Mpendwa rafiki yangu,

Ndoa ndiyo chemchem ya miito yote duniani. Ndoa ndiyo mama wa taasisi zote duniani hivyo kupitia ndoa tunapata yote katika jamii. Watu wengi wanaongozwa na hisia sana katika ndoa zao kuliko kutumia akili. Wanasema nyumba usiyolala huwezi kujua hila zake. Kila wito utakao chagua lazima utakutana na bwana changamoto yaani hakuna maisha ambayo utasema utaishi bila kukutana na changamoto hivyo jiandae unapotaka kuingia kwenye maisha ya wito wa ndoa changamoto ni kitu cha kawaida tu.

Wanandoa siku hizi wengi wanajikuta wanavumilia maisha ya ndoa badala ya kufurahia, hii yote ni kwa sababu ya kushindwa kufuata misingi ya ndoa.  Ndoa ina misingi yake kama ilivyo fedha, fedha usipofuata misingi yake lazima itakuadhibu vibaya.

Ndoa yoyote yenye ubinafsi ni dalili ya kwanza ya ndoa isiyokuwa na uhai. Ubinafsi ni mbaya sana, ubinafsi ndiyo unafanya dunia kuwa hovyo, ubinafsi katika ndoa ndiyo shetani anayemaliza ndoa nyingi.

Watu wengi wanaishi kibinafsi sana katika ndoa na hii hali ya ubinafsi ni zao la ndoa iliyokosa umoja. Ndoa ambayo imekosa umoja lazima itakuwa ina ubinafsi wa kutosha. Wanandoa wanaishi kama vile siyo watu waliounganika kuendesha ndoa yao.

Image result for UNITE IN MARRIAGE

Unakuta mke au mume anafanya mambo yake kivyake bila hata kumshirikisha mwenzake. Unapoanzisha ubinafsi wowote katika ndoa lazima pia ubinafsi utazaa ubinafsi. Ukiwa ni mtu wa kumshirikisha mwenza wako katika hatua zozote unazokwenda kuchukua lazima na yeye atakushirikisha pale anapotaka kuchukua hatua fulani.

Ndivyo ilivyo upendo unazaa upendo, lakini wewe ukiwa mbinafsi hutaki mwenza wako ajue kipato chako unafikiri na yeye atakua tayari kukuambia cha kwake? Unapojitoa kwa mwenza wako ndivyo utakavyopokea pia.

Maisha ya ubinafsi katika ndoa ni ishara ya wazi kabisa ndoa hiyo haina uhai, na kama kitu hakina uhai maana yake nini? Kimekufa na kama kimekufa kinasubiri kuzikwa.  Wanandoa wanatakiwa kuishi kwa umoja na ushirikiano, kushirikiana kwenye kila eneo la maisha yao, kusiwe na siri tena ndani yenu maana hizi siri ndiyo zinaleta ubinafsi.

SOMA; Hiki Ndiyo Kitu Kidogo Kinachochangia Kuvunja Mahusiano Mengi

Wanandoa wanatengeneza tabia kisha hizo tabia zinakuja kuwatengeneza. Kuwa mwaminifu katika maisha yako, ni silaha nzuri sana, muone mwenzako kama wewe, usimtendee kile ambacho wewe hupendi kutendewa bali mtendee yale anayopenda kutendewa yeye ili mradi kiwe sahihi.

Mwandoa mmoja anapokuwa anafanya kitu bila kumshirikisha mwenzake anakuwa amejitengenezea mwenyewe tabia ya usaliti. Katika ndoa nyingi, ukitumia sheria ya asili ya karma inayosema kwamba chochote unachomfanyia mwenzako malipo yake yako hapa hapa duniani. Ukimtendea vizuri mwenzake basi tegemea kupata mazuri na kama ni mabaya tegemea kupata mabaya pia.

Mwanamke mmoja  aliwahi kuniambia kuwa mume wake aliuza baadhi ya vitu vya familia bila hata kumshirikisha,baada ya mambo kumuendea vibaya ndiyo akaja kumwambia mke wake kuwa aliuza vitu. Unapotaka kufanya jambo mwambie mwenza wako kabla hujafanya na siyo kuja kumpatia ripoti. Kumshirikisha mwenzako ni rahisi sana lakini matokeo ya kutomshirikisha yana gharama kubwa sana.

Unapokataa kumshirikisa mwenzako ndipo anaanza kuibua mambo mengi ndani yake kwa kuanza kujipa tafsiri mbalimbali kwa kile ulichofanya. Iweje anifanyie kitu hiki, kwani kanionaje mimi na mengine mengi yanayofanana na hayo.

Hatua ya kuchukua leo; usiwe mbinafsi katika ndoa yako, kuwa na umoja na mshirikiane na mwenzako kwenye kila hatua ya maisha yenu mnayokwenda kuchukua. Uhai wa ndoa unaletwa na upendo, upendo ndiyo unaweza kuleta yote mazuri katika ndoa.

Hivyo basi, ndoa ikiwa na upendo inataa furaha, amani katika ndoa. Kinyume na hapo ndoa lazima itazaa chuki na ndoa ikishakuwa na chuki lazima itazaa mauti.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana