Hakuna kipindi ambacho watu wamevurugwa kama zama tunazoishi sasa.
Hizi ni zama pekee ambazo watu wanafikiri mafanikio yatatokana na mwonekano na siyo kutokana na kazi.
Hivyo watu wamekuwa wanaweka nguvu kubwa kwenye mwonekano, kuhakikisha wanaonekana na wengi.
Mitandao ya kijamii imechochea sana hili, sasa hivi watu wanapima mafanikio yao kwa ‘likes’, ‘followers’ na ‘comment’ mtu anazopata kwenye mitandao ya kijamii.
Wengi wanakazana kupata umaarufu wa kujulikana na sana, wakiamini huo ndiyo utakaowaletea mafanikio, kwenye kazi au biashara zao. Lakini hizi ni mbio za kujidanganya na kujipoteza.
Kitu pekee ambacho kitakuletea mafanikio makubwa ni kuifanya vizuri kazi yako, kuifanya kwa utofauti, kuifanya kwa ubora ambao hakuna mwingine anaweza kufanya hivyo. Kuweka thamani kubwa sana kiasi kwamba mtu kuona kama anakuibia.
Kwa njia hii, kazi itajitangaza yenyewe, wale wanaonufaika nayo watawaalika wengine nao waje wanufaike nayo na utakuza zaidi unachofanya pamoja na kufanikiwa zaidi.
Tatizo ni moja, kujenga kazi yako inahitaji juhudi kubwa, kujitoa, uvumilivu na muda. Matunda yake yanachukua muda kuonekana. Lakini kufanyia kazi mwonekano kutafuta umaarufu wa haraka kuna majibu ya haraka, lakini kwa muda mrefu haina matokeo mazuri.
Sasa kwa kuwa wengi wanaona karibu kuliko kuona mbali, wanaishia kufanya kile kinacholeta majibu ya muda mfupi na kuepuka kinacholeta majibu ya muda mrefu.
Ondoka kwenye kundi hilo la kukazana na mwonekano na nenda kwenye kundi la kukazana na kazi. Kazi ndiye rafiki pekee ambaye hatakuacha kama wewe hutamwacha. Ijue vizuri kazi yako, ifanye kwa ubora na maisha yako yatakuwa bora.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,