Tukisikia kupiga kura huwa tunafikiria kipindi cha uchaguzi pekee.

Lakini maisha yetu ya kila siku ni uchaguzi, kila siku tunajikuta kwenye sanduku la kupiga kura. Lakini wengi hatuelewi hili na ndiyo maana tunafanya maamuzi ambayo ni mabovu.

Kila mtu ana kampeni anayopiga kwako.

Wapo wanaotaka fedha ulizonazo, hivyo wanakupa matangazo mbalimbali ya bidhaa na huduma wanazouza.

Wapo wanaotaka muda wako, hivyo wana taarifa na maarifa mbalimbali wanayotaka uyajue.

Na wengi wanataka umakini wako, wanataka uwafuatilie kwa yale wanayofanya.

Ukuaji wa mitandao ya kijamii umefanya uchaguzi huu wa kila siku kuwa mkali na mrefu, kwa sababu kila mtu anataka muda wetu, kila mtu anataka umakini wetu.

Kwa kila dakika unayotumia kufanya kitu, maana yake umepiga kura kukubali kufanya kitu hicho.

Kwa kila senti yako unayotoa kununua chochote, maana yake umepiga kura kukubali kitu hicho.

Na kwa chochote unachokipa umakini wako, unachokifikiria, umepiga kura kukikubali.

Kuchukulia maisha yako kama uchaguzi kunakufanya ufikirie mara mbili kabla hujafanya kitu. Je ni kweli kitu hicho ndiyo muhimu, ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako? Je katika machaguo mengi ambayo umekuwa nayo kwenye siku yako, yale uliyofanya ndiyo bora kabisa?

Tunapoenda kwenye uchaguzi, huwa tuna vigezo vyetu vya nani tutampigia kura na kwa sababu gani. Hakuna anayekwenda kupiga kura akisema naenda tu yeyote nitakayemkuta kwenye karatasi namchagua huyo huyo.

Lakini maisha yetu tumekuwa tunayaendesha hivyo, hatuna vigezo tunavyotumia kuchagua matumizi ya muda wetu, fedha zetu na hata umakini wetu. Tunajiendea tu na chochote kinachojitokeza kinachukua fedha zetu, muda wetu na umakini wetu.

Haishangazi kwa nini mwisho wa siku unakuwa umechoka lakini ukiangalia hakuna kikubwa umefanya, kwa sababu umeingia kwenye uchaguzi bila ya kuwa na vigezo.

Anza sasa kuichukulia kila siku yako kama siku ya uchaguzi na jiwekee vigezo utakavyotumia kwenye kupiga kura na fedha zako, muda wako na umakini wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha