Kila sheria unayofuata kwenye maisha yako inapunguza uhuru wako. Hivyo kama unafuata kila sheria unayowekewa na wengine, huwezi kuwa huru na maisha yako.
Jamii zina sheria nyingi sana, sheria ambazo hazina hata mantiki yeyote.
Swali muhimu kujiuliza kabla hujafuata sheria yoyote unayowekewa ni watu gani walioweka hizo sheria? Je sheria hizo zina manufaa gani kwa jamii nzima kwa ujumla?
Ukihoji maswali hayo, utagundua kwamba sheria nyingi ambazo watu wanaishi nazo ni kwa sababu ya mazoea tu. Hazina manufaa yoyote na hata mtu akizivunja hakuna madhara yoyote.
Kama unataka uhuru kwenye maisha yako, hoji kila sheria na kizuizi unachowekewa. Hasa zile sheria za kijamii ambazo wengi wanafuata kwa kuwa wamezaliwa na kukuta zipo.
Njia bora kabisa ya kuvunja sheria zisizo na msingi bila ya kuleta madhara kwako ni kutoa thamani kubwa zaidi kwenye kile unachofanya. Kama unatoa thamani kubwa, hakuna atakayehoji kama unakwenda tofauti na mazoea.
Na mara zote kumbuka kufuata kila sheria ni kujinyima uhuru na kuishi maisha ya kawaida, ambayo hayana furaha wala msisimko. Huwezi kuwa na maisha bora kwa kufuata kila aina ya sheria na taratibu zilizowekwa. Hoji uhalali na umuhimu wa sheria zilizopo na siyo kuzifuata kwa mazoea.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,