“Just as when meat or other foods are set before us we think, this is a dead fish, a dead bird or pig; and also, this fine wine is only the juice of a bunch of grapes, this purple-edged robe just sheep’s wool dyed in a bit of blood from a shellfish; or of sex, that it is only rubbing private parts together followed by a spasmic discharge—in the same way our impressions grab actual events and permeate them, so we see them as they really are.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 6.13
Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata fursa nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MATUMIZI SAHIHI YA DHARAU…
Kuna vitu ambavyo tunavitamani sana kwenye maisha yetu, tunaona bila ya kupata au kuwa na vizuri hivyo basi maisha yetu hayajakamilika.
Lakini tunapochukua muda na kuchunguza vitu hivyo kwa undani, ndiyo tunagundua kwamba havina thamani kubwa kama tunavyofikiri, na tena ni vitu ambavyo tunapaswa kuvidharau kabisa.
Fikiria kwa upande wa chakula, labda ni nyama au samaki unaona ni chakula bora zaidi, ona nyama au samaki hiyo ni mnyama aliyekufa, aliyeuawa kinyama na kuwa mzoga, kisha nyama yake ukapatiwa.
Labda ni nguo nzuri unatamani sana kuwa nayo, ione kama pamba ambayo imewekwa rangi.
Na hata ufanyaji wa mapenzi, ona kama msuguano wa sehemu za siri ukifuatiwa na kutokwa na majimaji.
Kwa kuangalia vitu kwa uhalisia wake, tunapata nafasi ya kuvipa uzito sahihi na kutoruhusu vivuruge maisha yetu.
Haimaanishi kwamba hutafurahia tena vitu hivi au hutataka kuwa navyo, bali utaviona kwa uhalisia wake.
Kwa sababu inafika hatua watu wanaharibu kabisa maisha yao kwa sababu ya vitu hivyo vya nje, lakini unapoviangalia kwa undani, unagundua havina hiyo thamani kubwa kukinganisha na kuharibu maisha yetu.
Kitu chochote ambacho kinakupa tamaa ya kufanya, au unachojiambia maisha hayawezi kwenda bila ya kuwa nacho, hebu kiangalie kwa undani, hebu angalia mzizi wake na utaona ni jinsi gani kilivyo kitu cha kudharaulika.
Haya ndiyo matumizi sahihi ya dharau, ambayo yanatuwezesha kuielewa thamani halisi ya kitu na kulinda amani na utulivu wetu wa ndani.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kwenda kutumia dharau kwa usahihi, ili kuweza kuiona thamani halisi ya kitu na kutokuruhusu chochote kikuvuruge.
#AngaliaThamaniHalisiYaKitu, #HakunaChenyeThamaniYaKukuvuruga, #HakunaAmabchoUkikosaMaishaYatakwama
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha