Matatizo makubwa kwenye dunia yanasababishwa na watu kufanya vitu nusu nusu, watu kuingia kufanya kitu huku mguu mmoja upo ndani na mguu mwingine upo nje.
Watu hawafanikiwi kwenye biashara kwa sababu hawajaingia kwa ukamilifu na wazima wazima, wapo mguu mmoja nje mguu mwingine ndani. Hawajajitoa kweli kufanikiwa kwenye biashara hiyo, ikijitokeza fursa nyingine wanabadilika haraka kama vinyonga.
Hata matatizo yanayotokea kwenye mahusiano ya kila aina, na hasa mahusiano ya ndoa, ni kwa sababu watu wanakuwa hawajaingia na kujitoa kikamilifu kwa wenza wao. Wanakuwa mguu mmoja ndani mguu mwingine nje. Wanakuwa tayari kuwa na mahusiano mengine nje ya mahusiano hayo waliyonayo. Wanaweka nguvu nyingi kwenye kutafuta makosa na udhaifu wa wenzao kuliko uimara wao.
Na hata kwenye maisha ya kila siku, hakuna kitu kinachozalisha msongo kama kufanya vitu nusu nusu. Kuanza kitu na usikikamilishe, kisha kwenda kwenye kufanya kitu kingine nacho humalizi. Unaenda hivyo mpaka unajikuta umeanzisha vitu vingi na hakuna hata kimoja ambacho umekamilisha, umechoka lakini hakuna matokeo unayoweza kuyahesabu, hapo lazima upate msongo wa mawazo.
Kwa chochote unachochagua kufanya kwenye maisha yako, kifanye kwa ukamilifu, ingia mzima mzima na weka kila unachopaswa kuweka ili kukikamilisha. Hakikisha unamaliza kila unachoanza, usiachie kitu chochote katikati na kujiambia utakuja kumalizia siku zijazo, hapo unatengeneza msongo.
Kuwa na machaguo machache, lakini ukishachagua kitu, weka maisha yako yote kwenye kile ulichochagua, usiwe na mbadala bali kile ulichochagua kufanya. Kwa kuyaendesha maisha yako kwa namna hii, utaweza kufanya makubwa sana popote pale ulipo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,