Kwenye maisha huwa tunawadanganya wengine, tukijua kabisa kwamba tunadanganya, lakini inafika hatua tunajidanganya na sisi wenyewe.

Kuna kichekesho kimoja ambapo mtu alikwenda kisimani kuchota maji, akakuta kuna foleni ya watu wengi, na kuona atachelewa kuchota maji. Alikuwa amebeba embe anakula. Akajiuliza anawezaje kuwashawishi watu hao ili achote maji haraka. Baada ya kufikria, akaona awadanganye. Akawaambia nyie mbona mmekaa hapa wakati kuna mtu anagawa maembe matamu kule? Watu kusikia hivyo wakatoka mbio kuelekea walipoelekezwa.

Sasa mtu yule alibaki peke yake kisimani, badala ya kuchota maji akajiuliza mbona wameamini wote, labda ni kweli, basi na yeye akawafuata nyuma.

Unaweza kuona mfano huo ni kichekesho tu, lakini umebeba uhalisia mkubwa sana kuhusu maisha yetu. Huwa tunaanza kuwadanganya wengine, wanapoamini na sisi tunakuta tunajidanganya wenyewe. Kile ambacho awali tulijua kabisa kwamba tunadanganya, tunajikuta tukikiamini sisi wenyewe, na hapo ndipo tunapokuwa tumepotea kabisa.

Tabia zote mbaya tumekuwa tunazijenga kwa kuwadanganya wengine na hatimaye kujidanganya sisi wenyewe pia.

Unapaswa kuusimamia ukweli mara zote, unapaswa kusimamia kile kilicho sahihi. Usiwadanganye wengine, kwa sababu kitakachofuata ni kujidanganya mwenyewe. Na hata kama kila mtu anafanya kitu, kama siyo sahihi ni siyo sahihi, usifanye kwa sababu tu wengi wanafanya.

Utajiepusha na matatizo mengi sana kama utacha kudanganya wengine na kujidanganya mwenyewe. Pia ukiacha kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, na kufanya kilicho sahihi, utakuwa na maisha bora na tulivu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha