Ukirusha jiwe juu, baada ya muda litarudi chini. Jiwe hili limeweza kwenda juu sana na baadaye kurudi chini.
Je unafikiri kuna tofauti yoyote kati ya jiwe lililokuwa juu na lililorudi chini? Hakuna, ni jiwe lile lile.
Hivi ndivyo tunavyopaswa kujichukulia sisi wenyewe tunapokuwa juu na tunapokuwa chini.
Maisha yetu yanabadilika, kuna wakati tunakwenda juu, na kuna wakati tunashuka chini. Ni hali ya kawaida kabisa ya maisha, na hata asili ndivyo inavyokwenda.
Kinachotuumiza sisi ni kujichukuliwa watu wa tofauti katika nyakati hizo tofauti za maisha yetu. Tunapokuwa juu tunajiona wa thamani zaidi na tunapokuwa chini tunajiona tumekosa thamani.
Lakini kwa uhalisia hakuna kinachobadilika ukiwa juu na ukiwa chini, bali fikra na mtazamo wako pekee.
Chagua kuwa kama jiwe, chagua kujithamini sana wewe mwenyewe kila wakati, iwe uko juu au uko chini. Chagua kubaki kuwa wewe bila ya kujali ni kitu gani unapitia kwenye maisha yako. Kwa njia hii utakuwa imara na hakuna kitakachoweza kukuyumbisha.
Ukipata shukuru, ukikosa shukuru, ukipanda shukuru na ukishuka shukuru, maisha yako yatakuwa bora na tulivu na utaweza kupiga hatua zaidi licha ya kukutana na magumu mengi.
Kumbuka wastoa wanavyotuambia, chochote tulichonacho tumepewa tu kwa muda, ni kama tumekopeshwa, ipo siku tutakirudisha, hivyo hilo lisikubadili kwa namna yoyote ile.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,