“It isn’t events themselves that disturb people, but only their judgments about them.”
—EPICTETUS, ENCHIRIDION, 5

Ni jambo la kushukuru sana kwa kila mtu aliyeiona siku hii nyingine mpya kwetu.
Siyo kwa nguvu wala akili zetu tumepata nafasi hii, bali kwa bahati ya kipekee mno.
Tungeweza kukubwa na mabaya yaliyowakumba wengine siju ya jana, kama magonjwa, ajali na mengineyo.
Lakini sisi tumepata nafasi ya kuianza siku hii mpya, tukiwa na afya na nguvu ya kufanya makubwa zaidi.
Kuchagua kutumia nguvu na muda wako kwa mambo yasiyo muhimu, ni kuidharau bahati hii uliyoipata leo.

Tukaiishi siku hii ya leo kama ndiyo siku ya kwanza kwetu, hivyo tusahau kabisa mazoea ya nyuma. Lakini pia tuiishi siku hii kama ya mwisho, kama hakuna kesho na hivyo tuepuke kuahirisha chochote.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KINACHOKUUMIZA NI HUKUMU UNAZOTOA…
Hakuna kitu chochote kinachotokea kwenye maisha yako ambacho kina nguvu ya kukuumiza wewe, hakuna kabisa.
Kitu pekee ambacho kimekuwa kinakuumiza ni hukumu unazotoa kwa yale yanayotokea.
Kwa lugha nyingine, hakuna mtu yeyote anayeweza kukuumiza wewe bali wewe mwenyewe.

Kuna mtu umemsalimia hakuitika! Halafu wewe unajiambia ana dharau, ana visa na wewe na kadhalika. Lakini huenda mtu huyo hakusikia wakati unamsalimia, huenda ametungwa na mambo yake. Na huenda ana matatizo yake binafsi juu yako, ambayo hayapaswi kukupa wewe wasiwasi wowote.

Kuna mtu amukutukana au kukujibu vibaya! Na hilo linakuumiza sana. Lakini kumbuka siyo matusi au majibu ya mtu yanayokuumiza, bali maana unazoweka kwenye majibu na matusi hayo. Vipi kama mtu angetoa maneno hayo hayo lakini wewe hukuyasikia, je yangekuumiza? Na vipi kama mtu ametoa maneno hayo hayo kwa lugha ambayo huielewi kabisa, bado ungeumia? Kwa hakika huwezi kuumia kama hujasikia au hujaelewa lugha iliyotumika, hivyo unaona maumivu ni kitu unachotengeneza mwenyewe.

Acha kujiumiza wewe mwenyewe kwa hukumu unazotoa kwa yale yanayotokea kwenye maisha yako. Chukulia kila jambo kama linavyotokea na acha kulipa maana zozote zile. Kazana na maisha yako na mengine yasikusumbue kabisa. Muda na nguvu ulizonazo vina ukomo, ni vyema kuviwekeza kwenye yake muhimu unayofanya kuliko kuvitumia kujiumiza mwenyewe.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuacha kujiumiza kwa hukumu zako mwenyewe.
#Usihukumu, #DhibitiHisiaZako, #UsitakeWatuWaweKamaUtakavyoWewe

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha