“For philosophy doesn’t consist in outward display, but in taking heed to what is needed and being mindful of it.”
—MUSONIUS RUFUS, LECTURES, 16.75.15–16
Ni siku mpya, siku njema na ya kipekee sana kwetu.
Ni fursa bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari ACHA TABIA IPIGE KELELE…
Kinachokutofautisha wewe na watu wengine siyo maneno unayoongea wala ahadi unazotoa, siyo jinsi unavyovaa au mwonekano wako, bali tabia ulizonazo.
Watu watakujua kwa tabia zako, na hata uwe msemaji wa aija gani, watu wanaamini zaidi tabia zako kuliko maneno na ahadi zako.
Hivyo ili kuwa na maisha bora na yenye utulivu, usikazane kuwa mpigaji wa kelele ili watu wajue na wewe upo.
Bali kazana kujijengea tabia bora kabisa, tabia ambazo wengine hawana kabisa na hilo litawafanya wengi wakujue bila hata ya kupiga kelele.
Na kwa dunia ya sasa, dunia ambayo kila mtu anafikiri anaweza kufanikiwa kwa kupiga kelele au kuonekana zaidi, una nafasi kubwa na rahisi ya kupiga hatua kama utajijengea tabia bora, ambazo wengi kwenye zama hizi hawana.
Iwe ni kwenye ajira au biashara, kwa kujijengea tabia imara, wale wanaonufaika na unachofanya watajua wewe ni tofauti na watapenda kupata kile unachofanya, na hata kueleza tabia zako kwa wengine.
Ukichagua kuwa mwaminifu sana kwa kila unachofanya,
Ukachagua kujituma mno, kwenda hatua ya ziada kwa kila unachofanya,
Ukachagua kutekeleza kila unachoahidi, bila ya kujali inakuwa vigumu kiasi gani kwako.
Kwa tabia hizi chache tu, zinatosha kukutofautisha wewe na wengine wanaofanya kile unachofanya, na hivyo utapata wengi wanaohitaji huduma zako.
Acha wengine wapige kelele na kutaka kuonekana,
Lakini wewe kazana kujenga tabia imara, ambayo italeta matokeo bora ambayo yatapiga kelele inayosikika kuliko maneno matupu ya wengine.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujijengea tabia bora ambazo zinapiga kelele kuliko maneno ya wengine.
#TabiaNdiyoMsingi, #AchaTabiaZiongee, #UboraHaufichiki
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha