“Watch the stars in their courses and imagine yourself running alongside them. Think constantly on the changes of the elements into each other, for such thoughts wash away the dust of earthly life.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 7.47

Ni jambo kubwa na la kushukuru sana kwa sisi kuiona siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Siyo kila aliyelala jana amepata nafasi hii nzuri ya leo.
Hivyo ni wajibu wetu kuitumia vyema siku hii, kwa kuwa hatuna uhakika kama tutaipata tena siku nyingine kama hii.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari SAFISHA VUMBI LA MAISHA…
Mazoea ya maisha yetu yanatufanya tujione wadogo sana na tusiokuwa na kitu cha kufanya.
Tunapozifikiria changamoto mbalimbali za maisha tunajiona hatuna namna ya kupiga hatua zaidi.

Na pia changamoto kwenye kazi na biashara zetu zinaweza kutuvuruga na tusiweze kuona makubwa yajayo.
Mawazo yetu yananasa kwenye magumu tunayopitia na kukosa kabisa matumaini ya mambo mazuri zaidi ya baadaye.
Katika hali kama hizi ni rahisi sana kukata tamaa na kuona hakuna kikubwa unachoweza kufanya.

Lakini huo siyo ukweli, matatizo na changamoto unazopitia siyo kitu pekee ulichonacho kwenye maisha yako.
Bado ndani yako una uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo makubwa na maisha yako. Ni wewe kutambua na kutumia uwezo huo.

Njia nzuri ya kitambua na kutumia uwezo wako mkubwa ni kuiangalia asili.
Ziangalia nyota zikiwa kwenye mwendo wake, kisha jioni ukiwa miongoni mwa nyota hizo, ukiwa na mwendo wako pia.
Kwa kujipa matazamo huu, vitu vidogo vidogo havitakusumbua tena, maana tunajua nyota hazisumbuliwi na chochote kidogo.

Hivi ndivyo unavyoweza kusafisha vumbi la maisha, kuvuka changamoto na magumu unayopitia, kwa kujiona ukiwa juu kuliko chochote kile kinachokusumbua.
Angalia jinsi ambavyo asili inaendesha mambo yake, bila ya hofu wala mvurugano wowote, sayari zipo kwenye mwendo na nyota pia zipo kwenye mwendo, misimu ipo kwenye mwendo na hata viumbe wengine, mimea na wanyama wapo kwenye mwendo wao.

Na wewe kuwa kwenye mwendo na chochote kisikukatishe tamaa.
Una uwezo mkubwa wa kukabiliana na hata kuvuka chochote unachokotana nacho.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuziangalia nyota na kujiona miongoni mwa nyota hizo, ukiwa kwenye mendo wake na hilo likuondoe kwenye wasiwasi na hofu zisizo na msingi.
#MaishaNiMwendo, #UnaUwezoMkubwa, #MatatizoYasikukatisheTamaa

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha