Kinachowazuia watu wengi kufanikiwa ni kutokujua nguvu za kubwa ziko wapi. Au wanaweza kujua nguvu zao kubwa zilipo, lakini wasiwe tayari kuzitumia kwa mafanikio yao makubwa, kwa sababu wanakuwa wamezoea kuishi maisha ya kawaida.
Kuna kitu kimoja au vichache ambavyo unaweza kuvifanya kwa ubora wa hali ya juu sana, kwa upekee ambao watu wengine wanashangaa umefanyaje. Kila mtu ana vitu vya aina hii, iwe ni kwenye kazi, biashara au maisha.
Vitu hivi ambavyo tunaweza kuvifanya kwa upekee ambao unawaacha wengine wakishangaa tumefanyaje, ndipo nguvu zetu kubwa zilipo. Na hapo ndipo mafanikio yetu makubwa yalipolala.
Huwezi kufikia mafanikio ya kweli kama hutatumia nguvu hii kubwa iliyopo ndani yako, kwa sababu ni nguvu ambayo huwa haichoki na haishindwi na chochote. Unaweza kupata mafanikio madogo kwa kutumia nguvu nyingine, lakini mafanikio ya kudumu na yenye amani kwako ni yale ambayo yanatumia nguvu kubwa iliyopo ndani yako.
Kwa dunia tunayoishi, kila mtu na kila kitu kinakulazimisha uwe kawaida, uachane na nguvu kubwa iliyopo ndani yako na ufanye kile ambacho kila mtu anafanya au kimezoeleka kufanyika. Unapotaka kufanya kitu cha tofauti na cha kipekee, wengi wanakuambia haiwezekani au utashindwa.
Unapaswa kuacha kuwasikiliza wengine na kusikiliza sauti ya ndani yako, kuisikiliza nguvu yako ya ndani maana hii huwa haikubali kuzimishwa. Unaweza kujaribu kuikwepa kwa muda, lakini mara kwa mara itaibuka kukukumbusha uwepo wake.
Kanuni fupi na ya uhakika ya kufanikiwa, ni kujua nguvu zako kubwa ziko wapi, kisha wafanye watu wakulipe kwa kutumia nguvu hizo kubwa. Utakuwa tayari kujituma zaidi bila ya kuchoka, utawanufaisha wengi, utatengeneza kipato kizuri na utapata amani ya moyo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,