Rafiki yangu mpendwa,
Katika zama tunazoishi sasa, zama ambazo tumedanganywa kwa kipindi kirefu kuhusu njia kuu ya kuingiza kipato, biashara zinabaki kuwa njia bora kwa mtu yeyote kujiingizia kipato kwa uhuru na uhakika.
Tumedanganywa kwa miaka mingi kwamba njia bora na ya uhakika ya kuingiza kipato ni kupitia ajira. Kwamba ukishaajiriwa unakuwa na uhakika wa kipato na hata ukistaafu basi unapata mafao ya kukuwezesha kuendelea na maisha yako bila ya shida.
Lakini kama ambavyo kila mtu anashuhudia sasa, ajira zimekuwa siyo tena njia ya uhakika ya kujiingizia kipato. Kwanza wenye sifa za kuajiriwa ni wengi kuliko nafasi za ajira zinazopatikana. Pili kipato cha ajira hakitoshelezi kuendesha maisha ya kawaida. Na tatu, tunaona jinsi ambavyo sheria za mifuko ya jamii zinavyobadilishwa kila siku, kwamba hata baada ya kuteseka kwa kazi kwa miaka mingi, huna uhakika na mafao yako baada ya kustaafu.
Kwa changamoto hizo kubwa tatu za ajira, kila mtu anapaswa kuwa na biashara, ambayo itamwezesha kuwa na kipato kisichowekewa ukomo na yeyote na pia kumpa uhuru wa muda na maisha yake.
Lakini pia kwenye biashara mambo siyo rahisi kama wengi wanavyokuwa wakiamini kabla ya kuingia. Biashara zina changamoto zake pia na wengi wanaoingia kwenye biashara zinaishia kufa. Zipo takwimu zinaonesha kwamba asilimia 80 ya biashara mpya zinazoanzishwa zinakuwa zimekufa ndani ya miaka mitano tangu kuanzishwa.
Na wala huhitaji kujua takwimu ili kuelewa hilo. Wewe angalia biashara nyingi zinazokuzunguka popote ulipo. Utagundua nyingi zinaendeshwa kwa ugumu sana. Utagundua biashara hizo hazikui licha ya kuwepo kwa muda mrefu. Ni mtu alianzisha duka lake na liko hivyo kwa miaka mingi. Au mtu alianzisha saluni yake au mgahawa wake na hakuna ukuaji wowote kwa miaka mingi ambayo mtu amekuwa kwenye biashara.
Wakati mwingine hayo yanatokea kwako binafsi, umeingia kwenye biashara kwa miaka mingi lakini hakuna hatua kubwa ulizopiga. Kila siku kwenye biashara yako inakuwa siku ya kuzima moto, unahangaika na biashara lakini mwisho wa siku hakuna manufaa makubwa unayoyapata.
Kipo kikwazo kimoja kikubwa ambacho kinapelekea biashara nyingi kufa na hata zile ambazo hazifi basi kinazuia zisikue. Kikwazo hicho ni kukosekana kwa maono makubwa.
Kama biashara haina maono makubwa, maono ambayo yamepangiliwa sawasawa, biashara hiyo itakufa. Na kama kwa bahati biashara hiyo haijafa, basi kamwe haiwezi kukua.
Hatua ya kwanza ya biashara kukua na kuweza kufikia mafanikio makubwa ni mfanyabiashara kuwa na maono makubwa ambayo anayafanyia kazi kila siku kwenye biashara yake. Siyo yale malengo ya kusema nataka nifike kiwango fulani na kuishi hapo, bali kuwa na mchakato unaoufanyia kazi kila siku kwenye biashara yako kujihakikishia ukuaji zaidi.
Gino Wickman katika kitabu chake kinachoitwa TRACTION; Get A Grip On Your Business, ameeleza maeneo sita muhimu ya kufanyia kazi kwenye biashara yako kama unataka ikue na iweze kukuletea mafanikio makubwa. Moja ya maeneo hayo sita ni maono ya biashara hiyo.
Maono ndiyo kitu cha kwanza alichokielezea kwa kina kwenye kitabu hiki, na anasema tatizo siyo kwamba wafanyabiashara hawana kabisa maono, kila mtu ana maono. Tatizo kubwa ni kushindwa kuyaishi maono hayo kila siku na kushindwa kuyawasilisha kwa wengine wanaofanya kazi kwenye biashara hiyo.
Gino anasema, ukienda kwenye biashara yoyote yenye wafanyakazi, ukimuuliza kila mfanyakazi yapi maono makubwa ya biashara hiyo, kila mfanyakazi atakuja na jibu lake. Na ukiwauliza kile wanachofanya kinachangiaje kwenye maono ya biashara hiyo wanakuwa hawana uelewa kabisa.
Katika hali kama hiyo, ambayo watu wanakuwa kwenye biashara lakini hawayaelewi maono makubwa ya biashara hiyo, Gino anafananisha na watu waliopo kwenye boti ambalo kila mtu anapiga makasia kwa upande wake, boti hilo haliwezi kwenda popote.
Lakini kama watu wote kwenye biashara watayajua maono makubwa ya biashara hiyo, na wakajua kile wanachofanya kinachangiaje kwenye maono hayo, basi biashara itapata nguvu kubwa ya ukuaji, itakuwa ni sawa na watu waliopo kwenye boti na wote wanapiga makasia kuelekea upande mmoja, nguvu ya kusonga mbele inakuwa kubwa.
Kwenye kitabu hiki cha TRACTION, Gino Wickman ametushirikisha hatua nane za kujenga biashara yenye maono makubwa na ambayo itafikia mafanikio makubwa sana. Gino ameshirikisha hatua hizi nane kama maswali nane muhimu ambayo kila mfanyabiashara anapaswa kujiuliza na kujipa majibu sahihi ambayo yatakuwa ndiyo mwongozo wa kuendesha biashara yake.
Karibu tujifunze hatua hizi nane zitakazokuwezesha kuwa na maono makubwa kwenye biashara yako na ufanikiwe sana.
MOJA; MISINGI MIKUU YA BIASHARA.
Ipi ni misingi mikuu ambayo inaendesha biashara yako?
Wote tunajua kwamba kama unataka kujenga nyumba basi msingi ni sehemu ya kuweka umakini mkubwa. Kadhalika kwenye biashara, unapaswa kujenga msingi imara kama unataka biashara yako ifanikiwe.
Hatua ya kwanza kwenye maono ya biashara ni kuainisha misingi mikuu ambayo inaendesha biashara hiyo. Hizi ni kanuni na maadili ambayo kila anayekuwa kwenye biashara hiyo anapaswa kufuata, ukianza na wewe mmiliki wa biashara.
Misingi hii ni muhimu kwa sababu inaongoza jinsi maamuzi yanavyofanywa kwenye biashara. Pia inawavutia watu sahihi na kuwaondoa wale wasio sahihi.
Unapaswa kuwa na misingi imara ya maadili ya kuendesha biashara yako, ambapo maamuzi yote yataongozwa kwa misingi hiyo. Pia utaajiri, kutunza na hata kufukuza wafanyakazi kwa kutumia misingi hiyo.
MBILI; KIPAUMBELE KIKUU.
Kipi kipaumbele kikuu cha biashara yako?
Hakuna kitu kinachowapoteza wafanyabiashara wengi kama fursa mpya na nzuri zinazojitokeza kila wakati. Iwapo mfanyabiashara atakuwa mtu wa kukimbizana na kila fursa inayojitokeza, hawezi kufanikiwa kabisa kwenye biashara.
Hii ni kwa sababu fursa mpya huwa ni nyingi na haziishi, na ili upate mafanikio kwenye jambo lolote, unahitaji kuweka muda na kazi.
Jukumu lako kama mfanyabiashara ni kuweka kipaumbele kikuu cha biashara yako, yaani ni aina gani ya biashara utafanya na kisha kuachana na kelele nyingine zozote.
Ukishachagua biashara utakayofanya, funga masikio kuhusu biashara nyingine zisizoendana na biashara hiyo. Hata uambiwe kuna biashara mpya na yenye faida kubwa, usidanganyike kuondoka wenye vipaumbele vyako na kwenda kwenye biashara hiyo mpya, utajipoteza mwenyewe.
Ukichagua nini unataka na kuweka nguvu zako zote kwenye kitu hicho, lazima utakifikia. Lakini ukigawa nguvu zako kwenye kila kitu kipya kinachojitokeza, unajizuia mwenyewe kufanikiwa.
Kama biashara uliyoanzisha imekuwa na unaona fursa ya kuingia kwenye biashara nyingine, fanya hivyo kwa mipango na maono yako na siyo kwa kusukumwa na tamaa zako na za wengine.
TATU; LENGO LA MIAKA KUMI.
Ni lengo lipi kubwa unataka kufikia ndani ya miaka kumi?
Kabla hatujaendelea hapa, hebu tafakari hilo swali na jipe majibu sahihi. Ni lengo lipi kubwa unalofanyia kazi ambalo unataka kulifikia miaka kumi ijayo? Watu wengi wanaweza kushangaa unapangaje miaka kumi ijayo, wengi kupanga mwaka mmoja tu ni shida.
Huwezi kufanikiwa kwenye biashara kama huna malengo ya muda mrefu. Na hata kinachofanya wafanyabiashara wengi kukimbizana na fursa mpya zinazojitokeza ni kwa sababu hawana malengo yoyote ya muda mrefu, hivyo chochote kinachojitokeza wanaona ni sahihi kwao kukimbizana nacho.
Unapaswa kuwa na lengo kuu la miaka kumi ijayo ya biashara yako, wapi unataka kufika na kwa kiwango gani. Lengo hili ndiyo litakusukuma kila siku, ndiyo litakuwa mwongozo wako na ndiyo litaathiri kila maamuzi unayofanya.
Kama huna lengo la miaka kumi ijayo ya biashara yako, hujajitoa kufanikiwa kweli kwenye biashara hiyo.
NNE; MKAKATI WA MASOKO.
Upi mkakati wa masoko unaofanyia kazi?
Biashara ni wateja, bila ya wateja, haijalishi una bidhaa au huduma bora kiasi gani, huna biashara. Na njia pekee ya kuwaleta wateja kwenye biashara hiyo ni mkakati wa masoko.
Wafanyabiashara wengi wadogo huwa hawajisumbui kabisa na masoko. Huwa wanaendesha biashara zao kwa mtazamo wa kizamani kwamba ukijenga biashara wateja watakuja wenyewe. Lakini zama hizi ambazo wafanyabiashara ni wengi, hakuna mteja atakayekuja kwako, bali unapaswa kuwatafuta wateja.
Unawatafuta wateja kupitia mpango mkakati wa masoko unaokuwa nao kwenye biashara yako.
Hii ni kusema kwamba ili biashara yako ifanikiwe, lazima iwe na mkakati wa masoko, ambao unawatambua wateja wa biashara hiyo, kuwafikia kule waliko na kuwashawishi kununua.
Mkakati wako wa masoko unapaswa kuzingatia vitu vinne muhimu sana;
- Kuwatabua wateja sahihi wa biashara yako, wale ambao wanaweza kunufaika na bidhaa au huduma unazotoa.
- Kutambua vitu vitatu vinavyokutofautisha wewe na wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara kama yako. Kama huna utofauti wowote na wafanyabiashara wengine, hakuna sababu ya mteja kuja kwako.
- Mchakato sahihi wa ufanyaji wako wa biashara, jinsi mteja anavyohudumiwa na hatua zote zinazochukuliwa kwenye biashara yako.
- Uhakika unaowapa wateja wako. Wateja wamepata fedha zao kwa shida, hawataki kuzipoteza, hivyo wanahofia sana kufanya manunuzi mapya. Unapaswa kuwapa uhakika kwamba wakinunua kwako hawapotezi fedha bali wanapata thamani.
Tengeneza mkakati wako wa masoko ambao unajumuisha vitu hivyo vinne na utaweza kuwafikia wateja wengi na kuwashawishi kununua kwako.
TANO; PICHA YA MIAKA MITATU.
Ni kitu gani unataka kufikia ndani ya miaka mitatu?
Baada ya kuwa na lengo kuu la miaka kumi ijayo ya biashara yako, unapaswa kujipa picha ya miaka mitatu ijayo. Miaka kumi ni mingi, hivyo kusubiri mpaka iishe ndiyo ujiangalie umefika wapi ni rahisi kupotea. Lakini unapojipa picha ya miaka mitatu, inakuwa rahisi kwako kuona hatua unazopiga.
Picha ya miaka mitatu inatoka ndani ya lengo kuu la miaka kumi. Ni njia ya kuligawa lengo kukwa kwenye hatua ndogo ndogo ambazo unazifanyia kazi.
Kuwa na picha ya miaka mitatu ambayo unaifanyia kazi kila siku kwenye biashara yako.
SITA; MPANGO WA MWAKA MMOJA.
Ni mpango gani unataka kukamilisha ndani ya mwaka mmoja?
Baada ya kuwa na picha ya miaka mitatu ya biashara yako, unapaswa kuwa na mpango wa mwaka mmoja. Kila mwaka unapaswa kuwa na mipango na mikakati unayofanyia kazi. Mipango hii inatokana na lengo la miaka kumi na picha ya miaka mitatu. Ni rahisi kujipima na kujifuatilia ndani ya mwaka mmoja kuliko kusubiri miaka mitatu au kumi.
Kadiri unavyochukua hatua kwenye mipango ya mwaka, utajifunza mengi zaidi na hivyo kuweza kufanya maboresho kwenye picha ya miaka mitatu na hata malengo ya miaka kumi.
Kila mwanzo wa mwaka lazima uweke mipango ya kibiashara ya mwaka huo, na mwaka unapoisha unajitathmini na kuweka mipango mingine bora zaidi kwa mwaka unaufuata. Kwa kufanya hivi, lengo kuu la miaka kumi utalifikia bila ya shida yoyote.
SABA; HATUA ZA ROBO MWAKA.
Ni hatua zipi unataka kuchukua ndani ya miezi mitatu?
Sisi binadamu huwa tunachoka kitu baada ya siku 90, yaani miezi mitatu. Tunapokuwa tunaanza kitu chochote, tunakuwa na hamasa kubwa sana, tunajituma na kuchukua hatua kubwa. Kadiri tunavyoendelea kufanya kitu hicho kinakuwa tabia na tunaanza kufanya kwa mazoea, hamasa inashuka na hatujitumi tena.
Ndiyo maana wengi huwa wanaweka malengo makubwa mwanzo wa mwaka, lakini wafuate miezi mitatu baadaye na waulize malengo yao ya mwaka ni yapi na watakuwa hawayakumbuki tena. Wanakuwa wamesharudi kwenye maisha ya mazoea.
Kuondokana na hali hii kwenye biashara, unapaswa kuwa na hatua za kuchukua kila baada ya miezi mitatu, yaani siku tisini au robo mwaka.
Baada ya kuwa na mipango ya mwaka mzima, igawe mipango hiyo kwenye miezi mitatu mitatu, kisha weka mikakati na hatua za kuchukua kwenye kipindi cha robo mwaka. Miezi mitatu inapoisha, kaa chini na tathmini uliyoweza kukamilisha, uliyoshindwa na hatua zaidi za kuchukua.
Huwezi kufikia mipango ya mwaka kama hujajiwekea utaratibu wa kujipima na kujitathmini kila robo mwaka.
Baada ya kuwa na hatua za kuchukua kwenye miezi mitatu, unaendelea kuzigawa kwa kila mwezi na kisha kwa kila wiki. Wiki ndiyo kipimo bora kabisa cha muda, ambapo unaweza kujitathmini vizuri na kuweza kuchukua hatua sahihi kwa matokeo unayopata.
Muhimu sana ni kujipima na kujitathmini, kwa sababu chochote kisichopimwa na kufanyiwa tathmini, hakiwezi kukua.
NANE; CHANGAMOTO.
Ni changamoto zipi unazokutana nazo na unazoweza kukutana nazo mbeleni?
Kila biashara ina changamoto zake, hakuna biashara isiyokuwa na changamoto kabisa. Lakini watu wengi huwa hawapendi kukutana na changamoto, na hivyo huwa hawapo tayari kuzikabili.
Wanachofanya wafanyabiashara wengi pale wanapokutana na changamoto ni kuzipuuza au kuziacha wakiamini zitaondoka zenyewe. Changamoto hizo huwa haziondoki, badala yake zinakua na kuota mizizi, na hizo ndiyo huja kuua biashara.
Unapaswa kujua zipi changamoto kubwa zinazoikabili biashara yako sasa na hata siku za mbeleni. Kisha kuwa na mkakati sahihi wa kukabiliana na kila changamoto pale inapojitokeza. Usijaribu kupuuza au kukwepa changamoto, badala yake ikabili kila changamoto inapojitokeza, na siyo tu utaitatua, bali pia utapiga hatua zaidi kwenye biashara yako.
Rafiki, hizi ndizo hatua nane za kujenga biashara yenye maono makubwa na itakayokufikisha kwenye mafanikio makubwa. Kumbuka hatua zote hizi nane unapaswa kuziandika, mipango yote uliyonayo kwenye kila hatua na kila anayehusika kwenye biashara yako anapaswa kujua wapi inalekea na kuwa na majibu sahihi ya hatua hizo nane.
Biashara ni rahisi sana kama utachagua kuendesha kwa misingi sahihi, lakini ni ngumu kama utaendelea kuendesha kwa mazoea. Achana na mazoea sasa na jenga biashara yako kwenye misingi sahihi, utaweza kuikuza na kupata uhuru wa muda, fedha na hata maisha.
Kwenye tano za juma hili la 18 nitakwenda kukushirikisha kwa kina mafunzo kutoka kwenye kitabu hiki cha TRACTION, nitakwenda kukushirikisha maeneo mengine matano ya kuzingatia ili biashara yako iweze kuwa na mafanikio makubwa. Usikose makala ya tano za juma hili kama unataka kuwa na biashara yenye mafanikio.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge