“Do away with the opinion I am harmed, and the harm is cast away too. Do away with being harmed, and harm disappears.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 4.7

Siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi hii adimu ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUUMIZWA NI MAONI YAKO…
Kuumizwa ni maoni yako binafsi.
Pale mtu mwingine anapokufanyia jambo fulani au anaposema jambo fulani na wewe ukajiambia umeumia, siyo kwamba mtu yule amekuumiza, bali maoni yako mwenyewe ndiyo yanayokuumiza.
Hii ina maana kwamba, kama utapunguza na kuacha kuwa na maoni kwenye kila kinachotokea, kamwe hutaumizwa.
Kama utachukulia kila jambo kama lilivyotokea, bila ya kulipa maana na maoni yako binafsi, hakuna kinachoweza kukuumiza.

Lakini pale unapoanza kutafakari kwa kina yale wanayofanya au kusema wenyewe. Pale unapoanza kujipa maana, ndipo unapojiumiza mwenyewe.
Ni mara ngapi umekuwa huna tatizo na mtu, mnaendelea vyema, halafu mtu mwingine akaja kukuambia mtu huyo alikusema vibaya siku za nyuma, na hapo hapo ukaanza kuwa na shida naye?
Ulikuwa vizuri kabla hujaambiwa alikusema vibaya, licha kwamba alishakusema vibaya, lakini baada ya kujua, ndiyo unabadilika. Je huoni hapo kinachokuumiza wewe ni maoni yako binafsi juu ya mtu huyo?

Usikubali mtu yeyote avuruge amani na utulivu wako wa ndani,
Usikubali yeyote awe chanzo cha wewe kuumia,
Watu wanafanya mambo na kusema maneno usiyopenda wala kutaka, na wataendelea kufanya hivyo maisha yao yote, hilo lisikusumbue hata kidogo.

Ondoa maoni kwamba umeumizwa na hakuna kitakachoweza kukuumiza kwenye maisha yako.
Hata wale watakaojaribu kukuumiza kwa makusudi, watajisikia vibaya sana na kuumia zaidi wao watakapogundua kwamba huumii.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuachana na maoni kwamba umeumizwa na hakuna atakayeweza kukuumiza.
#KuumizwaNiMaoni, #DhibitiFikraZako, #UsiwapeWengineNguvuJuuYako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha