#4 TUONGEE PESA; KUPOTEZA FEDHA KUNAUMIZA KULIKO KUPATA.

Kubadili tabia ambayo umeshazoea kuiishi kila siku ni kitu kigumu mno. Watu wamekuwa wanatumia motisha mbalimbali kwao na hata kwa wengine ili waweze kubadili tabia. Moja ya motisha ambayo imekuwa inatumika ni zawadi, kwamba mtu akibadili tabia yake basi anapata zawadi, labda ni ongezeko la mshahara au kupewa bonasi fulani.

Lakini motisha hii ya zawadi imekuwa haina nguvu sana. Kwa wengi ambao wameshazoea tabia za zamani, zawadi haiwasukumi kubadilika. Mfano kama una wafanyakazi ambao wanachelewa kukamilisha majukumu yao, unaweza kuwapa motisha kwamba atakayewahi kukamilisha anapewa ongezeko la fedha, lakini wachache sana watakaokamilisha kwa muda.

FEDHA KWA BLOG

Ipo motisha nyingine ambayo ina nguvu sana ya kubadili tabia, kwa sababu ni motisha inayoumiza. Motisha hii ni mtu kupoteza fedha iwapo ataendelea na tabia ya zamani. Hakuna mtu anayepoteza fedha na hivyo tishio la kupoteza fedha linawafanya watu walazimike kubadilika. Kwa mfano huo hapo juu, ukiwaambia wafanyakazi kwamba yule anayechelewa kukamilisha majukumu yake kwa muda, anakatwa fedha kwenye malipo yake, utashangaa jinsi ambavyo wote wanakamilisha kwa muda.

Tafiti za kisaikolojia zinaonesha kwamba watu wanasukumwa zaidi pale panapokuwa na hatari ya kupoteza fedha kuliko panapokuwa na uwezekano wa kupata kiasi kile kile cha fedha. Hii ni nguvu unayoweza kuitumia kwa mabadiliko yako mwenyewe.

Kwa mfano kama kuna tabia ambayo umegundua ni sugu kwako, na ambayo unajitahidi kuibadili huwezi, basi waambie watu wako wa karibu wakufuatilie kwa karibu na kila utakapofanya tabia hiyo basi wakudai kiasi fulani cha fedha.

Mfano kama una tabia ya kuwakatisha watu wakiwa wanaongea, waambie watu wote wa karibu kwamba kila unapomkatisha mtu akiwa anaongea basi akudai shilingi elfu 10. Ukishalipa watu wawili au watatu, nakuhakikishia hutarudia tena, kupoteza fedha kutakuumiza na kukushikisha adabu.

Kadhalika kwenye tabia nyingine kama ulevi au uvutaji wa sigara, kutokufanya mazoezi, kula hovyo, kutumia maneno ya matusi na kadhalika. Tabia yoyote inayokupa shida kubadili, ingiza fedha na utabadilika haraka sana.

Kama huna wa kukufuatilia kwenye mabadiliko yako ya tabia, wasiliana na mimi Kocha wako kwa wasap namba 0717396253 na nitaweza kukusaidia kubadili tabia yoyote ile kwa motisha hii ya kupoteza fedha.

Hii ni sehemu ya makala ya TANO ZA JUMA la 21 kwa mwaka 2019. Kusoma makala nzima ambayo imechambua kitabu kinachoitwa What Got You Here Won’t Get You There: How Successful People Become Even More Successful ambacho kimeandikwa na Marshall Goldsmith, fungua hapa; Tano Za Juma Kutoka Kitabu; WHAT GOT YOU HERE WON’T GET YOU THERE (Jinsi Watu Waliofanikiwa Wanavyoweza Kufanikiwa Zaidi.)

Usiache kusoma makala hiyo ya tano za juma, ni moja ya makala ambazo zinakwenda kukujengea msingi wa kuendelea kufanikiwa baada ya kupata mafanikio kidogo. Watu wengi wamekuwa wanakwamishwa na mafanikio kidogo wanayopata kwa sababu wamekuwa wanahofia kubadilika. Lakini mabadiliko pekee ndiyo yatakuwezesha kufanikiwa zaidi. Soma makala hii kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO