Kama umewahi kuangalia mchezo wowote, hasa mpira wa miguu, ambao una ushindani mkali, pale timu moja inapoifunga timu nyingine, ghafla mchezo unabadilika.
Timu iliyofunga inapunguza kushambulia na kukazana kulinda zaidi ili isifungwe. Na timu inayokuwa imefungwa inakazana kushambulia zaidi ili kufunga.
Hali hii husababisha moja kati ya mambo haya mawili, timu iliyofunga kufungwa na mchezo kurudi kwenye ushindani, au timu iliyofunga kuweza kujilinda zaidi isifungwe na mchezo kukosa ladha.
Kwenye maisha yetu, hasa safari ya mafanikio, ndivyo mambo yanavyokwenda.
Tunapokuwa tunaanza, tunakuwa na kiu na njaa kubwa ya mafanikio, tunajituma sana, tunaweka juhudi, tunajaribu vitu ambavyo ni hatari kweli kweli na hatari hiyo inawaletea manufaa makubwa.
Lakini mtu anapoanza kupata mafanikio, ghafla anabadilika, anaanza kulinda mafanikio hayo yasipotee, hivyo hachukui tena hatua za hatari kama alivyokuwa anachukua mwanzo, hajaribu tena vitu vipya na kwa wengi, hawajitumi tena kama mwanzo.
Unapojikuta kwenye hali kama hii, jua umeanza kujenga ukuta kwenye mafanikio yako na ukuta huo ndiyo gereza lako, siyo kwamba tu unajizuia kufanikiwa zaidi, bali pia unajirudisha nyuma, kwa sababu kwenye maisha kuna kwenda mbele au kurudi nyuma, hakuna kusimama.
Kazi yako kubwa kwenye safari hii ya mafanikio ni kugundua pale unapoanza kujenga ukuta kwenye mafanikio yako na kuubomoa. Pale unapoanza kuona unaogopa kuchukua hatua ambazo huko nyuma ulichukua bila shida, pale unapoanza kujiambia enzi zangu nilikuwa nafanya hivi au vile, jua umeshajijengea ukuta na ubomoe mara moja.
Ifanye kila siku ya maisha yako, kazi yako na hata biashara yako kuwa siku yako ya kwanza na pia siku yako ya mwisho. Unapofanya kitu kwa mara ya kwanza unakuwa na shauku kubwa, na pia unapofanya mara ya mwisho unajituma zaidi, huahirishi chochote.
Usijenge ukuta wowote kwenye mafanikio yako, usiogope kujaribu vitu vipya, usiache kuchukua hatua za hatari. Unahitaji kuendelea kuchukua hatua zaidi kama unataka kufanikiwa zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,