Kama bado unasumbuka na kazi au biashara unazofanya, tatizo siyo kazi au biashara hizo, bali tatizo ni wewe mwenyewe.
Unapokuwa upo njia panda, hujui kazi au biashara ipi sahihi kwako kufanya,
Unapokuwa kwenye kazi moja lakini unatamani ungekuwa unafanya kazi ya aina nyingine.
Unapokuwa unafanya biashara uliyonayo lakini unajiambia wanaofanya biashara ya aina nyingine wananufaika zaidi na ungetamani kuingia huko.
Tatizo siyo kazi wala biashara wala wengine, tatizo ni wewe.
Na kama hutakubali tatizo ni wewe, hutaweza kuchukua hatua na kama hutachukua hatua hutajua kilicho sahihi kwako kufanya. Utaondoka kwenye jambo moja na kwenda jingine na huo ndiyo utakuwa mtindo wa maisha yako.
Kama bado unasumbuka na kazi au biashara unazofanya, tatizo ni hujajijua wewe mwenyewe na unachotaka kufanya na maisha yako.
Umejikuta unafanya kazi au biashara fulani kwa sababu ndiyo wengine wanafanya au wanategemea ufanye. Hujakaa chini na kujua unapendelea zaidi nini na una uwezo mkubwa kwenye maeneo gani.
Ukijua vitu hivi viwili, mapenzi yako na uwezo wako mkubwa, kisha ukavigeuza kuwa kazi au biashara yako kuu inayokuingizia kipato, hutapata hata dakika moja ya kufuatilia wengine wanafanya nini.
Utakuwa umetingwa kweli kweli na mengi ya kufanya, ambayo unapenda kuyafanya, unaweza kuyafanya vizuri na wengi wanakutegemea ukamilishe yale unayofanya.
Maisha ni yako na uamuzi ni wako, kama bado kazi au biashara unazofanya hazikupi utulivu wa ndani, jua kwamba hujajijua wewe mwenyewe vizuri. Chukua muda wa kujitafakari kwa kina na njoo na mpango mpya wa maisha yako.
Usijali wengine wanaishije au kufanya nini na maisha yao, maisha siyo mashindano, bali ni namna mtu unavyochagua kuyaishi, kulingana na kile unachopenda na unachoweza. Ukichagua kuishi maisha halisi kwako, hakuna kitakachokusumbua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,