Habari rafiki,

Maisha ni ushawishi, kiwango chako cha mafanikio kwenye maisha kinaendana na kiwango chako cha ushawishi. Wale wanye ushawishi mkubwa wanafanikiwa kuliko wasiokuwa na ushawishi.

Hali iko hivi kuanzia kwenye kazi zetu, biashara na hata maisha kwa ujumla.

Kwenye kazi wale wenye ushawishi mkubwa ndiyo wanapata nafasi nzuri za kazi na hata kuweza kushawishi kupata malipo mazuri. Kwa ushawishi wao wanaweza kufanya kazi na watu wengi na hilo linawafanya wapande cheo zaidi kupitia kazi zao.

Kwenye biashara, wale wenye ushawishi mkubwa ndiyo wanaopata wateja wengi, wanawahudumia vizuri na wanaendelea kuja pamoja na kuleta wateja wengine. Pia wenye ushawishi mkubwa ndiyo wanaozipata fursa nzuri, mfano kuweza kuwashawishi wengine kuongeza mtaji kwenye biashara yake na hata kuweza kushirikiana na wengine ambao wanahusika na biashara hiyo, mfano wazalishaji na wasambazaji.

Kwenye maisha ya kawaida, ushawishi una nafasi kubwa mno. Wale wenye ushawishi mkubwa ndiyo wanaopata wenza wanaowachagua, wanapata nafasi nzuri za kijamii, kama kwenye uongozi mbalimbali. Wenye ushawishi ndiyo wanaosikilizwa na maoni yao kufanyiwa kazi.

Kama unataka kufanikiwa zaidi kwenye maisha, basi eneo la ushawishi ni eneo moja unalopaswa kulifanyia kazi.

Uzuri ni kwamba, hakuna mtu aliyezaliwa akiwa na ushawishi, wengi wanajifunza kutokana na mazingira waliyokulia, lakini wengine wengi wanajifunza kupitia mafunzo na vitabu mbalimbali baada ya kuona kukosa ushawishi kunawagharimu.

Kwa mfano kuna mtu ambaye mmeanza naye kazi moja, au biashara ya aina moja, wote mna uwezo usiopishana sana, lakini unagundua mwenzako ana uwezo mkubwa wa kuwashawishi wengine kuliko wewe. Unaweza kujidanganya kwamba anapendelewa au ana bahati, au ukajifunza anachofanya na wewe ukakifanya pia.

Kama umeshindwa kupiga hatua kwa kukosa ushawishi au kama una ushawishi kiasi na ungependa kuwa na ushawishi zaidi, leo tunakwenda kujifunza njia tano za uhakika za kuweza kuwashawishi wengine kufanya chochote unachotaka.

Njia hizi tano zinatumia tabia za ubongo wetu binadamu inapokuja kwenye eneo la kijamii. Kuna vitu ambavyo ubongo wetu unapenda sana kuvipata, hivyo yeyote anayeweza kutoa vitu hivyo, atakuwa na ushawishi kwa wale wanaomzunguka.

SCARF MODEL OF BRAIN

Kwenye kitabu cha YOUR BRAIN AT WORK, mwandishi David Rock anatushirikisha mfumo wa ushawishi kwenye ubongo wa binadamu anaouita SCARF MODEL. Mfumo huu unagusa tabia tano kuu ambazo zina ushawishi mkubwa kwenye ubongo wa binadamu. Tabia hizo tano ndiyo zinawasukuma watu kuchukua hatua au kuwazuia wasichukue hatua. Kwenye makala hii, tunakwenda kujifunza tabia hizo tano, na jinsi tunavyoweza kuzitumia kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla.

Zifuatazo ni njia tano za uhakika za kuwashawishi watu wafanye chochote unachowataka wafanye.

MOJA; HADHI.

Sehemu yoyote ambayo kuna mtu zaidi ya mmoja, kitu cha kwanza ambacho ubongo wa binadamu hufanya ni kupima hadhi ya mtu ukilinganisha na wale wanaomzunguka. Mtu anapogundua hadhi yake ipo chini, anakosa msukumo wa kuchukua hatua yoyote ile. Lakini mtu anapogundua hadhi yake iko juu, anapata msukumo wa kuchukua hatua.

Hivyo jukumu lako wewe kwenye ushawishi ni kujua hitaji hili la watu kuwa na hadhi na kuwapa au kuwaonesha kwamba wana hadhi kubwa.

KAZI; Kwenye kazi, watu wanapenda kuonekana wana hadhi, hivyo waoneshe watu hadhi yako kwa kutambua michango yao na watakuwa tayari kufanya unachowataka wafanye.

BIASHARA; Kama unataka watu washawishike kununua unachouza, waoneshe ni jinsi gani kitu hicho kinaongeza hadhi yao kwenye jamii. Hii ndiyo sababu pekee dhahabu ni ghali kuliko chuma, kwa sababu dhahabu inamfanya mtu aonekane ni wa hadhi ya juu zaidi.

MAISHA; Chochote unachoshirikiana na wengine kwenye maisha, hakikisha huathiri hadhi zao. Epuka kuwakosoa watu mbele ya wengine, wasifie watu kwa mazuri wanayofanya, na kama hadhi yako iko juu ya wengine, angalia jinsi ya kuishusha kidogo na hilo litawashawishi kufanya unachowataka wafanye.

MBILI; UHAKIKA.

Hakuna kitu ambacho ubongo wetu wanadamu unapenda kama uhakika. Hii ndiyo sababu kubwa kwa nini watu hawapendi kubadilika. Watu wanapenda kufanya kile ambacho wameshazoea kufanya kwa sababu wana uhakika nacho, kuliko kujaribu kitu kipya ambacho hawana uhakika wanakwenda kupata nini.

Jukumu lako katika kuwashawishi wengine ni kuwapa uhakika wa kile unachowataka wafanye, na kadiri watu wanavyokuwa na uhakika, ndivyo wanavyokuwa tayari kuchukua hatua.

KAZI; Unapowapa watu jukumu la kufanya, waoneshe matokeo ambayo yanategemea kupatikana na hilo litawapa uhakika na kuwashawishi kuchukua hatua, kuliko wakifanya bila ya kujua matokeo gani wanategemea kupata.

BIASHARA; Unapotaka watu wanunue unachouza, wape uhakika wa kile unachowauzia, kwamba kitafanya kazi wanayotaka kifanye, na kama hakitafanya basi watakirudisha na kupewa kilicho sahihi au kurejeshewa fedha zao. Hii ndiyo sababu biashara nyingi huwa zinatoa waranti kwa wateja wake.

MAISHA; Kwa chochote unachotaka kuwashawishi watu wafanye, wape uhakika wa matokeo yanayokwenda kupatikana, hata kama ni kitu kipya, wasaidie watu kuona matokeo ya mwisho na watakuwa tayari kuchukua hatua. Hivi ndivyo viongozi wanavyokuwa na ushawishi kwa wale wanaowaongoza, kwa kuwa na maono makubwa ambayo wanayaeleza vizuri kwa watu na wanakuwa tayari kujitoa kuyafikia.

TATU; UDHIBITI.

Ubongo wetu wanadamu unapenda kuwa na udhibiti kwenye maisha yetu. Tunapenda kufanya maamuzi yetu, kuchagua kile tunachotaka sisi wenyewe na kuwa na maamuzi ya mwisho juu ya maisha yetu. Hii ipo hata kwa watoto, mtu anapogundua kwamba unamlazimisha kufanya kitu basi atafanya kinyume chake hata kama hakina faida kwake, ila tu akuoneshe kwamba ana udhibiti wa maisha yake.

Jukumu lako katika ushawishi ni kuwapa watu udhibiti juu ya maisha yako, kuwapa watu nafasi ya kufanya maamuzi juu ya maisha yao na nini wafanye.

KAZI; Epuka kuwasimamia wale walio chini yako kwa kila wanachofanya. Wape matokeo unayotaka wayapate, kisha wape uhuru wa kuchagua wanafanyaje kazi zao, muhimu ni wazalishe matokeo yanayotakiwa kupatikana. Kwa kuchagua jinsi ya kufanya kazi zao wenyewe, watu wanajituma zaidi.

BIASHARA; Usimchagulie mteja anunue nini, na wala usimlazimishe kununua chochote kile. Mpe maelezo sahihi kulingana na anachohitaji na bidhaa au huduma ulizonazo, kisha mpe uhuru wa kuchagua yeye mwenyewe. Watu wanapokuwa huru kuchagua wenyewe, wanakuwa huru na kushawishika kuchukua hatua kuliko wanapoona wanalazimishwa.

MAISHA; Epuka sana kuwapa watu ushauri ambao hawajakuomba, epuka kuwasaidia watu kutatua matatizo yao, na epuka kutoa maoni au mrejesho wa moja kwa moja kwa wengine. Wengi hupinga wanapoona wanapokea marekebisho au ushauri wa nini cha kufanya kutoka kwa wengine. Kama kuna mtu unaona anakosea au atanufaika zaidi kwa kufanya namna fulani, basi msaidie kufikia maamuzi hayo yeye mwenyewe, kupitia maswali na maelezo ambayo unakuwa unamla, lakini siyo kwa kumwambia hiki ndiyo unachopaswa kufanya.

NNE; UHUSIANO.

Ubongo wetu unapenda mahusiano kuliko kitu kingine chochote, kipaumbele chetu cha kwanza ni mahusiano. Ndiyo maana maumivu ya kuachwa au kutengwa ni makubwa kuliko maumivu ya kupigwa. Watu wanashawishika zaidi kufanya kitu pale wanapoona kwamba wengine pia wanafanya kitu hicho na siyo wao wenyewe. Pia wanapoona kila mtu anafanya, wanalazimika kufanya ili wasionekane wa tofauti na kutengwa.

Jukumu lako katika ushawishi ni kuwaonesha watu jinsi ambavyo kufanya kitu kinaboresha mahusiano yao na wengine, pia waoneshe kile unachotaka wafanye ndiyo kinafanywa na wengine.

KAZI; Unapotaka wengine wafanye jukumu fulani kwenye kazi, waoneshe kwamba ndiyo jukumu ambalo kila mtu anafanya. Au weka jukumu hilo liwe linafanywa kwa pamoja na wengine. Hakuna anayependa kuachwa nyuma.

BIASHARA; Waoneshe wateja wako watu wengine ambao wamenunua na kunufaika na bidhaa au huduma zako na watakuwa tayari kununua unachouza. Hapa ndipo nguvu ya shuhuda ilipo. Pia unaweza kutengeneza klabu au mfumo wa uanachama kwenye biashara yako, mtu anapoona kununua kwako anakuwa mwanachama, anathamini sana mahusiano yaliyo ndani ya uanachama kuliko kuwa nje.

MAISHA; Nguvu ya mahusiano na wengine ni kubwa, kila unapotaka watu wafanye kitu, waoneshe kwamba ndiyo kitu ambacho wengine wanafanya. Tumia watu ambao wale unaotaka kuwashawishi wanawaheshimu na kuwachukulia kama mfano kwao, na watashawishika zaidi. Mfano kama mtu unayetaka kumshawishi anampenda sana mchezaji fulani, unaweza kumwonesha kwamba kile unachotaka afanye, hata mchezaji huyo alikuwa anafanya au anafanya.

TANO; USAWA.

Ubongo wetu unapenda haki na usawa. Kunapokuwa na haki na usawa, ubongo unajiona uko salama na hivyo kusukumwa kuchuka hatua. Vitu hivyo vinapokosekana ubongo unakosa msukumo wa kuchukua hatua.

Jukumu lako katika kuwashawishi watu kuchukua hatua ni kutengeneza na kuonesha haki na usawa kwenye kile ambacho unawataka watu wafanye. Waoneshe watu kwamba kwa kuchukua hatua fulani, siyo tu inakuwa manufaa kwao, bali na kwa wengine pia.

KAZI; Waoneshe watu kwamba ni haki na usawa kwao kutekeleza majukumu fulani, ambayo kama hayatatekelezwa basi usawa ukakosekana. Pia mazingira ya kazi yawe na usawa kwa wote na watu watashawishika kuchukua hatua zaidi, kuliko pale ambapo baadhi ya watu wanapendelewa.

BIASHARA; Ihusishe biashara yako na kitu chochote cha kuisaidia jamii, na waambie wateja wako kwa kununua siyo tu wananufaika wao, bali pia wanawanufaisha watu wengine wasiojiweza. Hilo litawasukuma watu kununua zaidi. Biashara nyingi huwa zinatumia mbinu hii, kwa kuwaambia wateja sehemu ya faida inakwenda kuwasaidia watu walio kwenye mazingira magumu.

MAISHA; Simamia haki na usawa kwenye kila unachotaka watu wafanye, usionekane kupendelea upande wowote. Pia waoneshe watu kutokufanya kitu fulani kunawafanya waonekane ni watu wasio na haki au usawa. Hilo litawasukuma watu kuchuka hatua zaidi.

Rafiki, hizi ndizo njia tano za kukuwezesha kuwashawishi watu kufanya chochote unachotaka. Zitumie njia hizi kwenye kazi yako, biashara na hata maisha kwa ujumla na utaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine, ambao utakuwezesha kufanikiwa zaidi.

Kama ungependa kujifunza tabia za ubongo wako, ambazo kwa kuzijua utaweza kuutumia vizuri na hata kupiga hatua kwenye maisha yako, soma makala hii; Tano Za Juma Kutoka Kitabu Your Brain At Work (Mbinu Za Kushinda Usumbufu, Kuongeza Umakini Na Kuweza Kufanya Kazi Kwa Ubora Siku Nzima)

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge