“Atreus: Who would reject the flood of fortune’s gifts?
Thyestes: Anyone who has experienced how easily they flow back.”
—SENECA, THYESTES, 536
Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KATAA ZAWADI ZINAZOTAMANISHA…
Kama umewahi kuvua samaki au kuona watu wakivua samaki, unajua kabisa kwamba ukiweka ndoano pekee kwenye maji hakuna samaki ambaye ataingia kwenye ndoano hiyo, hata awe mjinga kiasi gani.
Lakini weka chambo kwenye ndoano hiyo, weka mdudu mtamu ambaye samaki wanamtamani sana na hakuna samaki anayepita karibu atakayeweza kukwepa kunasa kwenye ndoano hiyo.
Hivi ndivyo maisha yetu binadamu yalivyo.
Wengi wanajua wakija kwetu na mahitaji wanayotaka tuwafanyie hatutakubali. Hivyo wanachofanya ni kutupa kwanza zawadi, zawadi ambayo wanajua hatuwezi kuikataa, zawadi ambayo inatutamanisha kweli.
Ukishapokea zawadi hiyo ndipo sasa mahitaji ya wewe kuwafanyia watu hao vile wanavyotaka yanapoanza, inakubidi ufanye hata kama ulikuwa hutaki, kwa sababu umeshapokea zawadi.
Rafiki, sisemi usipokee zawadi, bali kuwa makini sana na zawadi unazopewa na hata wale wanaokupa zawadi hizo.
Angalia mahusiano yako na anayekupa zawadi na jiulize ananufaikaje kwa yeye kukupa zawadi hiyo.
Angalia ukubwa wa zawadi unayopewa ukilinganisha na kile unachofanya.
Kadiri ambavyo huna uhusiano wa karibu na anayekupa zawadi, na kadiri zawadi inavyokuwa kubwa na inayotamanisha, nyuma yake kuna masharti ambayo yatakutesa sana.
Kataa zawadi ambazo zinatamanisha na zinazotoka kwa watu ambao hawana sababu yoyote ya kukupa zawadi. Itakuepusha na utumwa wa kujitakia.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kukataa zawadi zinazotamanisha.
#UsipendeVyaBure, #TamaaNiKifungo, #KilaMtuAnafanyaKinachomnufaisha
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha