Kinachowazuia watu wengi kufanikiwa kwenye maisha ni kuyafanya mambo rahisi kuwa magumu.

Kwa kuwa mafanikio yanaionekana kuwa magumu kufikia, basi wengi huamini hata njia za kufika kwenye mafanikio zinapaswa kuwa ngumu. Na hapo ndipo watu huyafanya mambo rahisi kuwa magumu, na hivyo kujiwekea vikwazo zaidi kwenye mafanikio yao.

Mwandishi mmoja amewahi kusema, kila kitu ni rahisi mpaka pale mtu anapochukua kozi juu ya kitu hicho. Akiwa na maana kwamba mfumo wa elimu, unachokua vitu rahisi na kuvifanya kuwa vigumu.

Njia ya kuelekea kwenye mafanikio ni rahisi, haihitaji kufanywa ngumu. Unachohitaji ni kukaa kwenye njia hiyo, kujituma na kuwa na subira, utayafikia mafanikio.

Chukua mfano mzuri kwenye fedha, njia ya kuelekea kwenye utajiri ni kuwa na shughuli inayokuingizia kipato, kuyafanya matumizi yako kuwa madogo kuliko kipato chako na kile cha ziada unakiwekeza sehemu ambayo inaweza kuzalisha zaidi. Je kuna ugumu wowote kwenye hilo?

Sasa njoo kwenye uhalisia, watu wanavyoishi, watacheza kamari au michezo ya bahati nasibu, watajiunga kwenye vikundi vya kuzungusha fedha kwa wengi na watashawishika kujiunga na biashara zinazoahidi kipato kukua mara mbili bila ya kufanya kazi yoyote. Na njia zote hizo, zinaishia kuwatenganisha watu na fedha zao.

Njia za kuelekea kwenye mafanikio zipo wazi na ni rahisi, usitake kuzifanya kuwa ngumu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha