Mpendwa rafiki yangu,
Kadiri siku zinavyokwenda na teknolojia kuwa kubwa ndiyo watu wanapotea zaidi katika kuimarisha mahusiano yao. Sasa ukikutana na mtu mtaongea dakika mbili baada ya hapo kila mtu anakimbilia kuangalia simu yake nini kinaendelea. Au unaongea na simu huku kwenye kikao na mtu, unakuta karibu muda mwingi uko kwenye simu kuliko kile ulichokiendea kukifanya.
Tunapata matokeo ambayo hayana ufanisi katika kazi zetu kwa sababu ya kukosa umakini kwenye kile tunachofanya. Kazi ya kufanya na kila dakika unataka kujua nini kinaendelea kwenye mtandao utaweza kufanya kazi bora? Unafanya kazi, lakini kila baada ya muda unachungulia kwenye simu.
Kiufupi mahusiano yetu tunayavuruga sisi wenyewe. Mtu aliyekuwa kijijini ana utulivu mkubwa wa akili kuliko mtu ambaye yuko mjini. Hata yule ambaye hana simu ana kuwa huru sana kuliko yule ambaye mwenye simu. Jaribu siku kujitenga na dunia, kuwa mbali na mitandao ya kijamii, weka simu yako pembeni na kuwa wewe kama wewe utaona utakavyojiona uko huru ukilinganisha na muda ambao ulikuwa na simu.
Fedha ni muhimu kweli, lakini fedha haijengi mahusiano yetu na kuwa bora zaidi ya muda. Muda ndiyo mtaji namba moja wa kuimarisha mahusiano yetu na kuwa bora. Mahusiano yetu mengi yamekosa muda, kwa mfano, mahusiano yetu ni kama bustani na kama tunavyojua bustani isiyoangaliwa na kumwagiliwa maji vizuri lazima itakauka. Sasa ili bustani zetu zisikauke tunatakiwa tuzipe muda mzuri wa kuziimarisha.
SOMA;Huu Ndiyo Aina Ya Msamaha Usiyo Kuwa Na Fadhila
Ukitaka kuanzisha mahusiano na mtu yeyote awe rafiki au mpenzi, mtaji wenu wa kwanza ni muda. Utakua na fedha lakini bado fedha haitoshi bila ya nyie kupeana muda na kuzungumza. Muda ni mtaji wa bure ambao tunaweza kuutumia vizuri na mahusiano yetu yakawa bora sana.
Hatua ya kuchukua leo; jitahidi kila siku kuimarisha mahusiano yako kwa kutenga muda maalumu wa kukaa na familia yako au watu ambao uko nayo kwenye mahusiano. Tenga muda wa kumsalimia hata mteja wako mmoja kila siku au ndugu, jamaa na marafiki.
Kwahiyo, hatuwezi kuwa na mahusiano bora kama tutashindwa kuyaimarisha kwa kutumia muda. Kila mmoja atumie muda wake vizuri. Usiwe mtumwa wa mitandao ya kijamii na ukasahau mahusiano yako na kumbuka watu wanapenda sana unapowapa muda kuliko maelezo.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana