Zama tunazoishi ni zama ngumu sana kwa fikra zetu sisi binadamu.

Ni zama ambazo watu wenye ushawishi wanaonekana kuweza kuigawa jamii kama watakavyo. Wale wanaopata nafasi za uongozi au kupata ushawishi kwa njia nyingine, wanaonekana kuwa na nguvu ya kuweza kuibua hisia kali ndani ya watu na kuwagawa.

Mitandao ya kijamii imeweza kuchochea sana hili, na watu wa kawaida wanajikuta wakiwa wamejigawa upande mmoja au mwingine, bila hata kujua msingi wa mgawanyiko huo.

Watu wengi wanajiona kama hawana tena udhibiti, wanajiona kama wanasukumwa huku na kule na wale wenye ushawishi.

Pia tumefika hatua ambayo mtu anatamani angeweza kuacha kutumia simu yake muda mwingi lakini hawezi. Mtu anajiambia kabisa kwamba matumizi ya mitandao ya kijamii yameleta uraibu kwake, anatamani angeacha lakini hawezi.

Ni jambo la kushangaza kwamba sisi binadamu, kwa uwezo mkubwa ambao tunao ndani yetu, tunashindwa kufanya maamuzi ya msingi kwetu. Maamuzi kama tunasimamia nini na tunatumia au hatutumii nini.

Ninachotaka kukukumbusha hapa ni kimoja, udhibiti upo ndani yako. Wengine wanaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwako, mitandao na teknolojia zinaweza kuwa na nguvu kubwa kwako, lakini mwisho wa siku udhibiti uko ndani yako.

Maamuzi bado ni yako wewe mwenyewe, wewe pekee ndiye unayefanya maamuzi kama ukubaliane na mtu au upingane naye. Wewe ndiye unayeamua kama utumie kitu au uache kutumia.

Usikubali kutoa nguvu hiyo kwa mtu mwingine yeyote, usikubali yeyote akufanyie maamuzi muhimu ya maisha yako. Baki na udhibiti huo muhimu wa maisha yako na utakuwa na maisha bora na huru.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha