#TANO ZA JUMA #21 2019; Unajizuia Kufanikiwa Zaidi, Jijengee Tabia Bora Kwa Mafanikio Makubwa, Tabia 20 Zinazokuzuia Kufanikiwa Zaidi, Kupoteza Fedha Kunaumiza Kuliko Kupata Na Dalili Kuu Ya Watu Wasiosaidika.

Rafiki yangu mpendwa,

Zawadi kubwa kabisa tuliyokuwa nayo kwenye maisha yetu, zawadi ya muda wa juma la 21 inatuacha. Muda ni zawadi ambayo tunapewa kwa usawa watu wote, lakini jinsi tunavyotumia muda huu ndiyo kunatutofautisha. Wapo wanaotumia muda wao vizuri na kupiga hatua kwenye maisha yao, na wapo wanaoupoteza kwa mambo yasiyo muhimu na kujirudisha nyuma.

Ni imani yangu wewe rafiki yangu, umetumia vyema muda wako wa juma hili la 21 la mwaka 2019, kwa kujifunza na kuchukua hatua kwenye kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Katika kumaliza juma hili bora kabisa ambalo tumekuwa nalo, nimekuandalia tano za juma kutoka kwenye kitabu kinachozungumzia jinsi tabia zetu zinavyoathiri mafanikio yetu. Kitabu hiki kinaitwa What Got You Here Won’t Get You There: How Successful People Become Even More Successful ambacho kimeandikwa na Marshall Goldsmith

what got you here

Kwenye makala hii ya tano za juma tunakwenda kujifunza jinsi ya kutengeneza tabia bora zitakazotuwezesha kufanikiwa zaidi. Moja ya vitu vinavyotuzuia kufanikiwa zaidi ni tabia zetu wenyewe, ambazo kwetu zinaweza zisionekane tatizo, lakini kwa wengine ni tatizo kubwa.

Karibu sana rafiki kwenye tano za juma, tujifunze kwa kina jinsi ya kuacha kujizuia kufanikiwa zaidi.

#1 NENO LA JUMA; UNAJIZUIA KUFANIKIWA ZAIDI.

Mtu mmoja amewahi kusema kama unamtafuta mbaya wako kwenye maisha, kama unataka kumwona mtu ambaye anakuzuia usipige hatua, basi simama mbele ya kioo. Na yule utakayemwona kwenye taswira ya kioo, ndiye adui namba moja kwako, ukiweza kukabiliana na huyo, utaweza kufanikiwa zaidi. Naamini umeshajua adui yako ni nani, ni wewe mwenyewe.

Kwenye kitabu cha juma hili, mwandishi anatuambia kwamba kile tulichofanya siku za nyuma kikatufikisha hapa tulipo sasa, siyo kitakachotuwezesha kupiga hatua zaidi. Kwa maneno mengine ni kwamba, unaweza kuchukua hatua fulani mwanzoni na ukapiga hatua sana, lakini ukafika mahali hupigi tena hatua, kwa sababu unaendelea kufanya yale uliyozoea kufanya. Katika hali kama hii, unahitaji kubadilika kama unataka kupiga hatua zaidi.

Na mwandishi anatuambia kitu kimoja kinachotuzuia kufanikiwa zaidi ni tabia zetu binafsi, hasa zile ambazo zinawagusa wengine.

Mfano umeanzisha biashara yako, na mwanzoni unajituma sana, unafanya kazi usiku na mchana kuikuza, unaajiri watu wa kukusaidia na unataka wafanye kazi kama wewe, unawasukuma usiku na mchana na uzalishaji unakuwa juu. Biashara inaanza kuwa na mafanikio makubwa, na unaona kwamba umeshaijua kanuni ya kufanikiwa kwenye biashara. Lakini wakati huo ambapo mambo yanaonekana kwenda vizuri, tatizo linaanza kujitokeza, wafanyakazi wako hawakai muda mrefu. Kila baada ya muda mfupi wanaacha kazi. Unafikiria labda mshahara hauwatoshi, unaongeza mshahara, lakini bado hawakai. Hili linaathiri sana biashara yako na kupelekea kuanza kushuka.

Katika mfano kama huo hapo juu, ambao umekuwa unatokea kwenye biashara nyingi, tatizo linaanzia kwenye tabia za mmiliki wa biashara, ambazo zinaathiri wafanyakazi wake. Landa wafanyakazi hawaoni kama wanajalia, maoni yao hayafanyiwi kazi, hawathaminiwi kwa kazi wanazofanya na mengine mengi. Hizo zote ni tabia ambazo mwanzoni zilimwezesha mtu kufanikiwa, lakini baadaye zinakuwa kikwazo kwake kufanikiwa zaidi.

Rafiki, jikague wewe mwenyewe, kuna tabia ambazo zilikusaidia au hazikuwa na madhara sana pale ulipokuwa unaanza kazi au biashara, kwa sababu hukuwa na watu wengi wanaofanya kazi chini yako. Lakini kadiri unavyopanda cheo kwenye kazi au biashara yako inakua na unakuwa na watu wengi chini yako, ndivyo tabia zako binafsi zinavyoathiri mahusiano yako na wale walio chini yako na kukuzuia kukua zaidi.

Usizoee mafanikio, na wala usiishi leo kwa sababu ndivyo ulivyoishi jana. Badala yake jikague na kujitathmini kila siku, ni kipi unafanya vizuri na kipi unahitaji kuboresha zaidi. Na njia nzuri ni kuchukua maoni na mrejesho wa wengine kama tutakavyojifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hapo juu.

Ujumbe ninaotaka utoke nao hapa kwenye neno la juma ni huu, kama hupigi hatua kwenye maisha yako, anayekuzuia ni wewe mwenyewe na tatizo kubwa linaanzia kwenye tabia zako.

#2 KITABU CHA JUMA; JIJENGEE TABIA BORA KWA MAFANIKIO MAKUBWA.

Tabia zetu ni kikwazo kikubwa kwenye mafanikio yetu. Tunapokuwa tunaanzia chini kabisa, juhudi zetu zinatuwezesha kupiga hatua kubwa. Lakini tunavyozidi kupiga hatua, ndivyo madhara ya tabia zetu yanakuwa makubwa na kutuzuia kufanikiwa zaidi.

Kupitia kitabu chetu cha juma, What Got You Here Won’t Get You There: How Successful People Become Even More Successful mwandishi Marshall Goldsmith anatuonesha jinsi ambavyo tabia zetu zinatuzuia kufanikiwa zaidi. Anaanza kwa kutuonesha jinsi ambavyo tabia zetu zinakuwa kikwazo kwetu, kisha anatupa hatua saba za kujenga tabia bora kwa mafanikio yetu.

Karibu kwenye uchambuzi huu ambapo tunakwenda kuchambua kwa kina uongo tunaojipa kwenye tabia na mafanikio, hatua saba za kujenga tabia bora kwa mafanikio na ahadi ya kutoa kwa wale walio chini yako ili tabia zako zisiwe kikwazo kwao na kwako pia.

UONGO TUNAOJIAMBIA KUHUSU MAFANIKIO NA KWA NINI HATUPENDI KUBADILIKA.

Mwandishi anasema yapo mambo ambayo tumekuwa tunajidanganya sana kwenye mafanikio, na haya ndiyo yamekuwa yanachochea matatizo mengi tunayokutana nayo kwenye maisha.

Baadhi ya mambo tunayojidanganya kwenye mafanikio ni haya;

 1. Tunajikadiria zaidi kwenye mchango wetu kwa mafanikio ya kile tunachofanya. Tunafikiri bila sisi mafanikio yasingepatikana, huku ni kujidanganya.
 2. Tunachukua sifa ambazo hatustahili kuchukua, kazi wamefanya wengine lakini wewe kama kiongozi ndiye unayetaka upewe sifa.
 3. Huwa tunajiona tuna ujuzi wa juu kuliko wale wanaotuzunguka.
 4. Huwa tunapuuza muda na gharama ambazo tumeshapoteza kwenye miradi ambayo haizalishi.
 5. Kukuza matarajio ya mafanikio ya mradi, kuwa na mategemeo makubwa kuliko uhalisia.

Uongo huu ambao tumekuwa tunajiambia, hasa tunapokuwa viongozi kwenye kazi au biashara, unaathiri mahusiano yetu na wale walio chini yetu. Uongo huu unakuwa umetokana na mafanikio ambayo tunakuwa tumeyapata huko nyuma. Tunapopata mafanikio kidogo, huwa tunajiamini zaidi ya uhalisia. Kujiamini huku kulikopitiliza ndiyo kunawaingiza wengi kwenye matatizo na kuwazuia kufanikiwa zaidi.

Kwa nini mabadiliko ni magumu baada ya kufanikiwa kidogo.

Hakuna watu wagumu kubadilika kama wale ambao wameshapata mafanikio kidogo. Kwa sababu wanaamini wanachofanya ni sahihi ndiyo maana wakafanikiwa. Ambacho hawaoni ni kwamba kutokubadilika kwao kunawazuia kufanikiwa zaidi.

Pale ambapo mtu aliyefanikiwa kidogo anaambiwa abadilike ili kufanikiwa zaidi, mambo haya matatu hujitokeza kwenye akili yake;

Moja, anaona yule anayemwambia abadilike amevurugwa, hajui nini anachozungumza, labda wamemchanganya na mtu mwingine.

Mbili, pale anapoona kwamba mtu huyo hajavurugwa na anachosema kinaweza kuwa na ukweli, anaamua kukataa ukweli wa kitu hicho, kwa kujiambia kama ni kweli basi asingefikia mafanikio aliyonayo.

Tatu, pale ambapo kukataa ukweli kunashindikana, basi mtu anayeambiwa abadilike anaamua kumshambulia yule anayempa ujumbe wa mabadiliko, kwa kuona kwamba hana hadhi au uwezo wa kumwambia mtu aliyefanikiwa abadilike.

Imani nne zinazotufanya tufanikiwe ambazo pia ni kikwazo kwetu kubadilika na kufanikiwa zaidi.

Zipo imani nne ambazo watu wote waliofanikiwa wanazo, hizi ni imani ambazo zimewawezesha kufanikiwa, lakini pia imani hizo ndiyo zinakuwa kikwazo kwao kufanikiwa zaidi.

 1. Hii ni imani inayowafanya kuyaona mafanikio yao kwa kujilinganisha na wengine. Imani hii inamfanya mtu kujiamini na kufanikiwa zaidi. Imani hii ni kikwazo kwenye mabadiliko kwa sababu kumshawishi mtu ambaye anaamini amefanikiwa abadilike ni kutaka kumwambia aamini kwamba hajafanikiwa, kazi ambayo ni ngumu.
 2. Naweza kufanikiwa. Imani hii inawafanya waliofanikiwa kujiamini wao wenyewe na kuamini kupitia juhudi zao wanaweza kufanikiwa zaidi. Imani hii ni kikwazo kwenye mabadiliko kwa sababu kama mtu anaamini anaweza kufanikiwa kwa juhudi zake, hawezi kuona umuhimu wa kubadili tabia zake.
 3. Hii ni imani inayowasukuma wanaofanikiwa, kwa kuwafanya waone hakuna kinachoweza kuwazuia kufanikiwa zaidi siku za mbeleni. Kwa kujiamini huku, watu hawa hujikuta wanakubali au kuingia kwenye fursa au miradi mingi ambayo inakuwa kikwazo kwao. Imani hii ni kikwazo kwa sababu mtu anapokuwa anajihusisha mambo mengi kwa kuamini hawezi kushindwa, ni vigumu sana kubadilika.
 4. Nimechagua kufanikiwa. Hii ni imani inayowapa waliofanikiwa uhuru kwenye maisha yao, wanaona mafanikio ni chaguo lao, wanafanya walichochagua kufanya. Waliofanikiwa wanajali sana uhuru wao na hawapendi kulazimishwa kufanya kile ambacho hawataki kufanya. Imani hii ni kikwazo kwa sababu mabadiliko yanapotokea nje, waliofanikiwa huyakataa kwa kuona ni kupangiwa jinsi ya kufanikiwa, wakati wao wanataka kuwa huru watakavyo.

Imani hizi kuhusu mafanikio, pamoja na kuwa sababu ya sisi kufanikiwa, tunapaswa kuwa makini zisiwe kikwazo kwetu kufanikiwa. Tunapaswa kujua wakati ambapo tabia na mazoea yetu vinakuwa kikwazo kwa mafanikio yetu na kubadilika bila ya kujali mafanikio ambayo tumeshayapata. Tusikubali mafanikio kidogo tunayopata yawe kikwazo cha mafanikio makubwa zaidi tunayoweza kupata.

HATUA SABA ZA KUJIJENGEA TABIA BORA KWA MAFANIKIO MAKUBWA ZAIDI.

Ili kufanikiwa zaidi ya pale ulipofika sasa, mabadiliko ni lazima. Lakini kama ambavyo tumejifunza hapo juu, hakuna kitu kigumu kama mtu aliyefanikiwa kuamini kwamba anapaswa kubadilika. Ni rahisi kushindwa kuona madhaifu yetu wenyewe kwa sababu mafanikio yanafunika madhaifu yetu. Lakini wale wanaotuzunguka, wale tunaofanya nao kazi, tunaofanya nao biashara na hata tunaoishi nao, wanayaona madhaifu yetu kwa uwazi kabisa.

Hivyo hatua hizi saba za kujijengea tabia bora kwa mafanikio makubwa, zinatupa nafasi ya kuwatumia wengine kama njia ya sisi kubadilika na kuwa bora zaidi.

Karibu tujifunze hatua hizi saba na jinsi ya kuzitumia kwa mafanikio makubwa zaidi.

HATUA YA KWANZA; MAONI.

Hatua ya kwanza ya kujenga tabia bora kwa mafanikio yako ni kupata maoni kutoka kwa wale wanaokuzunguka. Hii ni hatua muhimu kwa sababu huwezi kuona madhaifu yako mwenyewe, lakini wengine wanayaona.

Kupata maoni ya ukweli ni changamoto sana kwa waliofanikiwa, kwa sababu kadiri mtu anavyofanikiwa ndiyo anavyopuuza maoni ya wengine, na pia watu huwa wanaogopa kutoa maoni kwa wale waliofanikiwa kuliko wao.

Njia bora ya kupata maoni ya kweli ni kutumia mfumo wa nyuzi 360, hapa unakusanya maono kwa watu wote wanaokuzunguka, walio chini yako, walio sawa na wewe na walio juu yako.

Ili kupata maoni sahihi na ya kweli, kwanza lazima uombe watu wakupe maoni yao. Na pili unahitaji kuwapa watu usiri katika kutoa maoni yao. Watu wengi wa karibu yako wataogopa kukupa maoni yao ya kweli kama yatakuumiza. Unapowapa usiri, wanakuwa tayari kukueleza ukweli jinsi wanavyokuona wewe.

Kitu kingine ni namna unavyoomba maoni hayo. Kuwauliza watu nakosea wapi, wataogopa kukuambia unapokosea. Lakini kuwauliza ni wapi naweza kuboresha zaidi, watakuwa tayari kukuambia maeneo ya kuboresha, na hapo utajua wapo unakwama.

Tumia kila njia unayoweza kupata maoni ya watu wote wanaokuzunguka kuhusu tabia zako na yale unayofanya kwa lengo la kutaka kuwa bora zaidi.

HATUA YA PILI; OMBA RADHI.

Baada ya kukusanya maoni kutoka kwa watu wanaokuzunguka, utaanza kuona picha halisi ya jinsi ambavyo watu wanakuchukulia, tofauti na ulivyokuwa unajichukulia mwenyewe. Utaanza kuona jinsi ambavyo mambo uliyokuwa unaona ni ya kawaida kwako, yalikuwa yanawakwaza wengine na hivyo kuharibu mahusiano yenu.

Baada ya kuona madhara ya tabia zako kwa wengine, ni wakati mzuri wa kuomba msamaha kwa wale wote waliokwazika na tabia ambazo umekuwa nazo.

Watu wengi ni wazito kuomba msamaha, hasa ambao wamefanikiwa, wengi huona kuomba msamaha ni kitendo cha kujidharaulisha, lakini ni kitu chenye nguvu sana katika kujijengea tabia bora na mahusiano mazuri pia.

Kuomba radhi kwa makosa uliyofanya kunawafanya wale wanaokuzunguka wajione wanajaliwa na ni wa muhimu kwako. Pia wanategemea wewe kuwa mtu mpya na hivyo kuwa tayari kushirikiana na wewe hata kama hapo mwanzo walishaacha kufanya hivyo.

Mchakato wa kuomba radhi unapaswa kuwa mfupi na usitake kuelezea au kuhalalisha chochote. Wewe sema ‘naomba radhi kwa tabia hii …. ambayo nimekuwa nayo, nitajitahidi kuwa bora zaidi siku zijazo.’ Halafu ishia hapo, usiongeze neno jingine kwa sababu litaharibu msamaha wako.

HATUA YA TATU; TANGAZA.

Kuomba msamaha ni njia ya kwanza ya kuwataka watu wajue kwamba umedhamiria kubadilika. Njia ya pili ni kuyatangaza mabadiliko yako kwa kila mtu. Unapoomba msamaha watu wanaweza kuwa na wasiwasi na wewe, wanaweza kufikiri labda unataka kuwalaghai.

Lakini unapoyatangaza mabadiliko yako, kwa kueleza ni kwa namna gani unatarajia kuwa bora zaidi ili kuondoa yale makosa uliyokuwa unafanya awali, watu wanaona umejitoa kweli kubadilika.

Iko hivi, huwa inawachukua watu muda mpaka wakuchukulie mtu wa tofauti. Kwa mfano kama watu walishakuchukulia kwamba wewe ni mtu usiyejali, hata ukianza kujali watajua unaigiza tu. Hivyo unahitaji kuweka kazi kubwa kubadili mtazamo wa watu juu ya tabia zako, na ndiyo maana eneo la kutangaza ni muhimu kwenye mchakato wako wa kubadili tabia.

Tengeneza ujumbe mfupi unaobeba nia yako ya mabadiliko na watangazie watu kila wakati kuhusu mpango wako huo. Kama ambavyo biashara huwa zinarusha matangazo yake mara kwa mara ndiyo zikubalike, unahitaji kutangaza mpango wako wa mabadiliko mara kwa mara huku ukifanyia kazi ndiyo watu wataamini kweli umejitoa kubadilika.

HATUA YA NNE; SIKILIZA.

Kusikiliza ndiyo njia pekee ya kujifunza kutoka kwa wengine. Kusikiliza ndiyo njia bora ya kuwafanya wengine waone kwamba unawajali.

Kusikiliza ni changamoto kubwa sana kwa wale waliofanikiwa. Kwa sababu muda wao ni mchache, na wana mengi ya kusikiliza kutoka kwa wengi wanaohitaji muda wao. Lakini pia kwa mafanikio yao, hujiona wanajua mengi hivyo hawana subira ya kusikiliza yale ambayo wanayajua. Hili linawakatisha tamaa wale wanaowazunguka kuwashirikisha mambo muhimu.

Jijengee tabia ya kusikiliza, mtu anapokuwa anaongea na wewe, weka umakini wako wote kwake, acha kufanya mambo mengine na msikilize. Kwa njia huu utaelewa zaidi na mtu atajiona anajaliwa zaidi.

Lakini pia kabla hujazungumza, hakikisha umesikiliza kwa umakini, umeelewa na jiulize je kile unachokwenda kuongea kinaongeza thamani yoyote kwenye mazungumzo hayo? Kama hakiongezi thamani basi kaa kimya.

Katika kujijenga kuwa msikilizaji mzuri, fuata mbinu hizi;

 1. Usimkatishe mtu wakati anaongea.
 2. Usimsaidie mtu kumalizia sentensi zake.
 3. Usiseme nilikuwa najua hilo.
 4. Usihukumu kile mtu anaongea, kama umesifiwa sema asante.
 5. Usikubali usumbufu wowote ukutoe kwenye mazungumzo yako, macho yako yawe kwa unayeongea naye.
 6. Endeleza maongezi hayo kwa kuuliza maswali sahihi, yanayomtaka mtu ajieleze zaidi na kuwa tayari kusikiliza zaidi.
 7. Ondokana na hitaji la kutaka kuonekana na wengine kwamba unajua sana kuhusu kile anachoongelea, sikiliza kama vile hujui kabisa.

Kusikiliza kwa umakini ni moja ya vitu vinavyowatofautisha wanaofanikiwa sana na wanaofanikiwa kawaida. Kuwa msikilizaji mzuri na utaweza kufanikiwa sana.

HATUA YA TANO; SHUKURU.

Shukrani ni kiungo muhimu sana kwenye mafanikio yako, kwa sababu kinawafanya watu waone unajali na kuwa tayari kushirikiana na wewe zaidi. Pia unapokuwa mtu wa shukrani, unakuwa mtu wa kuamini kwenye uwezekano zaidi.

Njia bora ya kujijengea tabia ya kushukuru ni kusema ASANTE kwa kila fursa unayoipata ya kushirikiana na wengine.

Kwa chochote ambacho mtu anafanya kwako, sema asante. Asante inaonesha umekubali kile mtu amefanya.

Asante pia ni neno zuri la kufunga mjadala wowote ule. Hata kama mpo kwenye ubishi mkali, ukisema asante, inakuwa hakuna tena mwendelezo wa ubishi huo.

Wale wanaokuzunguka unawahitaji sana kwa ajili ya mafanikio yako, hawa ni watu ambao wanahitaji kujitoa sana ili wewe ufanikiwe. Hivyo kuwashukuru ni moja ya njia ya kutambua mchango wao kwako na hilo linawafanya kuwa tayari kushirikiana na wewe zaidi.

Usikubali fursa za kushukuru wengine zikupite.

HATUA YA SITA; FUATILIA.

Baada ya kuwa vizuri kwenye kupata maoni, kuomba msamaha, kutangaza mabadiliko yako, kusikiliza na kushukuru, unahitaji kufuatilia ili kuona hatua unazopiga zinachukuliwaje na wengine.

Kumbuka mabadiliko unayofanya hukuwa unayaona wewe bali wengine, hivyo basi ili kujua mafanikio yako katika kubadilika, lazima uendelee kufuatilia wengine wanakuchukuliaje kwa hatua unazochukua.

Kufuatilia ni hatua muhimu sana katika hatua hizi saba za mabadiliko, kufuatilia kunawezesha kupima maendeleo yako, na pia kunawakumbusha watu kuhusu juhudi unazochukua ili kuwa bora zaidi.

Ni rahisi kupanga kubadilika, ni rahisi kutangaza kubadilika, lakini kuchukua hatua za kubadilika kuna ugumu wake. Hapa ndipo unahitaji kutengeneza mpango bora wa kufuatilia mabadiliko yako, ambao utakulazimisha kuchukua hatua licha ya ugumu utakaokutana nao.

Katika kufuatilia mabadiliko yako, waulize wale wanaokuzunguka wanaonaje hatua unazochukua na matokeo yake. Lakini njia hii huwa siyo bora sana.

Njia bora ya kufuatilia mabadiliko yako ni kuwa na kocha anayekufuatilia kwa karibu. Kocha huyu anakuwa anajali sana kuhusu kupiga kwako hatua na hakuruhusu kurudi nyuma. Pia kocha huyu anakusaidia kuvuka changamoto unazokutana nazo.

Hivyo unapopanga kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako, hakikisha una kocha wa karibu wa kukufuatilia na kukusimamia.

HATUA YA SABA;  KUPOKEA MAPENDEKEZO.

Hatua hizo sita zilizopita, zote zinakupeleka kwenye kubadili tabia ambayo wengine wanaiona siyo sawa kwako, ambayo wewe mwenyewe huioni. Unachukua maoni ya wengine na kisha kuyafanyia kazi.

Hatua ya saba katika mchakato huu wa kujijengea tabia bora ni kupokea mapendekezo ya wengine. Hapa unawakaribisha wengine kushirikiana na wewe kwa karibu katika kubadili tabia zako na kujenga tabia bora.

Katika kupokea mapendekezo ya wengine, unafanya vitu vinne;

Moja, unachagua tabia unayotaka kubadili au kuboresha.

Mbili, eleza nia yako ya kubadili au kuboresha tabia hiyo kwa mtu mmoja mmoja, wale wa karibu kwako ambao wanaguswa na tabia hiyo.

Tatu, muombe yule unayemweleza akupe mapendekezo mawili ya jinsi unavyoweza kuboresha au kubadili tabia hiyo.

Nne, sikiliza kwa makini mapendekezo ambayo mtu anakupa. Usihukumu, usipinge wala kukosoa mapendekezo ambayo mtu anakupa, wewe sema asante.

Watu wapo tayari kukupa mapendekezo mazuri kama utauliza na kuwa tayari kusikiliza. Na siyo lazima ufanyie kazi kila mapendekezo, lakini kwa kuwasikiliza wengine, utajifunza mambo mazuri na muhimu sana kwako.

Kupokea mapendekezo ni rahisi kuliko kupokea maoni. Watu wapo tayari kukushauri kipi ufanyie kazi kuliko kukuonesha wapi unakosea. Hivyo hatua hii ya kupokea mapendekezo inakupa fursa ya kujifunza jinsi ya kuwa bora zaidi na watu wanakuwa wakweli zaidi.

Tumia hatua hizo saba katika kubadili na kujenga tabia imara kwako kwa ajili ya mafanikio yako. Kumbuka kwamba kadiri unavyofanikiwa, ndivyo unavyoshindwa kuyaona madhaifu yako na ndivyo walio chini yako wanavyoogopa kukuambia madhaifu yako. Hivyo kama hutachukua hatua za makusudi za kujua unaendaje, utakuja kuishia kama hadithi ya mfalme aliyetembea uchi mtaani, kwa kuamini amevaa nguvu na huku wasaidizi wake wakiogopa kumwambia hajavaa nguo.

Watu wengi waliofanikiwa kwenye kazi kwa kuwa mabosi, waliofanikiwa kwenye biashara kwa kuajiri watu wengi na hata waliopata nafasi za juu za uongozi wana hatari kubwa ya kujidanganya kwa kuwa walio chini yao hawathubutu kuwaambia ukweli. Na hili ndiyo hupelekea wengi kuanguka baada ya kufanikiwa. Usikubali hili litokee kwako, tumia hatua hizi saba kujua ukweli wa mambo ulivyo na kuchukua hatua mapema.

AHADI YA KUTOA KWA WALE WANAOKUZUNGUKA ILI TABIA ZAKO ZISIWE KIKWAZO KWAO NA KWAKO PIA.

Pakiti ya sigara imeandikwa kwa herufi kubwa; UVUTAJI WA SIGARA NI HATARI KWA AFYA YAKO, hivyo unapewa tahadhari mapema ni nini utegemee kwa kutumia kitu hicho.

Sasa kila mmoja wetu ana madhaifu yake, licha ya kujitahidi kubadili na kuboresha tabia zetu, kuna madhaifu ambayo ni kama sehemu ya maisha yetu, hata tukazane kiasi gani, huwa hatuwezi kuondokana nayo.

Hapa mwandishi anatushauri tuchukue mfano wa pakiti ya sigara, ya kutoa tahadhari kwa wale wanaokuzunguka kuhusu tabia zako na udhaifu unaojua upo ndani yako.

Mfano kama huwa unakasirika haraka, licha ya kujitahidi kuzuia hasira zisikujie, ni vyema ukawajulisha wanaokuzunguka kwamba huwa unakasirika haraka na hivyo ikitokea kitu kidogo walichofanya kimekukasirisha wasijisikie vibaya, ndivyo ulivyo na baada ya muda mfupi hasira zitaisha na utarudi sawa. Tahadhari kama hii inasaidia kuimarisha mahusiano yako, na pia inawapa watu nafasi ya kukukumbusha pale unapokuwa umeingia kwenye tabia hiyo.

Kaa chini na pitia tabia zote 20 tulizojifunza kwenye makala ya juma hapo chini, kisha ona zile zenye madhara makubwa kwako na kwa wengine. Pamoja na kuweka juhudi katika kuzifanyia kazi, lakini pia watahadharishe watu kuhusu wewe na tabia hizo. Mfano kama tabia yako ni kutoa maoni kwenye kila jambo, inaweza kuwa inawaathiri sana wale walio chini yako kwenye kazi, kwa kuamini maoni unayotoa ni sheria. Sasa unapowapa tahadhari kwamba unapenda kutoa maoni sana, lakini wasichukulie maoni hayo kama sheria, badala yake watumie ujuzi na uzoefu wao kufanya maamuzi sahihi, unakuwa umewapa uhuru wa kufanya kilicho sahihi. Lakini kama hutawapa tahadhari hii, unapowapa maono wanajiambia bosi kasema hivi basi inabidi tufanye hivyo, hata kama wanajua siyo kitu sahihi kufanya.

Tengeneza sasa tahadhari kwenye zile tabia ambazo ni changamoto kwako, kisha washirikishe wale wote wanaoweza kuathiriwa na tabia hizo.

Rafiki, haya ndiyo muhimu sana ambavyo nimekuchambulia kutoka kwenye kitabu cha juma, mafunzo mengine zaidi pamoja na kitabu vitapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA. Kama hujajiunga na channel hii maelekezo yapo mwisho wa makala hii.

#3 MAKALA YA JUMA; TABIA 20 ZINAZOKUZUIA KUFANIKIWA ZAIDI.

Kama ambavyo tumeendelea kujifunza kutoka kwenye kitabu cha juma, tabia zetu ni kikwazo kikubwa kwa mafanikio yetu.

Tabia zile zile ambazo zilitutoa chini na kutufikisha ngazi fulani, ndiyo zinakuwa kikwazo kikubwa kwetu kupiga hatua zaidi kwenye maisha yetu. Bila ya kujua tabia hizi na kuzifanyia kazi, tutakazana sana lakini hatutapiga hatua. Inakuwa ni sawa na kuendesha gari, ukiwa umekanyaga mafuta na breki kwa wakati mmoja, nguvu itatumika sana, lakini gari haitasogea hata hatua moja.

Kwenye makala ya juma, nimekushirikisha tabia 20 ambazo umezoea kuziishi kila siku na zimekuwa kikwazo kikubwa kwa mafanikio yako makubwa. Tabia hizi 20 zinaathiri sana mahusiano yetu na watu wengine na hivyo kuharibu ushirikiano kwenye kazi, biashara na maisha.

Kila mtu anayetaka kufanikiwa zaidi, anapaswa kuzijua tabia hizi 20, na kujipima ni kwa kiwango gani anazo na kuzifanyia kazi.

Kama hukusoma makala hiyo ya juma, isome sasa hivi hapa, maana ndiyo kikwazo namba moja kwako kufanikiwa zaidi. Isome makala ya juma hapa; Tabia Hizi Ishirini (20) Unazoziishi Kila Siku Ndiyo Zinazokuzuia Usifanikiwe Zaidi. Zijue Na Hatua Za Kuchukua Ili Upate Mafanikio Makubwa.

Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku na utajifunza mambo mengi na mazuri kwa ajili ya mafanikio yako makubwa.

#4 TUONGEE PESA; KUPOTEZA FEDHA KUNAUMIZA KULIKO KUPATA.

Kubadili tabia ambayo umeshazoea kuiishi kila siku ni kitu kigumu mno. Watu wamekuwa wanatumia motisha mbalimbali kwao na hata kwa wengine ili waweze kubadili tabia. Moja ya motisha ambayo imekuwa inatumika ni zawadi, kwamba mtu akibadili tabia yake basi anapata zawadi, labda ni ongezeko la mshahara au kupewa bonasi fulani.

Lakini motisha hii ya zawadi imekuwa haina nguvu sana. Kwa wengi ambao wameshazoea tabia za zamani, zawadi haiwasukumi kubadilika. Mfano kama una wafanyakazi ambao wanachelewa kukamilisha majukumu yao, unaweza kuwapa motisha kwamba atakayewahi kukamilisha anapewa ongezeko la fedha, lakini wachache sana watakaokamilisha kwa muda.

Ipo motisha nyingine ambayo ina nguvu sana ya kubadili tabia, kwa sababu ni motisha inayoumiza. Motisha hii ni mtu kupoteza fedha iwapo ataendelea na tabia ya zamani. Hakuna mtu anayepoteza fedha na hivyo tishio la kupoteza fedha linawafanya watu walazimike kubadilika. Kwa mfano huo hapo juu, ukiwaambia wafanyakazi kwamba yule anayechelewa kukamilisha majukumu yake kwa muda, anakatwa fedha kwenye malipo yake, utashangaa jinsi ambavyo wote wanakamilisha kwa muda.

Tafiti za kisaikolojia zinaonesha kwamba watu wanasukumwa zaidi pale panapokuwa na hatari ya kupoteza fedha kuliko panapokuwa na uwezekano wa kupata kiasi kile kile cha fedha. Hii ni nguvu unayoweza kuitumia kwa mabadiliko yako mwenyewe.

Kwa mfano kama kuna tabia ambayo umegundua ni sugu kwako, na ambayo unajitahidi kuibadili huwezi, basi waambie watu wako wa karibu wakufuatilie kwa karibu na kila utakapofanya tabia hiyo basi wakudai kiasi fulani cha fedha.

Mfano kama una tabia ya kuwakatisha watu wakiwa wanaongea, waambie watu wote wa karibu kwamba kila unapomkatisha mtu akiwa anaongea basi akudai shilingi elfu 10. Ukishalipa watu wawili au watatu, nakuhakikishia hutarudia tena, kupoteza fedha kutakuumiza na kukushikisha adabu.

Kadhalika kwenye tabia nyingine kama ulevi au uvutaji wa sigara, kutokufanya mazoezi, kula hovyo, kutumia maneno ya matusi na kadhalika. Tabia yoyote inayokupa shida kubadili, ingiza fedha na utabadilika haraka sana.

Kama huna wa kukufuatilia kwenye mabadiliko yako ya tabia, wasiliana na mimi Kocha wako kwa wasap namba 0717396253 na nitaweza kukusaidia kubadili tabia yoyote ile kwa motisha hii ya kupoteza fedha.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; DALILI KUU YA WATU WASIOSAIDIKA.

“It’s hard to help people who don’t think they have a problem. It’s impossible to fix people who think someone else is the problem.” ― Marshall Goldsmith

Kuna watu unaweza kuwa unakazana kuwabadili sana kwenye maisha yako, unawawekea vizuri mazingira yote yatakayowasaidia kwenye kubadilika lakini hawabadiliki.

Wakati mwingine ni wewe mwenyewe, unasukumwa sana kubadilika lakini hubadiliki.

Unapaswa kujua dalili kuu ya watu wasiosaidika kwenye maisha, ili uache kupoteza nguvu zako kwa wengine.

Ukikutana na mtu ambaye anafikiri hana tatizo au anafikiri watu wengine ndiyo tatizo, basi jua hapo umekutana na mtu ambaye hawezi kusaidika. Huwezi kufanya chochote kikamsaidia mtu wa aina hii mpaka pale atakapokubali kwamba ana tatizo.

Na hili pia lianzie ndani yako mwenyewe, kama unafikiri huna tatizo, kama unafikiri watu wengine ndiyo tatizo kwenye maisha, nakuhakikishia wewe ni mzigo mkubwa kwa watu wengine. Huenda hawakuambii lakini unawapa mzigo sana.

Anza kujikagua na kujitathimini mwenyewe, anza na wale watu ambao unawalalamikia na kuwaona ni kikwazo kwenye maisha yako, na jiulize ni jinsi gani na wewe umechangia kwenye tatizo hilo. Kama ni mahusiano yako kwenye kazi, biashara na hata maisha hayajakaa vizuri, tatizo siyo watu wengine, tatizo ni wewe. Na kama hutakiri kwamba tatizo ni wewe, utaendelea kusumbuka maisha yako yote.

Upo usemi kwamba kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua, na hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye matatizo binafsi, kujua kwamba wewe ni tatizo, ni hatua ya kwanza kwako kupiga hatua na kuwa bora zaidi.

Usiwe mtu usiyesaidia, kubali pale ambapo wewe ni tatizo, kuwa tayari kubadilika na utaweza kupiga hatua zaidi.

Rafiki yangu mpendwa, hizo ndizo tano za juma hili la 21, nenda kafanyie kazi mafunzo haya ili uweze kuwa na tabia bora na mahusiano bora na wengine katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

Kwenye mafunzo ya ziada (#MAKINIKIA) ya kitabu hiki, nakwenda kukushirikisha tabia ya 21 inayokuzuia kufanikiwa, sheria nane muhimu za kuzingatia katika kubadili tabia na jinsi ya kujenga maisha yenye maana na mafanikio makubwa.

#MAKINIKIA yanapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA iliyopo kwenye mtandao wa telegram. Hakikisha umejiunga na channel hii kupata uchambuzi wa kitabu hiki na vingine vingi. Maelezo ya kujiunga na channel hii yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu

vitabu softcopy