“Nothing will ever befall me that I will receive with gloom or a bad disposition. I will pay my taxes gladly. Now, all the things which cause complaint or dread are like the taxes of life—things from which, my dear Lucilius, you should never hope for exemption or seek escape.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 96.2
Ni jambo la kushukuru sana kwa kuiona siku hii nyingine mpya ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Tusipoteze hata dakika moja leo, kwa sababu muda huu si wetu.
Tusijiambie tutafanya kesho yake tuliyopanga kufanya leo, kwa sababu hakuna kwenye uhakika wa kesho.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari LIPA USHURU WAKO…
Maisha mazuri tunayoyataka, hayaji kirahisi na wala hayaji bure.
Kwanza tutahitaji kujituma sana na wakati mwingine kujitesa ili kupata kile tunachotaka.
Na tukishakipata siyo kwamba mambo yatakuwa rahisi, bali yanazidi kuwa magumu zaidi.
Unapokuwa hujafanikiwa changamoto zako zinakuwa ni chache na za kawaida.
Kadiri unavyozidi kufanikiwa, changamoto zako zinakuwa nyingi na kubwa.
Unapokutana na vikwazo zaidi kila unapopiga hatua usiumie wala kuona kama dunia inakupinga,
Bali jua huo ni ushuru unaopaswa kulipa kuishi maisha ya mafanikio.
Unapokazana sana kuweka juhudi na kupiga hatua, lakini wengine wakasema umebahatisha tu au umependelewa, jua huo ni ushuru unapaswa kulipa.
Unapokazana kupiga hatua, huku wengine wanakazana kukurudisha nyuma ni ushuru unaopaswa kulipa kwa mafanikio yako.
Anza kuangalia kila ugumu unaokutana nao kama ushuru wa maisha yako, ushuru ambao huwezi kuukwepa kwa namna yoyote ile.
Pokea ushuru huo na ulipe mara moja ili maisha yaendelee.
Usiwe mtu wa kulalamikia yale magumu unayokutana nayo kwenye maisha,
Bali yapokee kwa shauku kubwa, ukijua lazima uyapitie ili kupiga hatua zaidi.
Na pia tegemea ushuru mkubwa zaidi kadiri unavyotaka mafanikio makubwa zaidi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa tayari kupokea na kulipa ushuru wa maisha yako.
#LipaUshuruWaMaishaYako, #MafanikioSiyoRahisi, #VikwazoHaviishi
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha