Unapojitoa kwa ajili ya mafanikio, unapochagua kuondoka kwenye maisha ya kawaida na kwenda kwenye maisha ya mafanikio, ya kufanya makubwa na kupiga hatua zaidi, watajitokeza watu wengi ambao watakupa ushauri, ambao kwao wanaamini ni ushauri muhimu sana.
Lakini sehemu kubwa ya ushauri ambao watakupa ni kukuonesha jinsi gani mambo yatakuwa magumu, watakuonesha wale walioshindwa na kwa nini wewe pia utashindwa. Watakuonesha ni jinsi gani malengo uliyojiwekea ni makubwa na yatakuumiza, bora ungeweka madogo kwanza.
Watu hawa wanafanya hivyo kwa nia njema kabisa, kwa kuwa wao wenyewe hawathubutu kuchukua hatua kama zako, hivyo wanajaribu kukulinda usiumie, maana huwezi kufanikiwa bila ya kuumia.
Kitu kimoja unachopaswa kukifanya ni kuwakata watu hawa kwenye maisha yako, au kwa kifupi kutokuwasikiliza wala kuwapa nafasi kabisa kwenye maisha yako.
Lakini wengi huwa hawawezi kufanya hivi, wengi huona kuna kitu wanaweza kujifunza kutoka kwa watu hawa. Na hapa ndipo ninapokuambia kwamba, huhitaji mtu wa kukukumbusha kwamba safari yako ya mafanikio itakuwa ngumu na utashindwa. Hilo liko wazi, siyo ugunduzi mpya. Na kama unaianza safari ya mafanikio ukiwa hujui hilo basi unajiandaa kushindwa.
Tatizo ni kwamba, muda wako ni mchache, mambo ya kufanya ni mengi, sasa ukitaka kumpa kila mtu nafasi, hutapata muda wa kuweka juhudi kwenye yale muhimu kwako. Hivyo chuja ni watu gani ambao hawana jipya na kutowapa nafasi kabisa. Na wa kwanza kabisa kukosa nafasi ni wale ambao kila mara wanakukumbusha jinsi safari ya mafanikio uliyochagua ni hatari, hilo tayari unalijua, huhitaji kukumbushwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,