Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio yetu yanawategemea sana watu wengine. Nimekuwa nasema kwenye mafanikio hakuna jeshi la mtu mmoja, kwamba mtu mmoja anajitengenezea mafanikio yake mwenyewe, huo ni uongo.

Ili ufanikiwe watu wengine wanahusika sana kukuwezesha wewe kupiga hatua. Kama ni kwenye kazi basi walio juu yako, walio ngazi sawa na wewe na hata walio chini yako wana mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yako. Kwenye biashara pia wale unaoshirikiana nao, uliowaajiri na hata wateja ni sehemu muhimu ya mafanikio yako.

Hata kwenye maisha ya kawaida, maisha ya kila siku, kuanzia kwenye familia na hata kwenye mahusiano ya kirafiki, watu wote tunaokutana nao kwenye maisha yetu wana mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yetu. Mfano kama hakuna maelewano mazuri ndani ya familia, huwezi kuwa na utulivu wa kufanya vizuri kazi au biashara yako na kufanikiwa.

Licha ya umuhimu huu mkubwa wa mahusiano kwenye mafanikio yetu, watu wengi wamekuwa hawayapi mahusiano uzito mkubwa. Wengi wamekuwa wanaangalia zaidi malengo yao na kuwasahau wale wanaochangia kutimia kwa malengo yake.

Matokeo yake watu wamekuwa wanafanikiwa, lakini mafanikio yao yanakuwa kikwazo kwao kufanikiwa zaidi. Mfano mtu anayefanikiwa kwenye kazi kwa kujituma sana na kutojali wengine, au anayefanikiwa sana kwenye biashara kwa kutohangaika na mahusiano yake ya kifamilia, kiwango kidogo cha mafanikio ambacho mtu anakuwa amekipata, kinamzuia asifanikiwe zaidi. Kwa sababu mafanikio hayo yanatengeneza changamoto kubwa za kimahusiano ambazo zinamzuia mtu asifanikiwe zaidi.

Mwandishi Marshall Goldsmith kwenye kitabu chake cha WHAT GOT YOU HERE WON’T GET YOU THERE anasema watu wengi waliopata mafanikio kiasi huwa ni wabishi sana na ndiyo maana hawapati mafanikio makubwa. Anasema watu hawa wanakuwa wamefanikiwa licha ya kuwa na mapungufu kwenye baadhi ya tabia zao, sasa kwa kuwa wamefanikiwa wakiwa hivyo, wanaamini hawahitaji kufanikiwa. Na hilo ndiyo linawazuia watu wasifikie mafanikio makubwa zaidi.

what got you here

Kwa mfano mtu ambaye amefanikiwa licha ya kuwa mkosoaji wa kila jambo, anaweza kuamini kwamba tabia hiyo haina madhara yoyote kwake, lakini kwa kutokuibadili, anajizuia kufanikiwa zaidi.

Msingi mkuu wa kitabu cha Marshall ni kwamba kile ambacho umekifanya ukafika hapo ulipo sasa, siyo kitakachokuwezesha kupiga hatua zaidi. Lazima ujifanyie tathmini na kuona vitu gani vinaweza kuwa vikwazo kwako na kisha kuchukua hatua ya kubadilika. Unapobadilika ndiyo unatengeneza nafasi ya kuweza kufanikiwa zaidi.

Katika kitabu chake Marshall anatushirikisha tabia 20 ambazo zinawazuia watu wengi waliofanikiwa kufanikiwa zaidi. Tabia hizi zinahusisha mahusiano baina ya watu, ni vitu vidogo vidogo sana ambavyo unaweza kuvichukulia kawaida, lakini vina madhara makubwa kwenye mahusiano.

Karibu ujifunze tabia hizi 20 na kuona zipi umekuwa unazifanya ili uweze kuachana nazo na ufanikiwe zaidi.

 1. Kutaka kushinda kwenye kila kitu.

Watu wanaofanikiwa huwa wana msukumo mkubwa ndani yao wa kutaka kushinda na kufanikiwa. Lakini kuna wakati msukumo huu unakosa mlinganyo na hivyo mtu kujikuta anataka kushinda kila kitu na kila mtu.

Mtu anakuwa na msukumo wa kutaka kushinda hata vitu ambavyo havina maana au uzito wowote. Hata ubishani kidogo mtu atakazana mpaka ashinde.

Tatizo la tabia hii ni kwamba hitaji lako la kutaka kushinda kila kitu linawafanya watu wajenge chuki dhidi yako, hasa pale unapotaka kushinda vitu ambavyo havina maana. Hakuna mtu ambaye anapenda kukaa na mtu anayehakikisha anashinda kila kitu.

Ili tabia hii isiwe kikwazo kwa mafanikio yako, jifunze kuacha vitu vidogo vidogo visikusumbue. Usitake kushinda kila kitu, wakati mwingine mahusiano yako ni bora kuliko kushinda ubishani ambao umetokea baina yako na wengine. Kazana kushinda kwenye yale muhimu kama kufikia malengo yako, lakini usitake kushinda kila kitu hasa kinachohusisha mahusiano yako na wengine.

 1. Kuongeza thamani zaidi.

Nimekuwa nakushirikisha sana umuhimu wa kuongeza thamani kama hitaji kuu la kufanikiwa. Kwamba mafanikio yako yanatokana na thamani unayozalisha. Ukitaka kufanikiwa zaidi basi ongeza thamani zaidi.

Lakini inapokuja kwenye mahusiano, hasa kwenye maongezi mbalimbali, kuongeza thamani zaidi ni kikwazo kwa mafanikio yako. Mfano mtu amekuja kwako na wazo ambalo ameliona ni bora zaidi, na kweli unaliona ni bora, lakini wewe unapenda kuongeza thamani zaidi, hivyo unamshauri jinsi gani ya kulifanya kuwa bora zaidi. Unaweza kuona unafanya kitu sahihi, lakini sivyo upande wa pili unavyopokea. Upande wa pili unaona kama umewanyang’anya wazo lao na kulifanya kuwa lako.

Tatizo la tabia hii ni kuwafanya watu kujiona wa chini na wasioweza kufikiri kama wewe. Hili linawafanya watu wakose hamasa ya kufanyia kazi kile ambacho wamekuja nacho, hasa baada ya wewe kukibadili na kukifanya kuwa kama chako.

Kuondokana na tabia hii, jifunze kujiwekea ukomo katika kutoa thamani zaidi, hasa kwa upande wa mazungumzo au unapotoa ushauri kwa wengine. Hakikisha huwafanyi watu kujisikia vibaya au kuona wamenyang’anywa kitu chao. Kama mtu amekuja kwako na wazo zuri, mwambie hilo ni wazo zuri, lifanyie kazi na jizuie kutaka kuongeza thamani zaidi kitu ambacho kitabadili kabisa wazo hilo na mtu aone kama siyo lake tena.

 1. Kuhukumu wengine kwa viwango vyetu.

Watu wanaofanikiwa huwa wana viwango vikubwa sana kwao binafsi. Ni watu ambao huwa hawajionei huruma, wanataka kilicho bora na mara zote wanaweka juhudi ili kupata kilicho bora.

Tabia hii inawasukuma kupata matokeo bora sana, lakini pia inakuwa kikwazo kwa upande wa mafanikio. Mtu anapowapima na kuwahukumu wengine kwa viwango vyake, anawafanya wengine kujiona wa chini pale wanaposhindwa kufikia viwango hivyo. Wakati mwingine watu wanajali vitu tofauti na unavyojali wewe, hivyo kuwapima na kuwahukumu kwa viwango vyako, inawafanya waone unawalazimisha kuwa tofauti na wanavyotaka wao.

Acha tabia hii ya kuwahukumu wengine kwa viwango vyako, usitake kila mtu afikiri kama wewe na kuwa kama wewe. Wakubali watu kama walivyo na kujua kuna mchango walionao kwenye maisha yako, kazi yako au biashara yako, hii inawapa watu nafasi ya kuwa huru na kuwa tayari kushirikiana na wewe zaidi.

 1. Kutoa maoni yanayobomoa badala ya kujenga.

Katika mahusiano yetu na watu wengine, kuna wakati huwa tunatoa maoni ambayo kwetu yanaonekana ni ya kawaida na hayana madhara yoyote, lakini sivyo wengine wanavyoyapokea. Hasa yale mambo ambayo huwa tunayachukulia kama utani. Unaweza kumtania mtu na kuona ni kitu cha kawaida, lakini ndani yake ukawa umeacha jeraha kubwa.

Utani mwingi ambao huwa unafanyika maeneo ya kazi huwa unachukuliwa kama kitu kidogo na cha kawaida, lakini wale wanaotaniwa huwa inawaumiza. Wakati mwingine mtu anaweza kujibu kwa dharau, kitu ambacho kinamfanya aliyejibiwa asijisikie vizuri.

Kuondokana na tabia hii, pima sana kila neno kabla hujalitoa, jiulize je neno hili linakwenda kujenga au kubomoa. Ili kujua maneno yanayobomoa, waulize wengine kuhusu maneno ambayo umekuwa unapenda kuyatumia, na watakupa mrejesho wa jinsi maneno hayo yalivyo na madhara kwao.

 1. Kuanza na maneno ‘HAPANA’, ‘LAKINI’, ‘HATA HIVYO’.

Kuna wakati mtu anasema kitu ambacho hukubaliani nacho moja kwa moja, au unaona siyo sahihi au kingeweza kuboreshwa zaidi. Watu wanaofanikiwa huwa hawawezi kuvumilia vitu kama hivyo vipite bila ya kuongeza maoni yao ya kufanya kitu kiwe sahihi.

Hivyo matumizi ya maneno HAPANA, LAKINI na HATA HIVYO ni makubwa sana kwa wale wanaofanikiwa. Wanapokuwa hawakubaliani na kitu wanaanza na neno hapana, wanapokuwa wanataka kutoa maoni yao zaidi wanaanza na maneno lakini au hata hivyo. Maneno haya wengi wamekuwa wanayatumia sana wanapopewa maoni au ushauri na wengine, hasa pale wanapokuwa hawakubaliani moja kwa moja na maoni au ushauri huo.

Tatizo la tabia hii ni kwamba unapotumia maneno haya, ujumbe unaotoa kwa wengine ni ‘mimi niko sahihi, wewe umekosea’ kitu ambacho kinawafanya wengi kujisikia vibaya kuwa karibu na wewe. Unapowafanya watu kujiona hawapo sahihi mara zote, wanakuepuka.

Kuondokana na tabia hii acha kutumia maneno HAPANA, LAKINI na HATA HIVYO katika mazungumzo yako na wale wa karibu. Kama mtu amekuambia kitu kuhusu anachofanyia kazi yeye sikiliza na mpongeze. Kama mtu amekupa maoni juu ya unachofanyia kazi sikiliza na sema asante. Usitake kuanza kujitetea kwamba maoni aliyotoa ni sahihi, badala yake shukuru kwa maoni na kama ni mazuri yatumie kama siyo mazuri achana nayo.

SOMA; Sababu Moja Kubwa Kwa Nini Unashindwa Kutoka Pale Ulipokwama Na Njia Moja Pekee Ya Kukuwezesha Kupiga Hatua Zaidi.

 1. Kutaka dunia ijue kwamba una akili na unajua sana.

Watu wanaofanikiwa ni watu ambao wanajituma sana katika kujifunza na kuchukua hatua. Hili linawafanya waweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao. Lakini wanapoanza kupiga hatua, huwa wanapata msukumo wa kutaka kila mtu aone na kujua jinsi ambavyo wana akili, wanajua na wanavyojituma. Tabia hii pia huoneshwa sana pale mtu anapokuja na wazo jipya kwa anayefanikiwa, na yule anayefanikiwa kuona ni wazo la kawaida kwa sababu tayari alishalijua, hii inawavunja watu moyo.

Tatizo la tabia hii ni kwamba siyo kila mtu anataka kujua kwamba unajua sana au unaweza sana. Na kadiri unavyokazana kuwaambia watu kuhusu wewe, ndivyo wanavyokuchoka na kutaka kukukwepa mara zote. Unapowaonesha kwamba unajua sana wale ambao wanataka kukusaidia, wanaepuka kuja kwako na mawazo bora zaidi.

Kuondokana na tabia hii kuwa mnyenyekevu, hata kama unajua sana usitake kujionesha. Kwa wale wa karibu kwako, mtu anapokuja kwako na wazo fulani au maoni fulani, pokea bila ya kuonesha kwamba tayari unajua, hili linawahamasisha kuja kwako na mawazo bora zaidi wakati mwingine.

 1. Kuongea wakati una hasira.

Watu wanaofanikiwa ni watu ambao wanajitoa sana kwenye kile ambacho wanakifanya. Hivyo inapotokea watu wengine hawajitoi kama wanavyojitoa wao, huwa wanapatwa na hasira. Na hasira wanazozipata wanaposhindwa kuzidhibiti vizuri huwa zinaharibu kabisa mahusiano yao.

Tatizo la tabia hii ni kwamba unapokuwa na hasira, unakuwa hufikiri vizuri, hivyo chochote unachosema au kufanya ukiwa na hasira, kwa sehemu kubwa utakosea. Utafanya au kusema kitu ambacho kitaathiri sana mahusiano yako na watu wengine.

Kuondokana na tabia hii jifunze jinsi ya kudhibiti hasira zako, kwa kuepuka kufanya au kusema chochote pale unapokuwa na hasira. Japokuwa utakuwa unasukumwa kusema au kufanya kitu, jizue pale unapokuwa na hasira na utajiepusha na mengi.

 1. Mtazamo hasi au ‘ngoja nikuambie kwa nini haiwezi kufanya kazi…’

Watu wanaofanikiwa huwa wameshajaribu vitu vingi na kujifunza sana kupitia makosa waliyofanya. Hili linawafanya kuwa makini sana na vitu ambavyo wana historia ya kushindwa huko nyuma. Hivyo huwa tayari kutoa ushauri wao kwa wale wanaotaka kujaribu vitu hivyo, lakini mara nyingi ushauri huo huwa hasi. Ushauri huo huwa na lengo la kuwaonesha watu kwa nini wanachotaka kufanya hakitafanikiwa au kitashindwa. Ni njia nzuri ya kutoa tahadhari, lakini huwa inawakatisha watu tamaa na kuzima hamasa ndani yao.

Tatizo la tabia hii ni watu kukata tamaa na kuondokwa na hamasa waliyonayo pale wanaposikia maoni yako kwa nini kitu hakiwezi kufanikiwa au kufaa. Hili linawafanya watu kukuepuka au kuepuka kukupa mawazo yao mazuri kwa kuogopa kukatishwa tamaa.

Kuondokana na tabia hii acha kuwa na mtazamo hasi kwenye kila kitu wengine wanakuambia. Hata kama umewahi kushindwa wewe huko nyuma, haimaanishi na wengine pia wakijaribu watashindwa. Wasikilize watu na washauri kilicho sahihi na siyo kuwakatisha tamaa.

 1. Kuzuia taarifa zisiwafikie wengine.

Watu wanaofanikiwa, kwa kujua au kutokujua wamekuwa wakishindwa kutoa taarifa kwa watu wote wanaohusika na kile anachofanya mtu huyo aliyefanikiwa. Labda ni kuhusu majukumu ya kazi ambayo mtu anampa msaidizi wake, anashindwa kumwelekeza vizuri na hilo linamzuia asiweze kuyatekeleza vizuri.

Tatizo la tabia hii ni wengine kujisikia kama wameachwa nje au hawajaliwi kwenye kile wanachofanya. Hili linaathiri mahusiano na wale unaofanya nao kazi na kujiona kama wanatengwa.

Kuondokana na tabia hii hakikisha unatoa taarifa kamili na sahihi kwa wale wote unaojihusisha nao kwenye kazi au maisha. Kama kuna kitu mtu anapaswa kukijua basi mweleze kwa usahihi na ukamilifu. Hili linamfanya mtu kuona anaheshimiwa na kuhitajika.

 1. Kushindwa kuwatambua watu kwa usahihi.

Watu wanaofanikiwa, huwa ni watu wa viwango vya juu sana, ambao mafanikio madogo madogo hayawasukumi sana. Wao wenyewe hawajipongezi kwa hatua ndogo wanazopiga. Hivyo wanapeleka hilo kwa wengine, kwa kutowapongeza watu kwa hatua ndogo walizopiga. Wengi huona wakiwapongeza sana watu watalewa sifa na kuanza kukosea, hivyo huwa siyo watu wa kutambua na kupongeza michango ya wengine.

Tatizo la tabia hii ni watu kujiona hawathaminiwi au kuheshimiwa, na chochote wanachofanya hakina umuhimu. Hili linawafanya wakose hamasa ya kujituma zaidi.

Kuondokana na tabia hii, kuwa na tabia ya kuwatambua na kuwasifia na kuwapongeza watu kwa kila hatua wanayopiga, hata kama ni ndogo. Watu wanaposifiwa na kupongezwa, huwa wanajituma zaidi, wanakuwa na hamasa ya kuchukua hatua zaidi.

 1. Kuchukua sifa usizostahili.

Hili hutokea sana pale ambapo mtu upo juu ya wengine, wale wa chini yako wanajituma sana na kuleta matokeo mazuri, halafu wewe wa juu ndiye unayejipa sifa kwamba bila wewe mafanikio hayo yasingefikiwa. Hii ni tabia ya wengi wanaofanikiwa, huwa wanajiona ni sehemu ya mafanikio mengi yanayowahusu.

Tatizo la tabia hii ni watu kuona hawaheshimiwi wala kujaliwa, na unapokuwa mtu wa kuchukua sifa usizostahili, watu hawakuheshimu kwa hatua unazopiga, kwa sababu wanajua unategemea mafanikio ya wengine na siyo mafanikio yako.

Kuondokana na tabia hii jijengee tabia ya kuwapa watu sifa wanazostahili, hata kama wewe ndiyo chanzo kikuu cha mafanikio, kumbuka hujafanya hivyo mwenyewe. Mtambue kila aliyechangia kwenye mafanikio yako na mpongeze kwa hilo. Unapokuwa mtu wa kutoa sifa kwa wengine, wengi wanapenda kushirikiana na wewe.

 1. Kutengeneza sababu.

Pale ambapo mambo yanakwenda tofauti na tulivyotegemea, pale ambapo tunakuwa tumekosea, huwa hatupendi kukubali makosa yetu, na hivyo huwa tunatafuta sababu ya kueleza kwa nini tumeshindwa au kukosea. Pia kwa wale ambao wana tabia zisizo nzuri kwao, labda uchelewaji, uvivu na kadhalika, huwa wana tabia ya kutengeneza sababu za kutetea tabia hizo.

Tatizo la changamoto hii ni kwamba hakuna mtu anayesikiliza au kuamini sababu unazotoa. Wengi wanajua sababu unazotoa ni za kujiridhisha tu, lakini makosa uliyofanya bado watayakumbuka na kukuhukumu kwa makosa hayo.

Kuondokana na tabia hii acha kuwa mtu wa kutengeneza sababu, usitake kukimbia majukumu yako. Kubali kile kinachotokea kwenye maisha yako, kubali makosa unayofanya na kazana kuwa bora zaidi ili usirudie makosa uliyofanya.

SOMA; Siri 20 Za Kistoa Za Kuwa Na Maisha Yenye Furaha Ya Kudumu.

 1. Kushikilia mambo yaliyopita.

Wapo watu ambao hutumia mambo yaliyopita kama sababu ya kushindwa kupiga hatua fulani sasa. Labda ni hali ngumu waliyopitia, maisha magumu waliyotokea, elimu waliyokosa au fursa fulani waliyokosa huko nyuma. Kwa kutumia mambo ya nyuma kama sababu ya kutokupiga hatua au kama sababu kwa nini mtu unakosea sasa mtu unakuwa unajizuia mwenyewe kufanikiwa zaidi.

Tatizo la changamoto hii ni watu kuchoshwa na visingizio vyako vya nyuma na kukuepuka pale unapoanza kutoa visingizio hivyo. Watu wengi hawataki kujua nini kilitokea huko nyuma kwenye maisha yako, bali wanataka kujua unafanya nini sasa.

Kuondokana na tabia hii acha kabisa kusingizia mambo ya nyuma kama kikwazo kwako. Acha kujipa sababu za vitu ambavyo vimeshapita. Badala yake angalia nini unaweza kufanya sasa ili kupiga hatua zaidi. Watu wanavutiwa kufanya kazi na wewe kama unakuwa mtu unayewaonesha kesho iliyo bora kuliko jana iliyokuwa mbaya.

 1. Kuwa na upendeleo kwa baadhi ya watu.

Unapofanikiwa, unakuwa na watu wanaofanya kazi chini yako, usipokuwa makini na watu hawa, utajikuta unawapendelea baadhi na kuwatenga wengine. Ni tabia ya binadamu kupenda wale wanaokubaliana na sisi na kutokuwapenda wale wanaopingana na sisi. Tambua kwamba unapokuwa kiongozi siyo kila mtu atakubaliana na wewe, hata ufanye mambo mazuri kiasi gani. Hivyo unapaswa kuwa makini katika kutoa nafasi kwa wale walio chini yako, hakikisha unatoa nafasi kwa usawa na siyo kuwapendelea zaidi wale wanaokubaliana na wewe na kuwaacha wale wasiokubaliana na wewe.

Tatizo la tabia hii ni kuwagawa wale walio chini yako na hili linaathiri ufanyaji kazi wa ushirikiano kama timu. Pia unapokuwa mtu wa kupendelea wale wanaokubaliana na wewe, inawafanya watu waache kuwa wao na kutumia uwezo wao na badala yake wafanye vitu vitakavyowafanya waonekane wanakubaliana na wewe. Hapa unatengeneza watu wanaoigiza ili kupata nafasi unazotoa.

Kuondokana na tabia hii, ondoa kabisa hali ya upendeleo kwa wale walio chini yako. Wachukulie watu wote kwa usawa, iwe wanakubaliana na wewe au hawakubaliani na wewe. Na pale unapochukua ushauri wa watu wengine au kutoa nafasi fulani, toa kwa usawa kwa wote. Watu wasiokubaliana na wewe siyo maadui wako, bali ni watu ambao wanakusaidia uwe bora zaidi. Wape nafasi na watakuwezesha kupiga hatua zaidi.

 1. Kukataa kukiri kosa na kuomba msamaha.

Katika safari yako ya mafanikio, kuna wengi ambao utawakosea kwa kujua au kutokujua. Katika kutekeleza majukumu yako ya kila siku, kuna hisia za wengine ambazo utaziumiza kwa namna moja au nyingine. Watu wanaofanikiwa hutengeneza mazingira ya aina hii kila mara, lakini kwa sababu ya mafanikio yao huona hawana haja ya kukiri kosa na kuomba msamaha. Na hili limekuwa kikwazo kwao kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao.

Tatizo la tabia hii ni kuwafanya watu wajione hawaheshimiwi wala kuthaminiwa, inawafanya waone mtu anawadharau na kuona hawastahili. Pale mtu anapokukosea halafu hakubali kosa wala kuomba msamaha, inaumiza zaidi.

Kuondokana na tabia hii tambua pale ambapo umewakosea wengine, pale unapoumiza hisia za wengine na kiri kosa na kuomba msamaha. Kuomba msamaha kunawafanya wale wanaoombwa msamaha kuona wanajaliwa na kuthaminiwa. Pia inajenga hali ya uelewano na ushirikiano.

 1. Kutokuwa msikilizaji mzuri.

Watu wanaofanikiwa ni watu ambao wanajiamini sana wao wenyewe, kwa mafanikio ambayo wameyapata, huona wanajua kuliko wengine na hivyo hakuna mtu anaweza kuwaambia nini wanapaswa kufanya. Hili linawafanya kutokuwa wasikilizaji wazuri. Kwa kukosa usikivu, watu hawa wanakosa nafasi nzuri za kujifunza kutoka kwa wengine na hata kupata michango mizuri.

Tatizo la tabia hii ni inawafanya watu waache kushirikiana na wewe. Pale ambapo huwasikilizi wengine, wanajiona hawathaminiwi, ujumbe unaokuwa unawapa ni kwamba sijali unachosema, hujui kama ninavyojua mimi na unapoteza muda wangu. Hata kama husemi hivyo moja kwa moja, hivyo ndivyo watu wanavyotafsiri tabia yako ya kutokusikiliza.

Kuondokana na tabia hii, kuwa msikilizaji mzuri, mtu yeyote anapoongea na wewe, weka umakini wako wote kwako. Waangalie watu wanapokuwa wanaonega na wewe na acha chochote unachofanya na sikiliza. Kwa kuwa msikilizaji mzuri utajifunza sana kutoka kwa wengine na wengine watakuwa tayari kukuambia yale muhimu unayopaswa kujua.

 1. Kushindwa kutoa shukrani.

Wale wanaofanikiwa huwa ni rahisi sana kusahau na kupuuza mchango wa wengine kwenye mafanikio yao. Ni rahisi kuona nguvu zao na akili zao ndiyo zimewapa mafanikio waliyonayo. Lakini ukweli ni kwamba kuna wengi wanaohusika na mafanikio ya mtu, moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Pia pale watu wanapowasifia watu waliofanikiwa, huwa wanapenda kuonesha kwamba wana mafanikio zaidi ya yale mtu anayosifia.

Tatizo la tabia hii ni kuwakatisha watu tamaa kwenye kukusaidia pale ambapo hawapati shukrani kutoka kwako. Na kwa wale wanaokusifia kwa kitu fulani ulichofanya, kama utataka kuonesha kwamba kuna mengine makubwa ambayo hawajaona, basi hujisikia vibaya na kuepuka kukusifia tena.

Kuondokana na tabia hii kuwa mtu wa shukrani, shukuru kwa kila jambo na shukuru kila mtu anayehusiana na wewe kama sehemu ya mafanikio yako. Na mtu anapokusifia kwa kitu kizuri, sema ASANTE na ishia hapo. Usiongeze neno lolote baada ya asante, la sivyo utaharibu kabisa asante yako.

 1. Kumwadhibu mjumbe.

Upo usemi kwamba mjumbe hauawi, lakini kwenye maisha ya kila siku, wajumbe wanaadhibiwa sana na hata kuuawa, hasa wale wajumbe ambao wanatoa habari mbaya. Wale wanaofanikiwa huwa wana tabia ya kuwaadhibu wajumbe kwa kujua au kutokujua. Mfano mtu anapokuja kwako na habari mbaya na ukazipuuza au kumpuuza, hapo umemwadhibu.

Tatizo la tabia hii ni watu kujifunza kutokukuambia ukweli, hasa wanapogundua kwamba hupendi kuambiwa habari mbaya au usizopenda. Hili linakunyima fursa ya kujua uhalisia wa kinachoendelea.

Kuondokana na tabia hii usiwe unawaadhibu wajumbe, wahamasishe watu kukupa taarifa kamili, iwe nzuri au mbaya na chukua hatua kwa taarifa hiyo na siyo kwa mbeba taarifa. Pia mtu anapokuka maoni hata kama yanaonesha unakosea, usimkasirikie na kumjibu vibaya, badala yake shukuru na ona kama ni maoni unaweza kufanyia kazi.

 1. Kulaumu wengine kwa makosa yako.

Wale wanaofanikiwa, huwa wanalewa mafanikio yao. Kwa mafanikio ambayo wanakuwa wamepata wanaamini hawawezi kushindwa au kukosea. Hivyo inapotokea kitu wanachofanya kimeshindwa au kuna makosa wamefanya, huwa wanatafuta mtu wa kumbebesha lawama na siyo wao.

Tatizo la tabia hii ni watu kutokukuamini na kukuona kama mwigizaji. Unapokosea kila mtu anajua umekosea, hata kama utatafuta watu wa kulaumu, lakini makosa yako yatabaki kuwa wazi.

Kuondokana na tabia hii, acha tabia ya kutafuta watu wa kulaumu, unapokosea au kushindwa kwenye chochote unachofanya, anza kujiuliza umechangiaje kukosea huko, na hatua zipo uchukue ili kutokukosea au kushindwa tena. Watu watakuheshimu na kuwa tayari kufanya kazi na wewe wakijua ni mtu wa kukubali na kubeba makosa yako.

 1. Kutaka kuwa wewe na wengine wakupokee kama ulivyo.

Wale ambao wanafanikiwa kidogo, huwa wanaamini tabia zote walizonazo ndiyo zimewafikisha pale walipo, na hivyo hawana umuhimu wowote wa kubadilika. Wanaona kama kuna wengine wanakwazika na tabia zao basi hao wanaokwazika wanapaswa kuwachukulia kama walivyo au kama hawawezi basi watajijua wenyewe. Hii ni tabia ambayo imeharibu sana mahusiano mengi ya kikazi, kibiashara na hata kwenye maisha kwa ujumla.

Tatizo la tabia hii ni watu kumchukulia yule asiyetaka kubadilika kama mtu mwenye kiburi na dharau na asiyejali kuhusu watu wengine. Hili linaathiri sana mahusiano na ushirikiano wa watu.

Kuondokana na tabia hii unapaswa kuwa tayari kubadilika kulingana na hatua unazopiga na yale unayojifunza. Kadiri unavyofanikiwa, ndivyo tabia zako zinavyowaathiri watu wengi. Unapogundua kwamba tabia fulani uliyonayo ni kikwazo kwa wengine badilika na siyo ung’ang’ane nayo kwa sababu imekufikisha hapo ulipo sasa. Kumbuka kilichokufikisha hapo ulipo sasa siyo kitakachokuwezesha kufika mbele zaidi, hivyo jifunze kila siku na kazana kuwa bora zaidi.

Rafiki, hizi ndiyo tabia 20 zinazokuzuia kupiga hatua na kufanikiwa zaidi kwenye maisha yako. Najua huwezi kuwa na tabia zote hizi 20, lakini zipo tabia 5 ambazo umekuwa unazionesha sana kwenye kazi zako, biashara zako na hata maisha yako kwa ujumla. Yatathmini maisha yako kwa kuangalia tabia hizo 20 na ainisha zipi ambazo umekuwa unaziishi zaidi na anza mkakati wa kubadili tabia hizo ili uweze kufanikiwa zaidi ya hapo ulipo sasa.

Kwenye TANO ZA JUMA hili la 21, nakwenda kukushirikisha uchambuzi wa kina wa kitabu hiki cha What Got You Here Won’t Get You There, ambapo tutajifunza hatua saba za kubadili tabia ambazo zimekuwa kikwazo kwetu kufanikiwa. Pia kwenye #MAKINIKI tutakwenda kujifunza jinsi ya kujifanyia tathmini na kujua tabia zipi zinakukwamisha kupiga hatua zaidi.

Kupata uchambuzi wa kina wa kitabu hicho, kitabu chenyewe na mafunzo ya ziada kutoka kwenye kitabu hicho (#MAKINIKIA) hakikisha umejiunga na CHANNEL YA TANO ZA JUMA kwenye mtandao wa telegram. Kama bado hujajiunga tuma ujumbe sasa wenye maneno TANO ZA JUMA kwa kutumia telegram app kwenda namba 0717396253 na utaunganishwa. Ni bure kwa wiki moja na baada ya hapo unalipa elfu moja kila wiki.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge

cropped-mimi-ni-mshindi