Kukosa maandalizi ni kikwazo kikubwa sana kwa wengi kufanikiwa.
Wengi huwa wanapanga kufanya kitu, lakini hawana maandalizi ya kutosha, hivyo wanakwama kwa sababu kile wanachohitaji ili kuendelea hakipatikani.
Ndiyo maana leo nakuambia kama unawahi mahali, tayari umeshachelewa. Yaani kama unaharakisha kufika mahali fulani, basi jua umeshachelewa. Ungepaswa kuondoka mapema kiasi kwamba huhitaji kuharakisha.
Pale unapopanga kufanya kitu, hakikisha una maandalizi ya kutosha, hakikisha hutakwama mahali kwa sababu ya uzembe wako.
Na moja ya maandalizi muhimu kuwa nayo ni matokeo tofauti na unayotegemea kupata. Unapopanga chochote usifikirie kila kitu kitaenda kama ulivyopanga. Hivyo fikiria matokeo mbadala yanayoweza kutoka na hivyo uwe na hatua mbadala za kuchukua. Fikiria vikwazo vyote vinavyoweza kujitokeza na kuwa na njia ya kukabiliana na vikwazo hivyo ili usikwamishwe na chochote.
Kama umeweka mipango fulani, lakini katika kuitekeleza ukakutana na vikwazo, ambavyo vimekustua na ukajiambia hukutegemea, basi jua hukuwa na maandalizi sahihi, ulikuwa unajidanganya tu na kujidanganya kwako kumekugharimu.
Usiharakishe kuwahi mahali, badala yake ondoka mapema ili uweze kufika kwa wakati. Kadhalika katika safari ya mafanikio, usifikirie kile tu unachotegemea kupata, bali fikiria matokeo mbadala yanayoweza kujitokeza na jiandae kuyakabili. Maandalizi ni muhimu sana, yape kipaumbele cha kutosha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,