Inapokuja kwenye utajiri, wengi huwa na sababu nyingi kwa nini hawajaweza kuufikia utajiri.
Wengi husema wamejaribu sana lakini siyo bahati yao.
Wengine hutoa lawama kwa wazazi kwa kutowapa misingi sahihi au elimu bora.
Wengine hulaumu uongozi na hata mazingira au hali ya hewa kuwarudisha nyuma.
Na wapo ambao husingizia majukumu waliyonayo, labda ya kifamilia au mengine, kama kikwazo kwao kufikia utajiri.
Lakini hizo zote siyo sababu sahihi zinazomzuia mtu kufikia utajiri. Hizo ni sababu za kujibembeleza, sababu za kujionea huruma na kutokutaka kuukabili ukweli wa kinachokuzuia usipate utajiri.
Zipo sababu tatu sahihi za kwa nini mtu hujawa tajiri.
Sababu ya kwanza; sitaki kuwa tajiri. Hii ni sababu sahihi, wengi hawataki kuwa matajiri, kwa sababu ambazo huenda wanajua au hawajui. Lakini kwa namna wanavyoishi maisha yao, jinsi wanavyofanya kazi au biashara zao, unaona wazi kwamba hawajajitoa kweli kufikia utajiri. Wanafanya kawaida sana na hawana ndoto zozote kubwa.
Sababu ya pili; natamani kuwa tajiri, lakini nina vipaumbele vingine. Kama huwezi kuacha baadhi ya vitu unavyopenda kufanya lakini havichangii kwenye utajiri wako, hiyo ni sababu halisi kwa nini hufikii utajiri. Kama kuna kitu chenye umuhimu zaidi kwako kuliko kazi au biashara unayofanya basi hiyo ni sababu kwa nini siyo tajiri. Ili kuwa tajiri kweli, kipaumbele cha kwanza kinapaswa kuwa kwenye shughuli inayokuingizia kipato.
Sababu ya tatu; sina akili za kutosha kufikia utajiri. Hapa wengi hujiona ni wajinga sana au hawana maarifa sahihi ya kufikia utajiri. Na hivyo hukubali umasikini walionao na kuona utajiri umetengwa kwa ajili ya watu wachache. Lakini huu siyo ukweli, utajiri upo wazi kwa yeyote anayeutaka kweli, aliye tayari kujitoa na kujituma sana.
Rafiki, ondokana na sababu hizi tatu na utaweza kupiga hatua kuwa kwa upande wa fedha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,