Unaweza kuyaishi maisha yako kwa mitazamo miwili,
Moja kila kitu ni kibaya kwako, na hapa kila kinachotokea utaona ubaya ndani yake. Ukifukuzwa kazi unaona kuna wabaya wako wamefanya ufukuzwe. Mahusiano uliyonayo yakivunjika unaona upande wa pili ulikuwa na matatizo. Ukianzisha biashara na ikafa unaona uchumi ni mgumu au huna bahati ya biashara.
Mbili kila kitu ni kizuri kwako, na hapa kila kinachotokea unakiona kama zawadi kwako, kikiwa na uzuri ndani yake. Ukifukuzwa kazi unaona ni zawadi kwako, ni nafasi sasa ya kwenda kujiajiri au kuanzisha biashara ili asiwepo mtu mwenye nguvu ya kukufukuza. Mahusiano uliyonayo yakivunjika unaona kama zawadi ya kujifunza makosa uliyofanya kwenye mahusiano hayo, ili unapoingia kwenye mahusiano mapya usirudie makosa hayo. Ukianzisha biashara na ikafa, unaona ni zawadi kwako kwa kujifunza mambo yaliyopelekea biashara hiyo kufa ili unapoanza biashara nyingine usirudie makosa ya awali.
Hakuna namna nyingine unaweza kuyachukulia maisha yako ukiacha namna hizo mbili, na uchaguzi ni wako, hakuna anayeweza kukulazimisha uwe na mtazamo huu. Japo jamii inaweza kuwa imekujengea mtazamo fulani, lakini ukishajitambua huwezi tena kumlaumu yeyote, ni wewe unayechagua mtazamo unaoenda nao kwenye maisha.
Ushauri wangu kwako rafiki yangu ni yachukulie maisha kama mchezo, na unachocheza nacho ni kutafuta zawadi kwenye kila unachopitia kwenye maisha yako. Chochote kile unachokutana nacho, hata kiwe kibaya na kigumu kiasi gani, ndani yake kuna zawadi kwako. Wakati mwingine ni dunia inajaribu kukustua, kwamba umelala sana, stuka, mambo siyo rahisi kama unavyofikiri.
Sheria ya asili ni kwamba kila kitu kinapanda na kushuka, kila kitu kina misimu yake, hivyo usiyumbishwe na mienendo hii ya asili, chagua mtazamo sahihi kwako na ishi maisha yako kwa mtazamo huo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,