“Epictetus says we must discover the missing art of assent and pay special attention to the sphere of our impulses—that they are subject to reservation, to the common good, and that they are in proportion to actual worth.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 11.37

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari WIGO WA HISIA ZAKO…
Hisia zisipowekewa wigo, huwa zinakua bila ya kizuizi.
Unaweza kuanza na kitu kidogo, lakini kadiri unavyokilisha hisia, kinakua kikubwa sana.
Tunapaswa kujua wigo wa hisia zetu na kuzuia usikue kupitiliza.
Tunapaswa kupima kila hisia tunazokuwa nazo na thamani yake kwenye maisha yetu.
Kwa sababu hisia ndiyo kitu kinatupa msukumo wa kujituma zaidi na kufanya makubwa, lakini kama hazitadhibitiwa vizuri, zitakuwa chanzo cha sisi kupotea zaidi.

Ni muhimu sana kudhibiti hisia zetu, siyo kuzifuta au kuziondoa kabisa, hicho ni kitu ambacho hakuna anayeweza.
Lakini kuzidhibiti, kuziwekea wigo, kuhakikisha zinakusukuma kufanya mambo mazuri na yenye faida, ni jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wa kila mmoja wetu.

Kuwa mlinzi wa fikra zako na elewa kila hisia inayoibuka ndani yako, jihoji kwa nini hisia hiyo imeibuka na iwekee ukomo isikue na kupitiliza, kiasi cha kukuzuia usifikiri sawasawa na hilo kupelekea kufanya maamuzi mabovu.

Unapojua wigo wa hisia zako, inakuwa rahisi kwako kuzidhibiti zisiwe na madhara na pia kunufaika na kila aina ya hisia inayoibuka ndani yako. Lakini kama utaacha hisia ziibuke na kukua bila ya ukomo, utakuwa na matatizo kila siku kwenye maisha yako.
Hisia ni kama moto, ukiudhibitibna kuutumia vizuri una manufaa makubwa mno, lakini ukiuachilia hovyo utaunguza kila kitu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kudhibiti na kujua wigo wa hisia zako ili usiuvuke.
#DhibitiHisiaZako, #JuaWigoWaHisiaZako, #UsichezeNaMoto

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha