Rafiki yangu mpendwa,

Msongo wa mawazo au kama unavyoitwa kwa Kiingereza ‘stress’ ni tatizo kubwa sana kwa zama tunazoishi sasa.

Limekuwa ni tatizo ambalo linawaua watu wengi taratibu na kabla ya muda kuliko matatizo mengine yoyote. Hii ni kwa sababu mwili unapokuwa kwenye msongo unakuwa dhaifu na hivyo kushindwa kupambana na mashambulizi mbalimbali yanayoukabili mwili.

Tunaishi kwenye zama ambazo watu wengi wamevurugwa sana, zama ambazo watu wanataka kitu na wanakitaka sasa, hakuna mwenye subira. Ni zama hizi pekee ambapo mtu anaweza kusema ndiyo kwenye kila kinachokuja mbele yake, licha ya kwamba hana muda wa kuweza kutekeleza vitu vyote anavyosema ndiyo.

Unapotaka kila kitu kiende kama unavyotaka, na kutaka kupata kitu pale unapokitaka bila ya subira, halafu ukasema ndiyo kwa kila kitu kizuri unachokiona, lazima uzalishe msongo mkubwa kwenye akili yako, kwa sababu unalazimisha vitu ambavyo haviwezekani viwezekane.

Pedram Shojai ambaye ni mwandishi wa kitabu The Urban Monk anatufundisha njia sahihi za kuondokana na msongo wa mawazo na kuwa na utulivu mkubwa kwenye maisha yetu

urban monk

Katika kitabu chake, Pedram anatushirikisha hekima za watawa wa mashariki hasa kutoka falsafa ya Tao, ambao wamekuwa wakiishi kwa misingi ya asili, kusikiliza mwili na kuisikiliza dunia ili kufanya kile kilicho sahihi

Njia anazotushirikisha Pedram kwenye kitabu chake siyo njia mpya, bali zimekuwepo kwa miaka mingi na zimekuwa zinatumiwa na watawa kupata utulivu mkubwa na kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Katika kitabu chake hiki, kwenye sura inayohusu msongo, Pedram anatushirikisha mambo matatu muhimu kuhusu msongo.

Kwanza ni jinsi mwili unavyozalisha msongo.

Pili ni madhara ya msongo kwenye mwili.

Tatu ni njia za kuondokana na msongo na kuwa na maisha tulivu.

Karibu tujifunze maarifa haya muhimu kuhusu msongo ili tuweze kuwa na maisha tulivu.

JINSI MWILI UNAVYOZALISHA MSONGO.

Kwa asili sisi binadamu tulikuwa tunaishi kwenye mazingira magumu na hatari. Enzi hizo kabla ya mazingira kuwa salama kama sasa, watangulizi wetu waliishi maporini ambapo wanyama wakali walikuwa karibu na waliwatumia binadamu kama vitoweo. Pia mazingira yalikuwa magumu, baridi kali, upatikanaji wa chakula mgumu na hata ushindani mkali ndani ya jamii yenye rasilimali chache.

Katika kuhakikisha mtu anazivuka hatari zote hizo na kuendeleza kizazi cha mwanadamu, ubongo wetu ulijijenga kwa njia ya kuutaarifu mwili na kuuandaa kupambana na mazingira yaliyo hatarishi. Na hapa ndipo msongo unapozaliwa.

Pale ambapo mtu yupo kwenye mazingira hatari, ubongo wake unazalisha homoni za msongo, ambazo zinauandaa mwili kupambana au kukimbia (fight or flight). Uwepo wa homoni hizo kwenye mwili, unaweka kipaumbele kwenye misuli mikubwa ya mwili ambayo inaweza kupambana au kukimbia kutoka kwenye changamoto hiyo. Hivyo maeneo yale tu ambayo yanaweza kuusaidia mwili kwa haraka ndiyo yanayopata mzunguko mzuri wa damu yenye virutubisho vya chakula na hewa safi ya oksijeni.

Sasa hali hii ilikuwa nzuri na yenye faida enzi hizo ambapo binadamu tuliishi kwenye hatari kubwa sana. Mfano umeenda msituni kuwinda, kisha ukakutana na simba, hilo ni jambo la kufa na kupona. Mwili wako unapata msongo mkubwa ambao unazalisha homoni nyingi za msongo na kukupa nguvu kubwa ya kukimbia ili kuokoa maisha yako.

Lakini zama tunazoishi sasa hatari kubwa zimepungua. Kwa walio wengi, kukutana na simba ni mpaka ukawatembelee kwenye hifadhi zao, na hapo wamelindwa. Kwa wengi maisha yetu hayana hatari ya kufa na kupona kila siku, lakini bado miili yetu inazalisha msongo.

Miili yetu inaendelea kuzalisha msongo mkubwa kwa mambo madogo ambayo tunayachukulia kwa uzito mkubwa. Kwa mfano umefika eneo lako la kazi na kumsalimia bosi wako lakini hakuitika, hapo mwili unapata msongo mkubwa sana, ukijiuliza ni kitu gani kinaendelea. Au unaendesha au kutembea barabarani na ghafla mtu mwingine akakatisha kwa kasi kubwa mbele yako kiasi cha kutaka kukugonga, hapo mwili wako utapata msongo mkubwa sana.

Simu janja na mitandao ya kijamii ambayo tunatumia kila siku imekuwa sehemu nyingine inayozalisha msongo kwa wengi. Pale mtu anapoangalia maisha ya wengine na kuyaona ni bora kuliko yake, au anapoweka vitu vyake na watu wasioneshe kuvipenda sana, mtu anapata msongo ambao unamsumbua sana.

Mambo haya yanayozalisha msongo tunayopitia kila siku siyo mambo makubwa na yenye hatari, lakini tumekuwa tunashindwa kutofautisha ukubwa wa mambo yanayoleta msongo na hili limeleta madhara makubwa kwetu kama ambavyo tutaona hapo chini.

Tunaweza kusema tunaishi kipindi ambacho ni salama sana, lakini miili yetu bado ina kumbukumbu za hatari kubwa na hilo limefanya msongo kuwa tatizo kubwa kwa wengi.

SOMA; Hizi Ndiyo Njia Nne Za Kutuliza Akili Yako Na Kupata Utulivu Pale Mambo Yanapokwenda Tofauti Na Ulivyotarajia.

MADHARA YA MSONGO KWENYE MWILI.

Kama tulivyojifunza hapo juu, msongo unazalishwa pale mwili unapouwa kwenye hali ya hatari, lakini akili zetu haziwezi kutofautisha hatari kubwa na hatari ndogo. Tunapohofia kitu chochote, ubongo wetu unazalisha homoni za msongo na mwili kuingia kwenye msongo ili kupambana au kukimbia.

Mwili unapokuwa kwenye hali ya msongo, nguvu zote zinapelekwa kwenye misuli mikubwa ya mwili inayoweza kusaidia kupambana au kukimbia, hivyo maeneo mengine muhimu yanasahaulika na hilo linaleta madhara makubwa kwenye mwili.

Mfano mzuri wa mwili uliopo kwenye msongo ni kama nchi ambayo ipo kwenye vita. Nchi ikiwa kwenye vita, rasilimali zote zinakwenda kwenye vita, hivyo maeneo mengine muhimu kama elimu, afya, miundombinu havipewi kipaumbele kwa sababu kushinda vita ni muhimu zaidi wakati huo. Ubaya ni kwamba, kwa maisha tunayoishi sasa, mwili upo kwenye vita kila siku. Sasa angalia nchi ambazo zipo kwenye vita kila siku, na utaelewa kwa nini afya za wengi zipo kwenye matatizo makubwa, ni kwa sababu ya msongo usioisha.

Yafuatayo ni madhara makubwa ya msongo kwenye mwili wako.

 1. Kinga ya mwili kudhoofu.

Kwa kuwa nguvu nyingi zinapelekwa kwenye misuli mikubwa wakati wa msongo, maeneo ya kuzalisha na kuimarisha kinga ya mwili hayapo kwenye kipaumbele. Hili linapelekea kinga ya mwili kudhoofu sana. Ndiyo sababu ni rahisi kupata magonjwa wakati mtu yupo kwenye msongo.

Tafiti za kitabibu zinaonesha asilimia 90 ya magonjwa yanatokana na msongo wa muda mrefu unaoshusha sana kinga ya mwili. Magonjwa kama saratani, shinikizo la damu na hata kisukari, yameongezeka sana zama hizi kutokana na wengi kuwa na msongo wa muda mrefu unaoharibu kabisa kinga ya mwili.

 1. Matatizo kwenye umeng’enywaji wa chakula.

Umeng’enywaji wa chakula unahitaji nguvu kubwa sana na mwili ambao ni tulivu. Ndiyo sababu wengi husinzia baada ya kula chakula, kwa sababu mwili huelekeza nguvu nyingi kwenye kumeng’enya chakula hicho.

Sasa mwili unapokuwa kwenye msongo, nguvu nyingi zinaelekezwa kwenye kuuandaa mwili kupambana au kukimbia, hivyo hakuna nguvu za kuendesha mfumo wa umeng’enyaji wa chakula.

Hili limekuwa chanzo cha magonjwa mengi ya kwenye mfumo wa chakula kama ukosefu wa virutubisho mwilini, kukosa choo au kuharisha, kuvimbiwa na kuwa na uchovu mkubwa wa mwili.

 1. Kupanda na kushuka kwa sukari kwenye damu.

Mwili unapokuwa kwenye msongo, homoni za msongo zinazozalisha zinahakikisha mwili una sukari ya kutosha ili kupambana au kukimbia. Hivyo mafuta na sukari iliyohifadhiwa kwenye mwili inageuzwa kuwa sukari na kuingia kwenye damu. Hili linafanya sukari kwenye damu kuwa juu sana.

Sukari kwenye damu inapokuwa juu sana, homoni ya insulini huzalishwa kwa wingi pia ili kupunguza sukari hiyo kwenye damu. Sasa kwa kuwa sukari iliingia kwa wingi, insulini nayo inazalishwa kwa wingi na hivyo sukari kupungua kwa ghafla na kuwa chini ya kiwango cha kawaida kinachopaswa kuwa kwenye damu.

Hali hii ya kupanda na kushuka kwa sukari, inapelekea mwili kuwa kwenye hali ya uchovu na mtu kutamani kula muda wote. Unafikiri kwa nini unapokuwa na msongo unatamani kula chochote kilichopo mbele yako? Ni kwa sababu mwili unateseka kwa kupanda na kushuka kwa sukari.

 1. Kudhoofu kwa mfumo wa homoni.

Mwili unapokuwa kwenye msongo kwa muda mrefu, mfumo wa homoni wa mwili huwa unakosa nguvu zinazohitajika ili kuzalisha homoni muhimu za kuendesha mwili. Na moja ya eneo ambalo linaathirika sana ni homoni za kike na za kiumbe, yaani estrogen na testosterone.

Mwanaume anapokuwa kwenye msongo kwa muda mrefu homoni zake za kiume (testosterone) zinashuka sana na hili linaleta matatizo kama kushindwa kusimamisha uume, kukosa hamu ya kushiriki mapenzi, kukosa nguvu na hamasa ya kufanya kazi na kushindwa kuzalisha mbegu za kiume kwa kiwango sahihi. Bila ya kiwango cha kutosha cha homoni hii ya kiume, maisha ya mwanaume yanakuwa magumu sana.

Mwanamke anapokuwa kwenye msongo kwa muda mrefu, homoni zake za kike (estrogen) sinasyika sana na hili linaleta matatizo kama kuvurugika kwa mfumo wa hedhi, kushindwa kubeba ujauzito, ujauzito kutoka, kukosa hamu ya kushiriki mapenzi, kuota ndevu na nywele maeneo ambayo siyo kawaida kwa wanawake kuwa na nywele hizo. Bila ya kiwango cha kutosha cha homoni ya kike, mwili wa mwanamke unakuwa kwenye hali ngumu na mbaya.

 1. Kushindwa kutumia ubongo wetu vizuri.

Ubongo wa binadamu ni kitu chenye nguvu kubwa sana, ni ubongo ulioendelea kuliko wa wanyama wengine wote na tunajitofautisha na wanyama hao kwa uwezo wetu wa kufikiri na kufanya maamuzi. Ubongo wetu umegawanyika kwenye sehemu tatu, ubongo wa chini ambao unahusika na mifumo inayotuweka hai, kama upumuaji na mapigo ya moyo, ubongo wa kati ambao unahusika na hisia na ubongo wa juu ambao unahusika na kufikiri na kufanya maamuzi. Ubongo wa juu ni mkubwa na unachukua sehemu kubwa ya nguvu inayotengenezwa mwilini.

Wakati mwili upo kwenye msongo, kipaumbele cha nguvu kinapelekwa kwenye yale maeneo ambayo yana msaada wa kukimbia au kupambana, na ubongo wa juu siyo moja ya maeneo hayo. Hivyo wakati wa msongo, ubongo wa juu unakosa nguvu na hivyo mtu hawezi kufikiri wala kufanya maamuzi sahihi.

Hii ndiyo sababu wakati wa msongo mtu hujikuta amefanya kitu lakini hajui amekifanyaje. Hii ni kwa sababu mwili unafanya kwa mazoea na hakuna nafasi ya kufikiri na kufanya maamuzi sahihi.

Sasa fikiria mwili ambao upo kwenye msongo kila siku, mtu anaweza kuwa anayaendesha maisha yake kila siku kwa mazoea bila ya kufikiri kabisa. Hapo anashindwa kutumia nguvu kubwa iliyopo kwenye ubongo wake.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu Your Brain At Work (Mbinu Za Kushinda Usumbufu, Kuongeza Umakini Na Kuweza Kufanya Kazi Kwa Ubora Siku Nzima)

NJIA ZA KUONDOKANA NA MSONGO NA KUWA NA MAISHA TULIVU.

Tumeona jinsi ambavyo msongo unazalishwa mwilini, tumeona jinsi ambavyo msongo una madhara kwenye miili yetu, na kama umekuwa unajitafakari wakati unasoma haya, umejionea mwenyewe jinsi msongo umeleta madhara kwako.

Sasa tunakwenda kujifunza njia sahihi za kuondokana na msongo na kuwa na maisha tulivu.

Kama tulivyojifunza, vitu vinavyozalisha msongo kwenye miili yetu kwa zama tunazoishi sasa havina hatari kubwa kama ilivyokuwa kwa watangulizi wetu. Naweza kusema tunatumia silaha kubwa kupambana na adui ambaye hata bila kupambana naye angeshindwa yeye mwenyewe.

Kwa kuelewa jinsi akili na mwili wetu unafanya kazi, tunaweza kuondokana kabisa na msongo kwenye maisha yetu, tukawa na maisha yaliyo tulivu, yenye furaha na mafanikio makubwa. Haimaanishi kwamba maisha yako yataacha kuwa na changamoto, changamoto zitaendelea kuwepo, lakini hazitazalisha msongo kwenye mwili wako.

Zifuatazo ni njia za kuondokana na msongo ili kuweza kuwa na maisha tulivu.

 1. Acha tamaa.

Chanzo kikuu cha msongo ni tamaa. Pale tunapotamani kuwa na vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wetu kwa wakati huo, tunazalisha msongo kwenye miili yetu.

Maisha ya sasa yamejengwa kwenye mashindano ya kijinga. Mashindano ya kutaka kitu kwa sababu kila mtu anacho. Mashindano haya yamepelekea wengi kuingia kwenye madeni ili kupata wanachotaka. Wanaweza kupata wanachotaka, lakini madeni wanayobaki nayo yanakuwa chanzo cha msongo mkubwa kwao.

Acha tamaa, acha kushindana na wengine na ishi maisha yako kwa ukamilifu, fanya kile unachoweza kufanya kwa pale ulipo sasa, na kama kuna kitu kipo nje ya uwezo wako usijilazimishe nacho.

 1. Dhibiti taarifa zinazoingia kwenye akili yako.

Taarifa tunazoruhusu ziingie kwenye akili zetu zina madhara makubwa kwenye miili yetu. Pale ambapo taarifa zinazoingia ni hasi na za kukatisha tamaa, tunaingiwa na hofu na hapo mwili unaingia kwenye msongo.

Tumezungukwa na taarifa nyingi hasi na za kutisha na hata wale waliotuzunguka wana kila njia ya kutukatisha tamaa. Unapaswa kuwa makini ni aina gani ya taarifa unaruhusu ziingie kwenye akili yako na aina gani ya watu unaowasikiliza ili kuepusha kuingia kwenye msongo usio na umuhimu.

Epuka sana kufuatilia habari na pia waepuke sana watu ambao ni wakatishaji wa tamaa na wanaoona magumu mara zote.

 1. Ishi wakati uliopo.

Sababu nyingine kubwa ya msongo ni pale ambapo mtu anashinda kuishi wakati uliopo. Kuna nyakati tatu kwenye maisha yako, wakati uliopita, wakati uliopo na wakati ujao.

Unapojikuta kwenye msongo, kwa hakika utakuwa unaishi wakati uliopita ambapo mambo yameshapita na huwezi kuyabadili au utakuwa unaishi wakati ujao, ambao bado hujaufikia na hivyo huwezi kubadili chochote.

Huwezi kuwa na msongo kama unaishi wakati uliopo, kama mawazo yako yote yapo kwenye kile kitu unachofanya sasa, msongo hauwezi kupata nafasi kabisa. Jifunze kuweka akili yako yote kwenye kitu unachofanya kwa wakati huo, linapokuja wazo la kitu cha nyuma au kijacho liandike pembeni na jilazimishe kurudisha akili kwenye kile unachofanya. Kwa njia hii utaondokana kabisa na msongo.

 1. Ondokana na vilevi.

Wengi wamekuwa wanatumia vilevi kama njia ya kuondokana na msongo, lakini wote tunajua vilevi vinasogeza msongo mbele, unajisahaulisha kwa muda lakini ulevi unapoisha msongo unarudi pale pale.

Vilevi vinazidi kuuchosha mwili na kutengeneza msongo mpya. Hivyo epuka kutumia njia ya vilevi kama sehemu ya kukabiliana na msongo.

Epuka matumizi ya kahawa au sigara, vitu viwili ambavyo watu hutumia sana wanapokuwa na msongo. Kemikali zilizopo kwenye vitu hivi vinauweka mwili kwenye hali ya msongo zaidi.

 1. Fanya mazoezi.

Mazoezi ni njia bora ya asili ya kukabiliana na msongo. Mwili unapokuwa kwenye mazoezi, unazalisha homoni tofauti na za msongo, homoni ambazo zinafanya mtu ajisikie vizuri.

Mazoezi pia ni njia ya kuurudisha mwili kwenye asili yake, kwa sababu sisi binadamu hatukuumbwa kukaa kwa muda mrefu, shughuli za watangulizi wetu zilikuwa za kuhusisha viungo vyote vya mwili. Lakini hali ya sasa tunajikuta tunakaa kwa muda mrefu, kitu ambacho kinachochea msongo zaidi. Unapofanya mazoezi unauondoa mwili kwenye hali ya msongo.

 1. Ongeza ukomavu wako kwenye msongo.

Sababu nyingine kubwa ya msongo kuwa tatizo kwa wengi zama hizi ni kwamba miili yetu haijazoea kabisa mazingira magumu. Tumeishi kwenye kipindi ambacho ni rahisi kupata kila tunachotaka, na hivyo mwili unabweteka na kuwa laini, usioweza kupambana hata na vitu vidogo.

Ondokana na hali hii kwa kuukomaza mwili wako. Unaweza kufanya hivi kwa kuupa mwili msongo wa muda mfupi ambao unakukomaza zaidi. Njia za kufanya hivyo ni kama kufanya mazoezi makali sana ambayo yanakuletea maumivu, lakini unayafanya kwa muda mfupi. Kuoga maji ya baridi kali sana wakati wa asubuhi pia ni njia nyingine ya kukomaza mwili kwenye msongo. Na pia kufunga ni njia ya kuufanya mwili kutokutegemea chakula muda wote.

 1. Tahajudi ya kuondoa msongo.

Njia bora kabisa ya kuondokana na msongo ni kufanya tahajudi (meditation) ya kuondoa msongo. Kwa sababu msongo unaendelea kuwa na sisi kila wakati, ni muhimu kujua jinsi ya kufanya na kuifanya tahajudi hii kila mara na tutaweza kuwa na maisha tulivu sana.

Maandalizi ya kufanya tahajudi ya kuondoa msongo.

Katika kufanya tahajudi hii, unapaswa kutenga sehemu tulivu ambapo unaweza kukaa na kufanya tahajudi bila ya kusumbuliwa. Unapaswa kutenga dakika 5 mpaka kumi za kufanya tahajudi hii. Pia unapaswa kuzima simu yako au kuiweka kwenye utulivu wakati ambao unafanya tahajudi.

Jinsi ya kufanya tahajudi ya kuondoa msongo.

Kaa wima, mgongo ukiwa umenyooka na macho ukiwa umeyafunga.

Pumua kwa kina kwa kuingiza na kutoa hewa kupitia pua, vuta pumzi kwa kuielekeza tumboni, chini kidogo ya kitovu.

Weka mkono wako wa kushoto kwenye goti la kushoto, kiganja kikiangalia juu na kidole gumba kugusana na kidole kidogo.

Tumia mkono wako wa kulia kufunga matundu ya pua yako, tundu moja kwa wakati.

Ingiza pumzi ndani kwa kutumia tundu la pua la kushoto huku ukiwa umeziba tundu la kulia. Toa hewa nje kwa kutumia tundu hilo hilo la kushoto.

Rudia kuingiza pumzi na kutoa kwa kutumia tundu la kulia, huku ukiwa umeziba tundu la kushoto.

Endelea kurudia zoezi hili, tundu la kushoto na tundu la kulia mpaka muda uliotenga wa kufanya tahajudi kuisha (hapo unakuwa umeweka alamu itakayoita baada ya muda uliotenga kuisha).

Muda unapoisha, maliza kwa kupumua kwa kina kawaida kwa matundu yote mawili ya pua na mdomo na hapo unarudi kwenye hali yako ya kawaida.

Hii ni tahajudi rahisi sana kufanya, ambayo itaweza kukusaidia kuondokana na msongo wowote unaokuwa nao. Lakini pia unaweza kuifanya ukiwa popote na kwa muda mfupi na ukapata manufaa makubwa.

Rafiki yangu mpendwa, hivi ndivyo unavyoweza kukabiliana na msongo wa mawazo kwenye maisha yako na kuweza kuwa na maisha tulivu. Fanyia kazi haya uliyojifunza kwa sababu kila mmoja wetu anapitia misongo mbalimbali kwenye maisha yake. Usikubali kuendelea kutesa mwili wako kwa msongo wakati zipo njia sahihi kwako kuondokana na msongo. Tumia njia hizi kuwa na maisha bora na tulivu.

Kwenye TANO ZA JUMA hili la 23 nitakwenda kukushirikisha uchambuzi wa kina wa kitabu hiki cha THE URBAN MONK ambapo mwandishi ameziangalia kwa kina changamoto kumi kubwa za zama hizi, ambazo ni msongo, kukosa muda, kukosa nguvu, kukosa usingizi, maisha yasiyo na mwendo, ulaji mbovu, kutengana ana asili, upweke, fedha na kukosa maana na kusudi.

Usikose tano za juma hili, kwani utakwenda kupata suluhisho la changamoto ambazo zinamkabili kila mtu kwenye zama tunazoishi sasa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge