachofanya.

TAALUMA.

Taaluma ni ujuzi ambao mtu umeupata kwa kusomea au kujifunza na unapofanya kazi unakuwa na nafasi ya kujifunza na kukua zaidi. Kwenye taaluma kuna ngazi za ukuaji, ambapo ukikazana kuweka juhudi na elimu, unaweza kufika ngazi za juu kabisa.

Kwenye taaluma unaondoka kufanya kazi kwa ajili ya malipo pekee, na hapa unakuwa na nafasi ya kukua zaidi kupitia taaluma hiyo. Unaweza kuanzia ngazi ya chini, labda ukiwa na cheti, ukaenda stashahada, shahada, na shahada za juu zaidi.

Taaluma iko juu zaidi ya kazi, lakini bado siyo kitu unachohitaji ili kuwa na maisha ya mafanikio, kwa sababu wengi huishia kukwama kwenye ngazi fulani ya taaluma, au kupanda ngazi mpaka mwisho lakini bado maisha yakawa hayamridhishi.

Mfano wa taaluma ni kazi zote watu wanazofanya ambazo zinahitaji kusomea au ujuzi maalumu. Ualimu, udaktari, uhasibu, uwakili na nyinginezo ni taaluma ambazo mtu anaweza kuzipata na kupiga hatua zaidi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; WHY WE WORK (Nadharia Ya Nini Kinawasukuma Watu Kufanya Kazi).

WITO.

Wito ni kazi ambayo mtu anaifanya kutoka ndani yake, ambayo ni sehemu muhimu ya mtu na ina maana kwake. Inapokuwa kwenye wito mtu hafanyi kwa sababu anataka fedha, au kwa sababu anataka kupiga hatua zaidi, bali kwa sababu anataka kufanya. Hii ina maana kwamba, hata kama mtu huyo halipwi, bado ataendelea kufanya kazi hiyo. Kuifanya tu kazi yenyewe inaleta hali ya mtu kuridhika zaidi ndani yake.

Mtu anapokuwa anafanya kazi ambayo ni wito wake, anakuwa na msukumo mkubwa ndani yake wa kufanya zaidi. Hasubiri kusukumwa wala haangalii analipwa nini, furaha kwake ni kufanya, kutoa kile ambacho kipo ndani yake.

Mtu anapokuwa kwenye wito, haoni kile anachofanya kama kazi, bali anaona ndiyo maisha yenyewe. Mtu aliyepo kwenye wito hasumbuki na kujiuliza kama afanye kazi au awe na maisha, kwake kazi na maisha ni kitu kimoja.

Wito unaweza kuwa kwenye kitu chochote, ambacho kwa nje kinaweza kuonekana ni kazi au taaluma, lakini kwa ndani kinakuwa na maana kubwa sana kwa mtu.

SOMA; Jinsi ya kugeuza kipaji chako kuwa biashara inayokuingizia kipato.

Unachopaswa kufanya ili kufanikiwa.

Ili uwe na mafanikio makubwa kwenye maisha yako, na yanayokupa kuridhika, unapaswa kuwa na wito wa maisha yako. Lazima kila siku uwe unafanyia kazi wito wako. Kama itatokea wito huo ukawa ndiyo kazi au taaluma yako, basi itakuwa rahisi zaidi kwako kwa sababu hutahitaji kusumbuka zaidi.

Lakini kama wito wako haujaanza kukulipa, utahitaji kuwa na kazi au taaluma unayofanyia kazi ili maisha yaende, lakini hupaswi kusahau wito wako. Endelea na kazi au taaluma yako huku pia ukiendelea kufanyia kazi wito wako kila siku. Na weka juhudi kubwa kwenye wito wako ili nao uwe sehemu ya kuingiza kipato.

Ukishafika hatua ambayo wito wako unakuingizia kipato, hapo sasa unaweza kuachana na kazi au taaluma yako na kuweka nguvu zako zote kwenye wito wako, kitu ambacho kitakuwezesha kufanikiwa zaidi na kuwa na maisha bora na ya kuridhika.

Hakikisha unaujua wito wako kwenye maisha ni nini, na kama hujajua basi fanya zoezi hili rahisi, jiulize ni kitu gani unapenda sana kufanya au kufuatilia, ambacho unafanya hata kama hakuna anayekulipa, na wengine hupenda kuomba ushauri kwako kwenye eneo hilo, au wanakutegemea zaidi kwenye eneo hilo. Huo ndiyo wito wako na wajibu wako ni kuendeleza wito huo.

SOMA; KITABU CHA MAY; Biashara Ndani Ya Ajira; Jinsi Ya Kuanzisha Na Kukuza Biashara Yako Ukiwa Bado Umeajiriwa.

Kuna kipindi kwenye maisha yako utahitaji kuwa na kazi, utahitaji kuwa kwenye taaluma, lakini hayo yote ni katika kujenga wito wako. Unapoufanya wito wako kuwa sehemu ya kukuingizia kipato, maisha yako yanakuwa kitu kimoja, hufikirii kazi, maisha na kupumzika, unafikiria maisha tu, ambayo yanajumuisha kila kitu ndani yake.

Usiache kufanyia kazi wito wako kila siku, hii ndiyo njia pekee ya kujitengenezea uhuru wa baadaye na kuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge