#TANO ZA JUMA #17 2019; Ubongo Wako Unakupoteza, Jua Ubongo Wako Unavyofanya Kazi Na Jinsi Ya Kuutumia Vizuri, Njia Nne Za Kutuliza Akili Yako, Fedha Ni Zawadi Mbaya Na Simu Yako Inakufanya Kuwa Mjinga.

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye tano za juma hili la 17 la mwaka huu 2019. Naamini limekuwa juma bora sana kwako, juma la uzalishaji na kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako. Kumbuka juma ndiyo kipimo kizuri sana cha muda kwako kama unataka kufanikiwa. Ni rahisi kuweka malengo ya juma na kuyafuatilia, pia kujitathmini kila juma ni rahisi kuona wapi unafanya vizuri na wapi unakosea.

Kwenye tano za juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kuhusu kiungo muhimu sana kinachotutofautisha sisi binadamu na viumbe hai wengine. Kiungo ambacho kinatupa sisi nguvu kubwa ya kufikiri na kufanya maamuzi. Lakini pia kiungo ambacho wengi hatujui nguvu kubwa ambayo kiungo hiki imebeba na hivyo tumekuwa hatuitumii vizuri.

Kiungo ninachozungumzia hapa ni ubongo wetu. Na tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu kinachoitwa Your Brain at Work: Strategies for Overcoming Distraction, Regaining Focus, and Working Smarter All Day Long ambacho kimeandikwa na David Rock. Kwenye kitabu hiki, David ametumia kisa ambacho kinaakisi maisha ya kila siku ya wanafamilia ambao wazazi ni wafanyakazi wenye majukumu mengi ya kukabiliana nayo kwenye siku. Kupitia kisa hicho, David ametuonesha makosa ambayo watu tunayafanya kwa kutokuelewa jinsi ubongo wetu unavyofanya kazi, na kutupa funzo na njia bora ya kukabiliana na changamoto za maisha yetu ya kila siku.

your-brain-at-work

Hiki ni kitabu ambacho kila mtu anayeishi zama hizi anapaswa kukisoma, kwa sababu usumbufu ni mwingi, msongo wa mawazo upo juu na utulivu hakuna. Lakini yote hayo ni matokeo ya kutokujua jinsi ubongo wako unafanya kazi.

Kwenye tano za juma hili, nakwenda kukushirikisha yale muhimu unayopaswa kujua kuhusu ubongo wako, jinsi unavyofanya kazi na njia bora ya kuutumia ili kuondokana na usumbufu, kuongeza umakini na kufanya kazi zako vizuri pamoja na kuwa na utulivu siku nzima.

Karibu sana kwenye tano za juma, uujue ubongo wako na uweze kuutumia kwa manufaa zaidi kwako mwenyewe.

#1 NENO LA JUMA; UBONGO WAKO UNAKUPOTEZA.

Kitu kimoja ambacho huenda hukijui ni kwamba ubongo wako unakupoteza. Ni kitu ambacho kinaweza kukushangaza na kukustua kwa sababu umekuwa unauamini ubongo wako na kufikiri unafanya kile ambacho ni bora kwako. Lakini siyo kweli. Ubongo wako haufanyi kile ambacho ni bora kwako, bali unafanya kile ambacho ni bora kwa ubongo wenyewe.

Na kile ambacho ni bora kwa ubongo, kilikuwa na mantiki miaka elfu 5 iliyopita, ambapo mazingira yalikuwa hatari na hivyo kipaumbele cha kwanza cha ubongo ilikuwa kukulinda. Lakini kwa zama hizi, hatari hizo zimeondolewa kabisa, lakini bado ubongo unaishi kwa mazoea hayo.

Tukianza na kwenye hofu, kuna mambo mengi sana yanatupa hofu kwenye maisha yetu, lakini hofu ambayo ubongo inapata na kuuandaa mwili kwa mapambano, haiendani na uhalisia. Mfano miaka elfu 5 iliyopita, mwanadamu ambaye aliishi porini kwenye wanyama wakali, angesikia kishindo asichokielewa, ubongo uliuambia mwili upo hatarini, mwili ulizalisha kemikali za msongo ambazo zinaupa mwili nguvu ya kupambana au kukimbia. Na mtu alipata nguvu kubwa ya kupambana au kukimbia ili kujiokoa, na hilo liliwezesha binadamu kuondokana na mazingira hatarishi kwa afya yako.

Lakini kwa zama hizi, hakuna hatari kubwa ya kuliwa na wanyama wa kali, bali tuna hofu zinazotokana na vitu vya kawaida, labda kuchelewa kazini au kuongea mbele ya watu. Pamoja na kwamba hutakufa kwa kuchelewa kazini au kwa kuongea mbele ya wengine, unapokuwa na hofu, ubongo unauambia mwili kwamba upo kwenye hatari na mwili unazalisha kemikali za msongo, ambazo zinaupa mwili nguvu ya kupambana au kukimbia. Lakini hupambani wala hukimbii, hivyo kemikali hizo zinakaa kwenye mwili kwa muda mrefu na ndiyo chanzo cha msongo wa mawazo pamoja na magonjwa sugu.

Kitu kingine ambacho ubongo wako unakudanganya ni kwenye kufikiri. Ubongo ndiyo kiungo kinachotumia nishati kwa wingi kwenye mwili wako, kuliko kiungo kingine chochote. Na ubongo unatumia nishati zaidi pale unapofikiri kitu kipya, ambacho hujakizoea kabisa. Kufikiria au kufanya vitu ambavyo umeshazoea kufanya hakuhitaji nishati nyingi, kwa hiyo unafanya kirahisi. Lakini kufikiri kitu kipya, au kufanya kitu kipya, kunahitaji nishati kubwa sana na hapa ndipo ubongo unapokudanganya. Kwa sababu ubongo unafanya kazi kama ulivyokuwa unafanya miaka elfu 5 iliyopita, basi umekuwa unaepuka sana kupoteza nishati. Ubongo unapata nishati kutoka kwenye sukari pekee, sasa miaka elfu 5 iliyopita, sukari ilikuwa chakula adimu, hivyo ubongo ulikuwa ukidhibiti matumizi ya sukari, kwa kuhakikisha unakuzuia usitimie sukari yote kwa mambo yasiyo muhimu, na kuitunza kwa hali za hatari.

Kwa kuwa kipaumbele cha kwanza cha ubongo ni kutunza sukari, na kwa kuwa kufikiri vitu vipya kunahitaji nishati nyingi ambayo inahitaji kuunguzwa kwa sukari nyingi, ubongo wako umekuwa unakuzuia usifanye au kufikiri vitu vipya. Ndiyo maana ukitaka kuweka malengo makubwa ya baadaye, ambayo hujazoea, akili yako inakataa. Ukitaka kufikiria suluhisho la tatizo kubwa unalipitia, akili yako inakurudisha kwenye tatizo na huendi kwenye suluhisho. Hii yote ni kazi ya ubongo katika kulinda rasilimali zake.

Unapaswa kuujua ubongo wako ili kuweza kuvuka vikwazo hivi vikubwa ambavyo ubongo wako unakuwekea kwenye kupiga hatua.

Kwa upande wa hofu, unapaswa kujua kwamba vitu vingi unavyohofia kwenye maisha yako havina hatari kubwa kama ubongo wako unavyokuaminisha, hivyo tuliza akili yako, jipe uhalisia wa kitu unachohofia na ona hatua sahihi za kuchukua. Kwa kufanya hivi utaondokana na msongo na kuwa na maisha ya utulivu.

Na kwa upande wa kufikiri na kufanya vitu vipya, kwanza lazima uhakikishe unapanga kufikiri au kufanya vitu vipya wakati ambapo mwili na akili yako vina nguvu. Mfano asubuhi na mapema ambapo mwili wala akili havijachoka, itakuwa rahisi kwa ubongo kubeba majukumu hayo. Pia unapokuwa umechoka na akili yako inakuwa kikwazo kwako, upe ubongo wako kitu cha sukari na utakuwa tayari kutekeleza majukumu unayoupa ubongo wako. Tafiti zinaonesha watu wanapopewa vitu vyenye sukari hata kwa kiwango kidogo, huondokana na kukwama kifikra na kuweza kufanya maamuzi muhimu.

Uelewe ubongo wako ili usiwe kikwazo kwako kupiga hatua kwenye maisha.

#2 KITABU CHA JUMA; JUA UBONGO WAKO UNAVYOFANYA KAZI NA JINSI YA KUUTUMIA VIZURI.

Rafiki, ubongo tulionao sisi binadamu, ni ubongo wa kipekee sana, ubongo ambao una eneo kubwa la kufikiri na kufanya maamuzi linaloitwa PREFRONTAL CORTEX. Eneo hili halipatikani kwa wanyama wengine wote, na ndiyo linatupa sisi utashi, ni eneo tunalotumia katika kuweka malengo na mipango ambayo inatuwezesha kufanya mambo makubwa zaidi.

Lakini pia eneo hili ni changa ukilinganisha na historia yetu sisi binadamu, ni eneo ambalo linachukua muda mrefu kuendelezwa. Mfano mzuri unaweza kuuona kwa mtoto mdogo. Mtoto anayezaliwa leo anaweza kunyonya, lakini hawezi kuongea. Hii ni kwa sababu kunyonya kunadhibitiwa na ubongo wa chini, ambao unazaliwa ukiwa umeshakomaa, huu ndiyo ubongo unaodhibiti mambo ya muhimu ya mwili kama mapigo ya moyo na upumuaji. Lakini kuongea kunadhibitiwa na ubongo wa juu, ambao kwa mtoto mdogo ni mweupe kama daftari jipya, hauna kumbukumbu yoyote. Unahitaji kuanza kujenga kumbukumbu ndiyo uweze kufanya kazi.

Kutokana na uchanga huu wa ubongo wa juu, unahitaji nishati kubwa sana ili kuweza kufanya kazi, na hapa ndipo matatizo mengi yanapojitokeza. Pale ambapo nishati inakosekana au ubongo huu unakosa nafasi nzuri ya kufanya yale muhimu, mtu anajikuta akifanya mambo ambayo hajui hata kwa nini anafanya.

Kwa kuujua ubongo wako na jinsi ambavyo unafanya kazi, utaweza kuyaendesha vizuri maisha yako, kwa kuepuka mambo yanayochosha ubongo na yasiyo na matokeo na kufanya yale ambayo yanaleta matokeo mazuri.

Karibu kwenye uchambuzi huu wa kitabu cha Your Brain at Work: Strategies for Overcoming Distraction, Regaining Focus, and Working Smarter All Day Long ambacho kimeandikwa na David Rock. Kwenye kitabu hiki, tunakwenda kujifunza jinsi ubongo wetu ulivyo, jinsi unavyofanya kazi na njia za kuutumia vizuri ili tuweze kuondokana na usumbufu, tuepuke msongo, tuongeze umakini kwenye kazi zetu na kuweza kupata matokeo bora.

WEKA KIPAUMBELE KWENYE KUWEKA VIPAUMBELE.

Kila maamuzi ambayo unafanya, yanachosha ubongo wako. Kila kitu kipya unachofanya, kinatumia nishati kwenye ubongo wako na kuuchosha. Hili linafanya ubongo huo usiweze kufanya kitu kingine ambacho ni kigumu.

Kwa kujua hili, unapaswa kuweka kipaumbele kwenye kuweka vipaumbele. Yaani pangilia siku yako kwa kuanza na yale majukumu ambayo ni muhimu zaidi kabla ya kwenda kwenye yale ambayo siyo muhimu. Kwa kuanza na majukumu muhimu, akili yako inakuwa ina nguvu na utaweza kuyafanya vizuri. Lakini kama utaanza na majukumu ambayo siyo muhimu, ubongo utachoka haraka na inapokuja kwenye majukumu muhimu hutakuwa na nguvu za kuyafanya.

Epuka sana kuianza siku yako kwa kusoma na kujibu barua pepe, jumbe za wengine, kutembelea mitandao ya kijamii au kufuatilia habari. Hapa ni kuuchosha ubongo wako kwa vitu ambavyo sivyo muhimu na inapofika wakati wa kufanya kazi unajikuta unataka tu kuahirisha. Anza siku yako kwa majukumu yale muhimu, ukishayakamilisha ndiyo unaweza kufanya hivyo vingine.

FANYA JAMBO MOJA KWA WAKATI.

Watu wamekuwa wanajisifia kwamba wanaweza kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na hivyo kuokoa muda na kuwa na uzalishaji zaidi. Lakini tafiti zote ambazo zimekuwa zinafanywa, zinaonesha kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kunapunguza ufanisi, yaani mtu anayefanya mambo mawili kwa wakati mmoja, ana ufanisi mdogo kuliko anayefanya kila jambo kwa wakati wake.

Kinachopelekea ufanisi kupungua pale mtu anapofanya mambo mengi kwa wakati mmoja ni ukomo ambao ubongo wetu unao, hasa kwenye ubongo wa juu. Ubongo huu una nafasi ndogo sana ya kushikilia vitu vingi kwa wakati mmoja. Tafiti zinaonesha mtu anaweza kushikilia namba nne kwa wakati mmoja kwenye fikra zake, zaidi ya hapo anashindwa.

Kama unataka kuwa na ufanisi mkubwa, kama unataka kuwa na utulivu kwenye kile unachofanya, fanya jambo moja kwa wakati. Hasa pale inapokuwa mambo hayo ni mageni kwako na yanakutaka kufikiri vizuri.

Lakini inapokuja kwenye mambo ambayo unayafanya kwa mazoea, yaani yale ya kujirudia rudia, unaweza kuyafanya kwa pamoja. Mfano kama umekuwa unaendesha gari kila siku, kwa njia ambayo umeizoea, unajikuta unaweza kuendesha bila hata ya kufikiria sana. Hivyo unaweza ukaendesha na kusikiliza muziki au kitabu bila ya shida. Lakini siku ukiendesha njia ambayo huijui, ni vyema ukaweka akili yako kwenye kuendesha pekee, kwa sababu akili ikiwa inaendesha huku unasikiliza vitu vingine ni rahisi kupotea.

Akili yako inafanya vizuri pale unapofanya jambo moja kwa wakati, weka ratiba yako vizuri na pangilia majukumu muhimu uyafanye yenyewe bila ya kuchanganya na kitu kingine.

PALE UNAPOHITAJI KUFANYA MAMBO MENGI NDANI YA MUDA MFUPI.

Utakubaliana na mimi kwamba mambo ya kufanya ni mengi na muda tulionao ni mdogo. Hivyo kama tutasema tufanye kila jambo kwa wakati tutajikuta tunabaki na vitu vingi ambavyo hatujafanya. Na pia kwenye kazi zetu za kila siku, kuna mambo tunayofanya, ambayo huwa yanajirudia kila siku. Sasa haya ni mambo mazuri ambayo unaweza kuyafanya kwa pamoja na ukaokoa muda pamoja na kutoa uhuru kwenye ubongo wako.

Kama nilivyokuambia, ubongo wetu wa juu, unaoitwa PREFRONTAL CORTEX ndiyo unaofanya maamuzi na kuweka mipango, ndiyo unaofikiria vitu vipya na kutengeneza maono. Kitu kikishakuwa cha kujirudia, kinaondolewa kwenye ubongo huu wa juu na kupelekwa sehemu nyingine ya ubongo inayoitwa BASAL GANGLIA, eneo hili huwa linafanya vitu kwa mazoea, lina nafasi kubwa na halitumii nishati nyingi, hivyo halina ukomo mkubwa kama ubongo wa juu.

Mfano mzuri wa kuelewa hili ni kupata picha mara yako ya kwanza kuendesha baiskeli, pikipiki au gari, ulikuwa unafikiria kila kitu, nakanyagaje breki, mafuta na vingine. Lakini baada ya kuzoea unajikuta unafanya tu moja kwa moja bila hata ua kufikiria, hapo zoezi linakuwa limetoka kwenye ubongo wa juu na kwenda kwenye basal ganglia.

Sasa unachoweza kufanya pale unapokuwa na majukumu mengi ya kufanya huku muda wako ni mdogo, ni kutengeneza utaratibu unaojirudia kila siku, ambapo majukumu hayo utakuwa unayafanya kwa ubongo wa chini badala ya ubongo wa juu. Hivyo unapaswa kuwa na utaratibu wako wa siku, jinsi unavyoianza siku yako, jinsi unavyofanya kazi zako, kiasi kwamba ukishagusa kitu, basi akili inaendelea yenyewe. Hili litawezekana kwa yale majukumu ambayo yanajirudia kila siku, labda kujibu email au jumbe mbalimbali, huku ukifuatilia mkutano ambao haukuhitaji wewe kufanya maamuzi magumu. Mfano mwingine ni kuendesha gari huku unasikiliza vitabu vilivyosomwa.

Njia nyingine unayoweza kutumia ni kukusanya majukumu yanayofanana pamoja na kuyafanya kwa pamoja. Majukumu ambayo yanaendana, mfano kuwasiliana na watu kwa njia mbalimbali, unaweza kuyatengea muda wake na kuyafanya kwa pamoja.

Lakini kwa yale majukumu makubwa, muhimu na mapya, unapaswa kuyatengenea muda wake yenyewe, kwa sababu haya yanahitaji zaidi ubongo wako wa juu katika kuyafanyia kazi.

SEMA HAPANA KWA USUMBUFU.

Ubongo wetu ni rahisi sana kusumbuliwa, tunapokuwa tunafanya kazi, kitu chochote kipya kinachotokea, ni rahisi kututoa kwenye kile tunachofanya na kujihusisha na kitu hicho kipya. Ndiyo maana ni vigumu sana kufanya kazi muhimu ukiwa kwenye eneo lenye kelele, akili yako haiwezi kutulia kwenye kile unachofanya.

Upo usumbufu wa aina mbili ambao ni kikwazo kwa ubongo wako.

Kuna usumbufu wa nje, ambao unatokana na vitu vipya vya nje ambavyo ubongo unashawishika kujihisisha navyo. Simu zetu za mkononi ndiyo chanzo kikuu cha usumbufu wa nje. Tafiti nyingi zinaonesha watu hawawezi kukaa kwa zaidi ya dakika kumi bila kuangalia simu zao, kitu ambacho kinawazuia kuweka umakini kwenye kazi zao. Hivyo kama unataka kuwa na ufanisi mzuri, pale unapokuwa unafanya jukumu muhimu, zima kabisa simu yako. Au iweke kwenye ukimya na ikae mbali kabisa na wewe. Pia fanyia kazi zako eneo ambalo halina usumbufu wa watu wengine au makelele.

Aina ya pili ya usumbufu ni usumbufu wa ndani, hapa akili yako mwenyewe inakuwa inahama hama kutoka kwenye kitu kimoja na kwenda kwenye kitu kingine. Kama hutaweza kuidhibiti akili yako na kuiweka kwenye kile unachofanyia kazi, utajikuta unachoka sana lakini hukamilishi unachofanya. Njia bora ya kuondokana na usumbufu huu ni kujikamata pale mawazo yako yanapotaka kuhama na kuyarudisha kwenye kile unachofanya. Ukichelewa kujikamata na ukajikuta mawazo yameshahamia sehemu nyingine, inakuwa kazi kubwa kuyarudisha kwenye kazi kuu. Kuwa mlinzi wa mawazo yako na yakamate pale yanapotoroka na uyarudishe kwenye jukumu kuu.

KUTAUFUTA UKANDA WA UFANISI WA HALI YA JUU.

Huwa tunaona msongo wa mawazo ni kikwazo kwetu kupiga hatua, tunatamani tungeweza kuondokana kabisa na msongo. Lakini ubongo wetu hauwezi kufanya kazi kama hatuna msongo. Bila ya msongo kabisa, ubongo hautakuwa na kitu cha kuusukuma kuchukua hatua.

Hivyo ili uweze kuchukua hatua unahitaji kuwa na kiwango fulani cha msongo. Kiwango hiki hakipaswi kuwa chini sana, kwa sababu kikiwa chini hutapata msukumo. Na pia kiwango hiki hakipaswi kuwa juu sana kwa sababu kitakuzuia usiweze kuchukua hatua.

Mfano mzuri wa kuelewa hili ni kwenye kufanya jambo ambalo lina tarehe ya ukomo. Mfano umepewa kazi ambayo unapaswa kukamilisha ndani ya mwezi mmoja, siku za mwanzo za kazi hiyo unakuwa huna msongo kabisa, muda upo wa kutosha na hivyo husukumwi sana kuchukua hatua. Zikibaki siku kumi kufika tarehe ya mwisho na hujaanza kufanya, unapaswa na msongo, ambao unakusukuma kuchukua hatua, ghafla unajikuta unapata nguvu ya kuchukua hatua. Lakini kama utajichelewesha na kukuta upo siku ya mwisho na hujachukua hatua, akili inakuwa kama inakwama, unajikuta huwezi kufanya chochote.

Hivyo unahitaji kiasi fulani cha msongo ili uweze kuchukua hatua. Na zipo njia mbili za kutengeneza msongo huu, ambapo unategemea homoni mbili zinazochangamsha ubongo wako.

Njia ya kwanza ni kutengeneza hofu au uharaka, hapa unajiweka kwenye hali ambayo inakutaka kuchukua hatua haraka kabla muda haujaisha au kukosa kitu fulani. Hali hii inazalisha homoni ya norepinephrine kwenye ubongo wao, ambayo inaupa mwili nguvu ya kuchukua hatua. Mfano wa njia hii ni kujiwekea ukomo wa kukamilisha kitu.

Njia ya pili ni kujiwekea zawadi ambayo utapata kwa kuchukua hatua, huenda kwa kuwa na lengo kubwa ambalo linakusukuma zaidi, au kuwa na kitu unachotarajia kupata kwa kuchukua hatua fulani. Hali hii inazalisha homoni ya dopamine kwenye ubongo ambayo inaupa mwili nguvu ya kuchukua hatua zaidi.

Kama unataka kujisukuma kuchukua hatua, na kuwa na ufanisi wa hali ya juu, tengeneza hali hizi mbili na utapata nguvu kubwa ya kuchukua hatua na kuondokana na usumbufu usio na umuhimu.

JINSI YA KUVUKA MKWAMO WA KIAKILI.

Kuna wakati akili zetu zinakuwa kwenye mkwamo, ambapo unashindwa kabisa kufanya maamuzi unayotaka kufanya. Fikiria wakati ambapo ulikuwa unataka kukumbuka kitu lakini kumbukumbu haziji, na kadiri ulivyokuwa unajilazimisha kukumbuka, ndivyo inavyozidi kuwa vigumu kukumbuka. Labda ni jina la mtu unataka kukumbuka, lakini haliji kabisa, unajilazimisha kweli kulikumbuka lakini haliji. Lakini baadaye, ukiwa unafanya shughuli zako nyingine, kumbukumbu za jina lile zinakuja bila hata ya kutumia nguvu kubwa.

Kwa mfano huo hapo juu, ambao umewahi kukutokea, inaonesha jinsi ambavyo ubongo huwa unapatwa na mkwamo, hasa unapokuwa na msongo sana au kuwa na taarifa nyingi kuhusu kitu na hivyo kushindwa kuchambua kwa umakini.

Njia ya kuondokana na mkwamo huu wa kiakili ni kuliacha lile tatizo linalokupa mkwamo na kufanya mambo mengine. Fanya mambo ambayo hayana uhusiano kabisa na pale ulipokwama, na utashangaa, bila ya kujua, jibu linakuja lenyewe kwenye akili yako. Unapopeleka mawazo yako kwenye jambo jingine unatoa uhuru mkubwa kwa ubongo wa juu kutulia na akili ya ndani kufanyia kazi tatizo ulilokwama na majibu kujitokeza yenyewe ukiwa hata hutegemei.

Hii ndiyo maana mara nyingi unajikuta unapata mawazo mazuri sana ukiwa haujilazimishi kupata mawazo mazuri. Mfano wakati unaoga, wakati unatembea na hata ukiwa umepumzika. Wapo watu ambao huenda na vijitabu vya kuandika mawazo mazuri wanayopata wakati wa kuoga.

Unapojikuta umekwama kwenye jambo lolote, ambapo akili inaonekana kutokuja na jibu, ipumzishe akili kwa kuipa jukumu jingine rahisi, mfano kutembea au kujihusisha na kitu kingine ambacho hakiilazimu akili yako kufikiri, majibu yatakuja kwako yenyewe.

MTAMBUE MWONGOZAJI MKUU WA MAISHA YAKO.

Ili kuweza kuwa na ufanisi wa hali ya juu na kuyaishi vizuri maisha yako, unahitaji muunganiko wa vitu viwili, moja kujua ubongo wako na pili kuweza kuangalia jinsi ubongo wako unavyofanya kazi. Mpaka sasa tumeshajua vizuri kuhusu ubongo wetu na jinsi unavyofanya kazi. Kitu kingine muhimu sana tunachopaswa kujua ni kuweza kuuangalia ubongo huo unavyofanya kazi na kuweza kufanya maamuzi juu ya ufanyaji wake wa kazi.

Kwa maneno mengine, ni lazima uweze kuufuatilia ubongo wako, na kuona ufanisi wake, kisha kujirekebisha kutokana na kile unachoona. Yaani ni sawa na wewe kujiangalia mwenyewe kama vile mtu mwingine anakuangalia. Au tunaweza kusema ni kufikiri kuhusu kufikiri, yaani unajipa muda wa kufikiria kuhusu kile unachofikiria.

Njia bora ya kuweza kujiangalia mwenyewe na kupiga ufanisi wa ubongo wako ni kuwa kwenye uwepo (mindfullness). Hapa unajihoji kwa kila unachofikiria na kila unachofanya, na hivyo inakuwa rahisi kujikamata pale fikra zako au hatua zako zinakuwa siyo sahihi.

Kwa kujua mwongozaji mkuu wa maisha yako, ambayo tunaiita nafasi yako, utaweza kudhibiti ubongo wako na kupata matokeo bora kabisa. Unapaswa kuwa tayari kujiangalia wewe mwenyewe kama mtu mwingine anavyoweza kukuona, na kuweka hisia pembeni. Hapo utaona makosa unayofanya na kuweza kujirekebisha.

JINSI YA KUPATA UTULIVU UNAPOKUWA KWENYE MSONGO.

Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia, huwa tunaendeshwa kwa hisia kuliko kufikiri, kitu ambacho hatupendi kukikubali, lakini ndiyo uhalisia. Tunasukumwa na hisia kuu mbili, tamaa ya kupata tunachotaka au hitaji la kuondokana na maumivu tuliyonayo au tunayoweza kupata.

Kuna wakati unajikuta kwenye hali ya msongo mkubwa, hasa pale hisia zinapokuwa juu na kukuzuia kufikiri kwa usahihi. Katika nyakati kama hizo ndipo wengi hufanya makosa yanayowagharimu sana.

Kazi zetu nyingi huwa zinatuweka kwenye hali hizi za msongo, ambapo hisia zinakuwa juu, mfano katika kufikia makubaliano mbalimbali au kufanya maamuzi muhimu.

Unapojikuta kwenye hali kama hiyo, kuna hatua tatu unaweza kuchukua,

Moja ni kuonesha hisia zako, kitu ambacho kwa mazingira ya kawaida siyo rahisi, mfano unapokuwa na hasira unaweza kutamani kulia, lakini kulia mbele ya watu haileti picha nzuri, hasa kama ni kwenye majadiliano muhimu.

Mbili ni kuzuia hisia hizi zisitoke nje, lakini hii nayo haifanyi kazi vizuri, maana hisia ni kama moto, unaweza kuuficha lakini moshi utakuumbua. Ni rahisi kwa wengine kujua pale unapokuwa unazuia hisia ndani yako.

Tatu ni kubadili namna unavyochukulia hisia hizo kifikra, na hapa kuna mambo mawili unaweza kufanya. Unaweza kuzipa jina hisia hizo, na hii itakusaidia kuzielewa, mfano unapokuwa una hasira, jiambie hapa nina hasira, hii inakusaidia kufanya hasira hizi zisiendelee. Jambo la pili unaloweza kufanya ni kubadili maana ya kile kilichotokea, kwa kuangalia kwa ndani na kukielewa vizuri zaidi. Mara nyingi tumekuwa tunachukua hatua haraka kabla ya kuelewa kitu, lakini unapokielewa kwa ndani unagundua ulichokuwa unafikiri siyo.

Hiyo ndiyo njia bora ya kukabiliana na msongo, kuzipa jina hisia zako na kupata maana tofauti ya kilichosababisha hisia hizo.

JINSI YA KUTUMIA MATEGEMEO KUDHIBITI HISIA ZAKO.

Mategemeo tunayokuwa nayo kwenye maisha huwa yana mchango sana kwenye hisia tunazopata. Mategemeo haya huwa chanya na kutupa furaha na matumaini au huwa hasi na kutupa hofu na kukata tamaa.

Kemikali kuu inayohusika na furaha kwenye ubongo ni dopamine, na inaonekana kwamba unapokuwa na mategemeo chanya, dopamine huzalishwa kwa wingi pale unapoyafikia. Lakini unapokuwa na mategemeo makubwa, na usiyafikie, ubongo huenda kwenye hali hasi na kuzalisha homoni ya msongo badala ya dopamine.

Hivyo kama tunataka kuwa na furaha wakati wote, tunapaswa kuwa na mategemeo chanya, ambayo tuna uhakika wa kuyafikia. Tunapoyafikia ubongo unatuzawadia dopamine ambayo inatufanya tujisikie vizuri. Usiweke mategemeo makubwa sana ambayo huwezi kuyafikia, au kuweka mategemeo yako kwa wengine, kwa sababu mambo yatakapokwenda tofauti itakuvuruga sana.

Rafiki, ni imani yangu umepata mwanga mkubwa wa jinsi ubongo wako unavyofanya kazi, na jinsi ya kuutumia vyema katika kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako. Kwa zama tunazoishi sasa, bila ya kushika hatamu na umiliki wa ubongo wako, wengine watakutumia kwa manufaa yako. Watakuletea kelele za kila aina, wataibua hisia zako na kuishia kunufaika kwa makosa unayofanya. Shika hatamu ya ubongo wako, jidhibiti wewe mwenyewe na utakuwa na maisha tulivu, bora na yenye mafanikio makubwa.

#3 MAKALA YA JUMA; NJIA NNE ZA KUTULIZA AKILI YAKO.

Kama ambavyo tumeshajifunza, huwa tunatengeneza msongo wa mawazo na hali ya kukosa utulivu kwa kutokuuelewa ubongo wetu wenyewe. Tukielewa jinsi ambavyo ubongo wetu unavyofanya kazi, tutaweza kutuliza akili zetu na kuondokana na msongo wa mawazo.

Kwenye makala ya juma hili nimekushirikisha njia nne za kutuliza akili yako na kuweza kupata utulivu, hasa pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea. Njia hizi nne zinatupa namna tofauti ya kuliangalia tatizo na kupata maana tofauti ambayo haiwi tishio kwetu.

Kwa kuwa huna udhibiti wa mambo yanayotokea kwenye maisha yako, ni muhimu sana kuzijua njia hizi nne na kuzifanyia kazi kila siku ili uwe na maisha yenye utulivu na yasiyokuwa na msongo wa mawazo.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo ya juma, isome sasa hapa; Hizi Ndiyo Njia Nne Za Kutuliza Akili Yako Na Kupata Utulivu Pale Mambo Yanapokwenda Tofauti Na Ulivyotarajia. (https://amkamtanzania.com/2019/04/26/hizi-ndiyo-njia-nne-za-kutuliza-akili-yako-na-kupata-utulivu-pale-mambo-yanapokwenda-tofauti-na-ulivyotarajia/)

Pia endelea kutembelea mtandao wako wa AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA, kila siku kuna makala mpya zinazowekwa za kukuwezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

#4 TUONGEE FEDHA; FEDHA NI ZAWADI MBAYA.

Ubongo wetu huwa unafanya kitu kutokana na misukumo miwili, msukumo wa kwanza ni wa TAMAA, ambapo hapa unafanya ili kupata kile ambacho unataka. Msukumo wa pili ni wa MAUMIVU, ambapo unasukumwa kufanya kitu ili kuepuka maumivu ambayo utayapata kama hutakifanya.

Kwa kujua misukumo hii miwili ya kufanya kitu, wanasaikolojia walikuwa na njia mbili za kuwahamasisha watu kufanya kitu au kubadili tabia. Njia hizo ni ZAWADI na ADHABU. Zawadi inachochea msukumo wa tamaa, wa kupata kitu kizuri na adhabu inachochea msukumo wa maumivu, kukwepa kile ambacho siyo kizuri.

Hivyo watu wamekuwa wanatumia njia hizi mbili pale wanapotaka kuwahamasisha wengine kuchukua hatua fulani au kubadili tabia zao. Wengi wamekuwa wanaahidi zawadi, kwamba mtu akifanya kile ambacho anatakiwa kufanya basi anapata zawadi, na kweli wengi hujituma ili wapate zawadi waliyoahidiwa. Pia watu wamekuwa wanapewa adhabu pale ambapo wanafanya kile ambacho hawapaswi kufanya au wanaacha kufanya wanachopaswa kufanya. Na kwa kuwa adhabu inaumiza, basi wengi hukwepa kupata adhabu hiyo kwa kufanya wanachopaswa kufanya.

Zawadi ambayo imezoeleka na wengi, hasa kwenye maeneo ya kazi na hata wakati mwingine kwenye familia ni fedha. Mtu anaahidiwa kama atatekeleza kile alichopangiwa kufanya basi atapewa zawadi ya fedha, au kitu kingine kinachoweza kuthaminishwa kwa fedha.

Njia hii hufanya kazi mwanzoni, ila ikiendelea kutumika haileti tena matokeo mazuri, labda kama zawadi itakuwa inaendelea kuongozwa kadiri muda unavyokwenda. Hii inafanya zawadi ya fedha kuwa zawadi mbaya katika kuwahamasisha watu kuchukua hatua.

Iko hivi, unapopewa zawadi, ubongo wako unachilia kemikali inayoitwa dopamine, ambayo ndiyo inakuletea raha, lakini kemikali hii inavunjwa baada ya muda mfupi na ile  raha inaondoka baada ya muda mfupi. Sasa kama baadaye utapewa tena zawadi ile ile, yaani kiwango kile kile cha fedha, ubongo unaachilia kiwango kile kile cha dopamine ambacho kwa sasa hakitaweza kusisimua tena ubongo wako kama awali. Ili upate msisimko wa kukupa raha kama mwanzo, lazima kiwango cha zawadi kiwe kikubwa kuliko mwanzo. Hii haina tofauti na uraibu kwenye ulevi na madawa ya kulevya, kwamba ukitumia kiwango kile kile ulichozoea hupati raha kama ya mwanzo, hivyo inabidi uongeze kiwango zaidi.

Zawadi ya fedha na vitu vyenye thamani ya fedha itafanya kazi kama utaendelea kuongeza kiwango kila wakati. Sasa kama huwezi kuongeza kiwango, kuendelea kutoa kiasi kile kile hakutaleta matokeo mazuri.

Swali ni je ni zawadi gani sahihi kumpa mtu ambayo itamsukuma kuchukua hatua zaidi?

Na hapa tunarudi kwenye tabia za ubongo, ambapo mwandishi David Rock ametushirikisha ubongo wetu unahitaji vitu vitano muhimu sana, ambavyo vinausukuma kuchukua hatua au kutokuchukua hatua.

Kitu cha kwanza ni HADHI, ubongo wetu unajali sana hadhi yetu kwa kujilinganisha na wengine. Unapopewa hadhi ya juu, unajisukuma kufanya zaidi.

Kitu cha pili ni UHAKIKA, kama kukiwa na uhakika basi ubongo unakuwa tayari kuchukua hatua.

Kitu cha tatu ni UDHIBITI, mtu anapoona ana udhibiti wa maisha yake, anasukumwa kuchukua hatua zaidi.

Kitu cha nne ni UHUSIANO, kama wengine wanafanya kitu fulani, mtu anahamasika kufanya pia, hakuna anayependa kuachwa nyuma.

Kitu cha tano ni HAKI, ubongo unapenda sana haki, inapoonekana ni haki kufanya kitu fulani, basi mtu anasukumwa zaidi kufanya.

Hivyo kama unataka mtu ahamasike kufanya kitu fulani, kwanza mwoneshe kwamba kufanya kitu hicho kunaongeza hadhi yake, mpe uhakika wa namna ya kufanya kitu hicho na matokeo yake, mpe nafasi ya kuchagua mwenyewe anafanyaje, mwoneshe kwamba wengine pia wanafanya hivyo na mfanye aone ni haki kwake kufanya hivyo.

Ukiweza kutumia njia hizo tano, utaweza kuwahamasisha wengine kuchukua hatua unazotaka wachukue au kubadili tabia, na watajiona wanafanya kwa maamuzi yao na siyo kulazimishwa na yeyote.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; SIMU YAKO INAKUFANYA KUWA MJINGA.

“A study done at the University of London found that constant emailing and text-messaging reduces mental capability by an average of ten points on an IQ test. It was five points for women, and fifteen points for men. This effect is similar to missing a night’s sleep. For men, it’s around three times more than the effect of smoking cannabis.” ― David Rock

Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha London unaonesha kwamba matumizi ya mara kwa mara ya simu, hasa kwenye kutuma na kupokea email na jumbe za simu, kunapunguza uwezo wa akili kwa alama kumi kwenye kipimo cha IQ. Madhara haya ni makubwa zaidi kwa wanaume kuliko wanawake.

Kwa matokeo ya utafiti huu, na maisha ambayo watu wanaishi sasa, ni dhahiri kwamba simu zinawafanya watu kuwa wajinga zaidi na zaidi kila siku. Kwa sababu sasa hivi ni kama simu zimewekewa gundi kwenye mikono ya watu. Watu hawawezi kukaa kwa nusu saa kabla hawajaangalia simu zao. Mitandao ya kijamii imefanya hali kuwa mbaya zaidi.

Watu hawawezi tena kuweka umakini wao kwenye kazi wanayoifanya kwa muda mrefu na kuepuka usumbufu. Wanakaa karibu na simu zao, wanafanya kazi kidogo, simu zinaita au ujumbe unaingia, wanaacha kazi waliyokuwa wanafanya na kuangalia ujumbe, ambao hata siyo muhimu. Wanajibu ujumbe huo, na kurudi kwenye kazi. Wanaporudi kwenye kazi, hawawezi tena kuendelea pale walipoachia, inabidi waanze tena kujijengea mazingira ya kuweka akili hiyo kwenye kazi, kabla akili haijatulia, ujumbe mwingine tena unaingia, anaacha kazi na kuangalia. Mambo yanaenda hivyo mpaka siku inaisha, mtu anakuwa amechoka lakini akiangalia hakuna kazi kubwa aliyokamilisha.

Rafiki, kama unataka kurudisha akili zako, kama unataka kuwa na ufanisi mkubwa, jitengee muda ambao utafanya kazi bila ya usumbufu kabisa. Tenga vipande vya muda, vya masaa mawili mawili ambapo utafanya kazi tu. Katika muda huo simu unaizima au kuiweka kwenye ukimya na huiangalii mpaka muda huo uliotenga wa kazi uishe. Ukiwa na vipande viwili mpaka vitatu kwenye siku yako, utakamilisha ndani ya siku moja kile ambacho kinawachukua wengine wiki nzima kukamilisha.

Usikubali simu yako ikufanye wewe kuwa mjinga, kuwa mjanja, imiliki simu yako na siyo simu ikumiliki wewe.

Rafiki, hizi ndizo tano za juma, tano ambazo zimekupa mwanga mkubwa kuhusu ubongo wako na jinsi ya kuutumia vizuri kwa manufaa kwako. Umeshayapata maarifa haya, njia pekee ya kunufaika nayo ni kuyaweka kwenye vitendo. Nakutakia kila la kheri katika kutumia vizuri ubongo wako na kushika hatamu ya maisha yako.

Kwenye #MAKINIKIA nakwenda kukupa mambo ya kushangaza usiyojua kuhusu ubongo wako na hatua za kuchukua ili uweze kuwa na maisha bora sana. Utajifunza vitu vipya vya kujaribu ili kuweza kutumia vizuri ubongo wako, kupata utulivu, kuondokana na msongo na kuweza kufanya kazi bora pamoja na kuimarisha mahusiano yako na wengine.

#MAKINIKIA yanapatikana kwenye channel ya telegram ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA. Kama bado hujajiunga na channel hii, unakosa mengi mazuri, chukua hatua sasa kwa kufuata maelekezo yaliyopo hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu