“Believe me, it’s better to produce the balance-sheet of your own life than that of the grain market.”
—SENECA, ON THE BREVITY OF LIFE, 18.3b
Ni siku nyingine mpya na ya kipekee sana kwetu.
Tumepata fursa bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari BOBEA KWENYE YALE MUHIMU…
Hapo ulipo umeshabobea kwenye mambo mengi mno katika kipindi chote cha maisha yako.
Kwanza ni kwenye kile unachofanya ili kuingiza kipato, unajua nje ndani kuhusiana na kazi au biashara yako.
Pili ni mambo yanayoendelea, umekuwa hupendwi kupitwa na chochote, hivyo umekuwa unakazana kuhakikisha unajua kila kinachoendelea.
Tatu ni michezo au sanaa nyingine, unahakikisha unajua kila kinachoendelea kwenye ulimwengu huo, timu au mchezo unaoushabikia unauelewa vizuri sana.
Sasa swali linakuja, je una ubobezi wa kutosha kwenye maisha yako mwenyewe kama ulionao kwenye maeneo hayo mengine?
Je unajua nini hasa unataka kwenye maisha yako na kuweza kuachana na mengine katika kufanyia kazi kile unataka?
Je unajua ni maeneo yapi upo vizuri na una uimara na maeneo yapi ambayo una udhaifu?
Je unajua kusudi la maisha yako, kile ambacho uko hapa duniani kukitekeleza na kukifanyia kazi?
Je unaelewa maana ya maisha mazuri na jinsi ya kuyaishi maisha yako kwa ukamilifu na kutokuipunja dunia?
Rafiki, inavyoonekana ni rahisi kubobea mambo ya nje ambayo hayana umuhimu mkubwa, kuliko kubobea mambo ya ndani.
Anza sasa kuweka jitihada kubwa kubobea mambo yaliyo ndani yako. Ukibobea ya ndani, ya nje hayatakusumbua.
Lakini kama utakazana kubobea ya nje na ukasahau ya ndani, kila wakati utaona kuna kitu hakijakaa sawasawa hata upate nini.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya maisha kubobea kwenye yale ambayo ni muhimu zaidi.
#BobeaYaliyoMuhimu, #JijueMwenyeweKwanza, #JaliMamboYako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha