#MAKINIKIA; Seneca Kuhusu Maisha Yenye Furaha (On The Happy Life)

“Kila mtu anapenda maisha yenye furaha, lakini inapokuja kwenye kitu gani kinacholeta maisha kwenye furaha, wengi wapo gizani.” Hivi ndivyo Mwanafalsafa Seneca anavyoianza insha yake aliyoiandika kwa kaka yake Gallio kuhusu maisha yenye furaha.

Seneca anaendelea kusema, “kadiri mtu anavyokaza mwendo kuyafikia maisha yenye furaha, ndivyo anavyozidi kwenda mbali na furaha. Kwa kuwa kukaza mwendo ukiwa haupo kwenye njia sahihi, unachofanya ni kupoteza zaidi.”

How-to-be-happy-10-most-practical-ways-to-live-a-happy-life

Katika Insha hii, Seneca amejadili kwa kina sana mambo yanayochangia kwenye maisha ya furaha, mambo ambayo yanaanzia ndani yetu na siyo nje yetu. Tofauti na wengi wanavyofikiri kwamba watakuwa na furaha wakishakuwa na mali, Seneca anatuambia kwamba mali hazileti furaha. Na pia tofauti na wengi wanaoamini kwamba ukiwa mwanafalsafa hupaswi kuwa na utajiri, Seneca anasema hakuna ubaya wowote kwa mwanafalsafa kuwa tajiri, iwapo utajiri huo ameupata kihalali na iwapo kama ukipotea hataumia kwa vyovyote vile.

Karibu kwenye mafunzo haya ya uchambuzi kutoka kwenye Insha ya Mwanafalsafa Seneca inayoitwa On The Happy Life, hapa nimekushirikisha yale muhimu sana kufanyia kazi kwenye maisha yako, ili uwe na maisha bora na yenye furaha.

 1. Hatua ya kwanza ya kuwa na maisha yenye furaha ni kujua nini hasa unachotaka, wapi unakotaka kufika, kisha kujua njia sahihi ya kufika unakopata kufika. Ukishajua unachotaka na ukaijua njia sahihi, kazi yako ni kukaa kwenye njia hiyo sahihi na kuweka juhudi mpaka ufike unakotaka kufika.
 2. Chagua mtu ambaye ameshafika kule unakotaka kufika wewe, na mtumie kama kiongozi wako, kama mtu utakayejifunza kwake kupitia hatua alizopiga mpaka kufika kule alikofika, ambapo ndiko unataka kufika wewe pia.
 3. Ukishajua njia sahihi, unapaswa kukaa kwenye njia hiyo na kuepuka njia nyingi zinazotamanisha utakazokutana nazo mbele yako. Maana wengi watakuja kwako na njia zinazoonekana ni nzuri, lakini zitakuwa siyo njia sahihi kwako.
 4. Ili kuwa na maisha yenye furaha, unapaswa kufanya kile ambacho ni sahihi na muhimu kwako kufanya, na siyo kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Unapaswa kuwa tayari kwenda kinyume na kundi kubwa la watu, kwa sababu mara nyingi kinachofanywa na wengi siyo kilicho sahihi. Kuwa tayari kusimama mwenyewe na kwenda kinyume na kile kinachofanywa na kila mtu.
 5. Tafuta kitu ambacho ni kuzuri kwa ndani na siyo chenye mwonekano mzuri wa nje. Watu wengi huwa wanahangaika na mwonekano wa nje, lakini ndani kunakuwa tupu. Wewe kazana na uzuri wa ndani na siyo mwonekano wa nje pekee.
 6. Maisha ya furaha ni maisha ambayo yanaendana na asili, maisha ambayo mtu anaishi kwa asili yake na kufuata kanuni za asili. Kwa sababu huwezi kuzivunja kanuni hizi na ukabaki salama.
 7. Mtu mwenye furaha ni yule ambaye kwake hakuna kitu kizuri wala kibaya, bali kuna fikra nzuri na mbaya. Hapa mtu haweki uzuri au ubaya kwenye kile kinachofanyika, bali uzuri au ubaya ni tafsiri ya fikra zake. Hivyo mtu anajijengea maadili mema ambayo yanamwezesha kutafsiri uzuri kwenye kila kinachotokea.
 8. Maisha mazuri ni yale ambayo hayaathiriwi na raha wala maumivu. Watu wengi wanasukumwa na nguvu hizo mbili, wanafanya kitu ili kupata raha, au kuepuka maumivu. Lakini raha na maumivu huwa vinakwenda pamoja, kamwe haviachani. Hivyo chochote unachofanya ili kupata raha, baadaye kinazalisha maumivu. Hivyo furaha ya maisha haipaswi kutegemea kwenye kupata raha, kwa kuwa mwisho wa raha ni mwanzo wa maumivu.
 9. Maisha yenye furaha ni yale yaliyojengwa kwenye misingi sahihi ya haki na maadili mema, misingi isiyobadilika wala kuvunjika, haya ndiyo maisha yenye uhuru kamili.
 10. Hakuna anayeweza kuwa na maisha ya furaha kama hana afya njema, hivyo afya ni msingi muhimu sana kwenye maisha bora na yenye furaha.
 11. Ili kuwa huru na kuwa na maisha yenye furaha, unapaswa kujitegemea wewe mwenyewe na kutokutegemea kitu chochote ambacho kipo nje yako. Unapaswa kutumia akili yako kufanya maamuzi na kupokea matokeo yake. Unapaswa kuweka kujiamini kwako kwenye kujifunza na kuendelea kujifunza ili kuwa na maarifa sahihi mara zote.
 12. Kuwa na maisha yenye furaha ni kuchagua kuishi kwa msingi wa wema, kuwa na tabia njema kwako na kwa wengine. Kufanya yale ambayo ni sahihi mara zote na kuepuka kufanya vitu kwa kusukumwa na tamaa au kupata raha. Kufanya ubaya ni kwa tamaa ya kupata raha ni kuharibu maisha yako ya furaha.
 13. Maisha ya furaha siyo kutokukosolewa na wengine, bali kupuuza wale wanaokukosoa, hasa pale wanapokuonesha kwamba unachofanya ni tofauti na unachosema. Pale watu wanapokuonesha kwamba unaishi kinyume na misingi unayoihubiri. Hilo lisikuondolee furaha ya maisha, kwa sababu unapojiwekea misingi ya maisha haimaanishi ndiyo umeshaweza kuifuata kwa asilimia mia moja, badala yake ni mwongozo wako, ambao kila wakati utajitahidi kuufuata na hata kujipima kwa mwongozo huo. Unapata furaha kila unapokaribia kuishi kulingana na msingi wako. Huku ukijua hujakamilika, hivyo kila siku ni nafasi ya wewe kuwa bora zaidi.
 14. Maisha mazuri siyo kuwa na mali na utajiri, wengi hufikiri ukishakuwa na mali na utajiri basi utakuwa na maisha yenye furaha. Lakini wanachokuja kugundua ni kwamba kadiri wanavyopata mali zaidi ndivyo maisha yao yanakosa uhuru zaidi. Maisha yenye furaha ni yale ambayo hata kama una mali nyingi, kama zitapotea zote hautatetereka hata kidogo. Hapa unakuwa umezimiliki mali na siyo mali kukumiliki wewe. Wengi wanaopata mali wanakosa uhuru wa maisha kwa sababu wanahofia kupoteza hata kidogo, na hili linawafanya wawe na maisha yanayoonekana mazuri kwa nje, lakini kwa ndani hawapo huru.
 15. Hakuna ubaya wowote kwa mwanafalsafa kuwa na utajiri, wala hakuna ubaya kwa mtu yeyote kuwa na utajiri, kama amepata utajiri huo kwa njia ambazo ni halali, kama hajamwibia yeyote na wala hajamuumiza yeyote kwenye kupata utajiri huo. Kwa kupata utajiri kwa njia sahihi ni kitu kizuri kwa wengine pia kwa sababu utajiri huo utawasaidia na pia wewe utakuwa hamasa kwao kupiga hatua pia.
 16. Kipimo cha kujua kama utajiri umepatikana kwa njia sahihi ni pale mtu anapoweza kutangaza hadharani kama kuna yeyote ana kitu anachonidai au nimechukua kwake basi aje kukichukua sasa kutoka kwangu. Kama hakuna anayejitokeza basi utajiri huo umepatikana kwa njia sahihi. Lakini kama watakuja watu, wakiwa na ushahidi sahihi kwamba uliwachukulia vitu vyao kwa njia ambayo siyo sahihi, utajiri ulionao siyo wako, bali umeiba kwa wengine.
 17. Tofauti ya utajiri kwa mwanafalsafa na kwa mtu wa kawaida ni hii; mwanafalsafa anamiliki utajiri na kuutumia kwa njia sahihi, na unapoondoka, hakuna kinachobadilika kwenye maisha yake. Lakini kwa watu wa kawaida, wanamilikiwa na utajiri, utajiri unawatumia kufanya yale ambayo siyo sahihi na wanapopoteza utajiri huo maisha yanavurugika sana, wengine wanakuwa tayari hata kukatisha maisha yao. Kwa mwanafalsafa utajiri ni kitu ambacho ni kizuri kuwa nacho, lakini hata kisipokuwepo maisha yanaendelea, kwa mtu wa kawaida utajiri ndiyo maisha yenyewe, na usipokuwepo basi hakuna maisha.
 18. Usipoteze muda wako kwenye kuhukumu wengine, hasa kwenye kutafuta makosa kwenye maisha yao, badala yake angalia kipi kizuri ambacho mtu anafanya na unaweza kujifunza kwake. Kwenye maisha watu wengi wamekuwa wanapenda kuangalia makosa ya wengine ili kujidhibitishia kwamba licha ya watu hao kupiga hatua, wana mapungufu makubwa, lakini hilo halitakuwa na msaada kwako. Kila aliyepiga hatua kuna vitu vizuri anavyofanya, ambavyo unaweza kujifunza na wewe ukawa bora sana. Jifunze mazuri ya wengine na yatumie kupiga hatua zaidi.
 19. Maisha yenye furaha ni maisha yenye maandalizi wakati wote, wanajeshi huwa wanafanya maandalizi ya vita wakati ambapo kuna amani. Hivyo na wewe unapaswa kufanya maandalizi ya hali ngumu wakati ambapo una hali nzuri. Mfano licha ya kuwa na mali na kuweza kupata chochote unachotaka, mara kwa mara ishi kama mtu asiyeweza kupata kile anachotaka. Licha ya kuwa na kitanda kizuri, mara kwa mara unaweza kuchagua kulala chini. Licha ya kuwa na gari binafsi, mara kwa mara unaweza kuchagua kutumia usafiri wa uma au hata kutembea kwa miguu kama wasioweza kumudu hata usafiri wa uma. Kufanya mazoezi ya aina hii siyo tu utakuweka imara pale unapopoteza unachomiliki, bali pia itakufanya uthamini zaidi kile unachomiliki. Unaweza kuwa umeshazoea sana kitanda chako, lakini siku moja ukilala chini, siku unapolala tena kwenye kitanda chako utashukuru mno.
 20. Maisha ya furaha ni matokeo ya mtu kuyaelewa maisha yako na kuishi kwa asili yake, kujijua wewe mwenyewe kwa uwezo ulionao na kujua wapi unataka kufika, kisha kukaa kwenye njia sahihi ya kufika unakotaka kufika. Baada ya kuwa kwenye njia sahihi, unachopaswa kuweka ni juhudi na kujifunza kwa waliokutangulia, huku ukiutumia utajiri na siyo utajiri kukutumia. Na kutokupoteza muda wako kuhukumu maisha ya wengine, badala yake kujifunza kutoka kwenye mazuri ya wengine. Na kwa kila unachopata kwenye maisha, kujua unaweza kukipoteza wakati wowote na hivyo kutokung’ang’ana na chochote. Hivi ndivyo unavyoweza kuwa na maisha yenye furaha, kitu ambacho kinawezekana kwa kila mmoja wetu. Chagua leo kuishi maisha ya furaha.

Rafiki, huu ndiyo msingi mkuu wa maisha ya furaha kutoka kwa mwanafalsafa Seneca, weka mafunzo haya kwenye maisha yako ili uweze kuwa na maisha bora na yenye furaha.

Uchambuzi huu wa kitabu umeandaliwa na Dr. Makirita Amani.

Dr Makirita ni daktari wa binadamu, kocha wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali. Kuendelea kupata chambuzi hizi za vitabu kwenye TANO ZA JUMA, hakikisha unajiunga na channel ya TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye mtandao wa telegram.

Kujiunga ni bure kwa juma la kwanza, kisha baada ya hapo unachagua kulipa tsh elfu moja kwa juma, au elfu tatu kwa mwezi au elfu 30 kwa mwaka. Kwa maelezo zaidi tuma ujumbe kwenda namba 0717396253, ujumbe utumwe kwa njia ya telegram pekee.

Karibu sana.