“Turn it inside out and see what it is like—what it becomes like when old, sick, or prostituting itself. How short-lived the praiser and praised, the one who remembers and the remembered. Remembered in some corner of these parts, and even there not in the same way by all, or even by one. And the whole earth is but a mere speck.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.21
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari GEUZA NJE NDANI…
Kuna baadhi ya vitu vinatusumbua au tunavihofia kwa sababu hatujavielewa vizuri.
Kitu chochote ukikielewa vizuri hakiwezi kukusumbua wala kukutesa.
Na ili kukielewa kitu vizuri, kigeuze nje ndani.
Angalia kwenye kila kona ya kitu na utaweza kupata uhalisia wake, na hilo litapunguza hali ya kutokuwa na uhakika, ambayo inazaa hofu.
Anza sasa na kitu chochote kinachokutisha, kukupa hofu au ambacho unaona hukielewi. Kigeuze nje ndani na uweze kuona uhalisia wake, uone undani wake na uone kile ambacho siyo rahisi kuonekana.
Kwa kufanya hivi utagundua hofu unayokuwa nayo kwenye vitu ni kwa sababu hujavielewa vizuri.
Kuna kazi unaiona ni ngumu kufanya? Hebu igeuze nje ndani, angalia kila sehemu ya kazi hiyo na utaona wapi rahisi kuanzia.
Kuna watu unawaona ni wagumu kuingilika? Hebu wageuze nje ndani na utawaona ni watu ambao wana hofu zao na hata mapungufu kama walivyo watu wengine.
Kitu chochote kisikutishe wala kukusumbua katika maisha yako, geuza kila kitu nje ndani na utaona huna sababu ya kutishwa au kusumbuliwa na chochote.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kugeuza kila kitu nje ndani ili kuweza kukielewa kwa uhakika na kuchukua hatua.
#GeuzaNjeNdani, #OnaKisichoonekana, #HakunaKinachoshindikana
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha