Nikuulize swali, ni mara ngapi umekuwa na sauti ndani yako inakuambia ufanye kitu fulani, lakini dunia inakuambia ufanye tofauti, unaifuata dunia na unapata matokeo ambayo siyo uliyotegemea?

Jibu ni mara nyingi, kila mmoja wetu amewahi kukutana na hali hizi, sauti ya ndani inakuambia ufanye X, dunia inakuambia ufanye Y, na matokeo yanakuwa mabaya.

Ndani ya kila mmoja wetu kuna sauti inayojua mengi kuhusu sisi, sauti hii inatujua kuliko tunavyojijua sisi wenyewe, kwa sababu ina kumbukumbu za muda mrefu kuhusu sisi, tangu tukiwa watoto.

Lakini dunia haijui chochote kuhusu sisi, dunia inaweza kwenda kwa mazoea, kwa kuangalia wengi wanafanya nini, lakini haitujui sisi kiundani.

Hivyo unapokuwa njia panda, hujui ni hatua gani uchukue, na sauti ya ndani inakuambia ufanye A, huku dunia ikikuambia ufanye B, basi sikiliza sauti yako ya ndani na fanya A.

Acha kuisikiliza dunia na isikilize sauti yako ya ndani pale unapokuwa njia panda na hukui kupi cha kufanya.

Siyo mara zote ukisikiliza sauti yako ya ndani utapata matokeo mazuri, lakini ni bora kushindwa kwa kusikiliza sauti yako ya ndani kuliko kushindwa kwa kusikiliza sauti ya dunia.

Unapaswa kujua kwamba ndani yako una uwezo mkubwa, akili yako ya ndani ina uzoefu mkubwa kwa mengi ambayo umewahi kupitia. Na kama hutaiuliza basi itakuambia kupitia sauti ya ndani.

Sikiliza sauti yako ya ndani, inajua mengi kuhusu wewe kuliko dunia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha