Ubongo wetu unapenda sana uhakika, wa mambo tuliyonayo sasa na hata yatakayotokea baadaye. Na hapa ndipo huwa tunapenda kutabiri mambo yatakayotokea baadaye.

Kwa utabiri huu, tunajipa uhakika sasa, lakini tunajiweka kwenye nafasi ya kuumia zaidi baadaye. Kwa sababu wote tunajua ya kwamba hakuna utabiri wowote wenye uhakika wa asilimia 100.

Hakuna anayejua kitakachotokea kesho, na kutumia mambo ya nyuma kama utabiri wa yatakayotokea kesho siyo tu kujidanganya, bali pia ni kujiweka kwenye nafasi ya kuumia pale mambo yanapokwenda tofauti na utabiri wetu.

Hivyo tunachohitaji ni kuwa tayari kukabiliana na chochote kitakachotokea, na kutegemea matokeo ambayo ni tofauti na matarajio yetu.

Tunapaswa kukumbuka kwamba, kitu chochote kinachoweza kutokea basi kina nafasi ya kutokea. Hivyo tusijipe uhakika wa yale tu tunayotaka, bali tujipe nafasi ya matokeo tofauti na matarajio yetu.

Punguza utabiri kwenye maisha yako na kuwa na maandalizi ya kuweza kukabiliana na chochote kinachotokea na utakuwa na maisha bora wakati wote. Kuliko kuweka matumaini yako kwenye utabiri uliojipa, mambo yakatokea tofauti na ukaumia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha