Kama kuna neno moja ambalo linaweza kukupa uhuru mkubwa kwenye maisha yako, basi ni neno HAPANA.
Kusema hapana kunakuepusha na mambo mengi ambayo yangechukua muda wako na kukuondoa kwenye yale muhimu.
Kusema ndiyo kunakuja na majukumu mengi ambayo unaweza usiyaone wakati unasema ndiyo. Mfano umekubali kufanya kazi ya mtu, ukiamini ni kazi ya mara moja, lakini unapoanza kufanya kila siku anakuja na marekebisho au mapendekezo mapya, unakuta kazi hiyo inakuchukua muda mwingi kuliko ulivyotegemea.
Wakati tunaanza kwenye maisha, tunashawishika kusema ndiyo kwenye vitu vingi, kwa sababu hatuna cha kufanya. Kama huna kazi, unakuwa tayari kukubali kazi yoyote. Kama umeanza biashara na huna wateja, utakuwa tayari kumpokea mteja yeyote. Lakini vingi unavyokubali unapoanza siyo bora kwako.
Hivyo kadiri unavyopiga hatua, kadiri unavyofanikiwa, unapaswa kuongeza vigezo vyako vya kusema ndiyo. Usikubali kitu kwa sababu huko nyuma ulishakubali kitu kama hicho. Kama umeshajua siyo bora kwako na umeshaweza kupata kilicho bora zaidi basi ondoa kitu hicho katika vitu unavyosema ndiyo. Sema hapana bila ya kuyumbayumba.
Najua wapo watakaokuambua siku hizi unaringa, siku hizi una dharau kwa sababu zamani ulikuwa unasema ndiyo kwa vitu kama hivyo ila sasa unasema hapana. Wewe waache waseme, lakini wewe linda uhuru wako, uhuru kwenye muda, fedha na maisha yako ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako.
Na kama kuna kitu kimoja kitakupa uhuru mkubwa basi ni kusema HAPANA mara nyingi uwezavyo, na kuwa na vigezo vya juu vya kusema ndiyo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha, kulinda Uhuru wangu ni muhimu, Neno HAPANA nitalisema bila kuogopa au kumung’unya maneno nitalisema kwa nguvu na kwa sauti. Asante sana.
LikeLike
Vizuri Beatus,
Uhuru upo kwenye neno HAPANA.
LikeLike