“If anyone can prove and show to me that I think and act in error, I will gladly change it—for I seek the truth, by which no one has ever been harmed. The one who is harmed is the one who abides in deceit and ignorance.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 6.21

Ni bahati ya kipekee sana kwetu kuiona siku hii nyingine mpya,
Siyo kila aliyepanga kuiona siku hii amepata nafasi hii.
Hivyo ni wajibu wetu kwenda kuitumia vyema siku hii, kwa kuweka vipaumbele na kuviishi, kutokuruhusu nguvu na muda wetu kwenda kwa yasiyo muhimu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari HAKUNA UBAYA KWENYE KUKOSEA…
Kama mtu akikuonesha kwa ushahidi kabisa kwamba unakosea kwa unachofanya, unachoamini au kusimamia, ni wajibu wako kujifunza kilicho sahihi na kubadilika.
Hakuna ubaya wowote kwenye kukosea, hakuna anayejua kila kitu na kila siku ni fursa mpya ya kujifunza kwa kila mmoja wetu.

Lakini hivi sivyo wengi wanavyoendesha maisha yao,
Wengi hawapendi kuambiwa wanakosea, hivyo huendelea kufanya kile walichozoea kufanya, hata kama hakileti matokeo mazuri.
Wengi ni wabishi sana wanapokuwa upande wa kukosea kuliko wanapokuwa upande ambao ni sahihi.
Na wengi huchagua ni kwa mtu gani wanaweza kujifunza na vitu gani vys kujifunza.

Wewe usiingie kwenye mtego wowote katika hiyo,
Weka kujifunza kuwa kipaumbele kwako na yeyote anapokuonesha kwa ushahidi kwamba unakosea, ni wajibu wako kubadilika.
Usichague nani unaweza kujifunza kwake na nani huwezi kujifunza, kuwa tayari kujifunza kwa kila mtu.
Na usiwe na msimamo wa kijinga, kwa kuwa tu umeshazoea kufanya kitu basi inabidi uendelee kufanya, kama siyo sahihi unajipoteza.

Na mwisho kabisa, kila mtu anakosea, kila mtu ana sehemu ya kujifunza na kuwa bora zaidi.
Hivyo usijisikie vibaya pale mtu anapokuambia umekosea, badala yake ni kuchunguza ukweli wa kauli yake hiyo, kuangalia ushahidi anaokupa na kisha kuchukua hatua sahihi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa tayari kujifunza na kubadilika pale unapokuwa umekosea.
#HakunaUbayaKwenyeKukosea, #HakunaAliyekamilika, #KujifunzaHakunaMwisho

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha