Mpendwa rafiki yangu,

Watu wengi ambao wako katika mahusiano mbalimbali wanayo tabia ya kununiana pale wanapokwaza. Wako wengine wanaonuniana kwa sababu tu ya kuambiwa ukweli na mwenzake. Labda amemuonya katika jambo fulani, akawa amechukia kuambiwa ukweli huo hivyo anaanza kumnunia tena bila hata kuongea naye.

Imekuwa ni kawaida kwa watu wengi kwenye mahusiano kununiana pale wanapokuwa wamekosana. Kwangu mimi kununiana na mtu ni ujinga, chuki na wivu na sababu binafsi ndiyo zinapelekea haya yote kutokea lakini kama ingekuwa tunachukulia tu poa mambo kama haya yasingeweza kutuyumbisha.

Katika mahusiano yoyote yale, kuna watu wawili ambao hawanuniwi, hata ufanye nini hutakiwi kumnunia na utakapothubutu kumnunia utakuwa unajiweka kwenye mtego wewe mwenyewe.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Watu ambao hawanuniwi duniani kote, kwenye mahusiano yoyote ni hawa hapa wawili, unatakiwa kuwaheshimu sana kwa sababu ndiyo wanakusaidia wewe kuweza kuendesha maisha yako nao ni.

 

Bosi wako, hutakiwi kumnunia bosi wako. Bosi hakosei, anafanya kile anachokitaka hivyo kumnunia bosi wako ni ujinga wa hali ya juu.  Mtu anayekusaidia maisha yako yaende siyo mtu wa kumnunia au kumchukulia poa. Mtu ambaye anamnunia bosi wake huenda akili yake haiku sawa hivyo anatakiwa akapimwe.

Bosi wako ndiyo mteja wako namba moja kama umeajiriwa. Hivyo basi, unatakiwa kumfanyia mambo mazuri bosi wako mpaka afurahi na siyo kumnunia. Kumnunia mtu anayekusaidia kukupatia kipato cha kuweza kuendesha maisha yako ni mtu unayepaswa kumweshimu sana.

Unatakiwa ujitume sana katika yoyote ile unayopewa na bosi wako, hata kama imekwisha omba tena majukumu mengine. Kazi yako wewe ni kufanya kazi bora za kumshangaza bosi wako kwa utendaji mzuri wa kazi. Na ukishampendeza bosi wako ataweza kukulipa vizuri kwa sababu unampa thamani nzuri kwenye kazi yake.

Mtu wa pili ni mteja wako. Kama uko kwenye biashara hutakiwi kumnunia mteja wako. Iko falsafa ya mteja ambayo inasema kuwa mteja hakosei na mteja yuko sahihi muda wote. Unatakiwa kumwacha mteja afanye kile anachotaka kwa sababu katika biashara yako yeye ndiyo bosi.

SOMA; Makosa 28 Ya Kisaikolojia Unayofanya Na Yanayopelekea Wewe Kufanya Maamuzi Mabovu Yanayokugharimu.

Inapotokea mteja wako amekwenda kununua sehemu nyingine hupaswi kumnunia tena anapokuja kurudi kwenye eneo lako la biashara mfurahie kwa kurudi kwake. Mpatie tena huduma bora sana ambayo hatoweza kuipata sehemu nyingine yoyote ila kwako tu.

Kumnunia mteja wako ni ujinga wa hali ya juu, kila mtu ni bidhaa inayojiuza hivyo unapokuwa uko vizuri zaidi ndivyo utakavyowavutia watu wengi kuja kununua kwako kadiri ya thamani unayotoa.

Hatua ya kuchukua leo; usiwanunie watu hawa wawili, moja bosi wako na pili mteja wako. Uwaheshimu kwa sababu hao ndiyo wanafanya maisha yako yaende mbele na biashara yako iende. Bila hao watu hakuna maisha katika mahusiano yetu.

Kwahiyo, jenga mahusiano bora kati ya wewe na mteja  wako na bosi wako pia. Wape thamani bora sana na siku zote usiwanunie bali wachekee, kumnunia mteja na bosi wako ni sawa na kukataa fedha. Unapokataa fedha maisha yako yatakuwaje?

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana