Mpendwa rafiki yangu,

Kila mmoja wetu anasukumwa kufanya  na vitu viwili kwenye maisha yake. Kitu cha kwanza ni kupata kile anachotaka ambacho ndiyo furaha. Watu wengi wanasukumwa kufanya ili waweze kupata kile anachokitaka. Imekuwa ni hamasa kwa kila mtu kuhamasika kufanya ili aweze kupata kile anachotaka.

Licha ya kusukumwa na kile tunachotaka lakini pia tunasukumwa ili kuepuka kile tusichotaka ambacho ndiyo maumivu. Kuna wakati unajikuta unajituma tu ili uweze kuepuka maumivu fulani kwenye maisha yako. Kwa mfano, unaweza kuwa ni mtu unayeogopa kuwa na maisha mabovu hapo baadaye hivyo unajikuta unajituma sasa kurekebisha mambo ili usije kuteseka kwa maumivu hapo baadaye.

Kila mmoja wetu anapenda kuishi maisha ya furaha na mafanikio. Hakuna mtu ambaye anakaa chini na kupanga ni namna gani anaweza kuwa mtu asiyefanikiwa wala kuwa na furaha. Hakuna anayependa shida, kumbe kila mmoja huwa kusudi lake ni kuwa bora kwenye maisha yake ndiyo kila siku tunasukumwa kufanya ili tuweze kupata kile tunachotaka na kuepuka kile tusichotaka.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Mafanikio na furaha zetu msingi wake mkuu uko kwenye mahusiano yetu.  hivyo basi, mafanikio na furaha zetu zinajengwa kwenye mahusiano yetu.

Kama unataka furaha hutoweza kuipata nje ya mahusiano yako. wale watu wako wa karibu, marafiki, ndugu na jamaa ndiyo wanakuwa msingi wa mahusiano yetu. Bila mahusiano mazuri basi mafanikio na furaha zetu zinakuwa hazina nguvu.

SOMA; Mtaji Namba Moja Wa Kuimarisha Mahusiano Yako

Tukiwa na mafanikio lazima tuwe na watu ambao tutaweza kufurahia nao mafanikio yetu tuliyoyapata sasa kama hatuna mahusiano mazuri furaha mafanikio yetu yanakuwa hayana maana. Ukiwa ni mtu wa kujenga mahusiano yako vizuri na wengine hata siku ukifa siyo fedha au mali zako ndiyo zitaongea bali ni namna gani mahusiano yako yaliyokuwa na wengine.

Mahusiano yako na wengine ndiyo yatakuwa msemaji wako. Jinsi unavyoishi na watu kwa ukarimu, bila kujali cheo au uwezo mkubwa ulio nao wa kifedha. Unatakiwa kushirikiana na watu kwa kujenga mahusiano.

Kila mmoja wetu hapa ametokea kwenye mahusiano. Sijui kama kuna mtu anaweza kusema mimi siko kwenye mahusiano, una mahusiano na ndugu zako kama vile wazazi na wengine, ukishakuwa binadamu aliyezaliwa na mwanamke basi huwezi kukwepa mahusiano.

Ili mahusiano yawe vizuri yanahitaji kujitoa kweli kweli kwa sababu mahusiano yana gharama na gharama yake ni kumwagilia upendo. Mahusiano yako yanahitaji upendo sana ili yaweze kuimarika vizuri.

Hatua ya kuchukua leo; kuwa na mahusiano mazuri na wengiene kwa kuwapa upendo, muda na kuwathamini. Ukiweza kuwapa upendo, muda na kuwathamini bila kujali jinsi walivyo utakua umeshibisha njaa ya mahusiano yako.

Kwahiyo, tukiwa na mahusiano mazuri kwenye kila eneo la maisha yetu lazima tutakuwa na mafanikio na furaha na mahusiano yetu. Miili yetu ikikosa chakula itakufa vivyo hivyo mioyo yetu inayojenga mahusiano ikikosa upendo itakufa. Jenga mahusiano yako kwani ndiyo msingi wa mafanikio na furaha yako.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana