Ili kufika kule unakotaka kufika kwenye maisha yako, unahitaji kuwa na mipango ya kukufikisha pale. Mipango ni muhimu sana, kwa sababu hakuna chochote kinachotokea kama muujiza. Lazima kifanyiwe kazi kwa mpango unaoeleweka.

Lakini mipango imekuwa kikwazo kwa wengi kupata kile wanachotaka. Kwa sababu wanapoweka mipango, wanataka kila kitu kiende kama walivyopanga, inapotokea baadhi ya vitu kwenda tofauti, wanaona mpango mzima umeshindwa.

Unachopaswa kujua ni kwamba mpango wowote unaoweka ni mwongozo tu wa kukufikisha kule unakotaka kufika, na siyo msaafu ambao haubadiliki. Mipango unayoweka inaweza kubadilika kadiri unavyokwenda.

Unapokuwa unaweka mipango ni kama unatabiri mambo yanakwendaje, lakini wote tunajua hakuna ambaye anaweza kutabiri kwa uhakika wa asilimia 100. Hivyo kadiri unavyokwenda, utagundua baadhi ya mambo uliyopanga hayaendani na hali ilivyo. Katika nyakati kama hizo unapasa kurekebisha na kuboresha zaidi mpango wako ili uweze kuchukua hatua sahihi kufika unakotaka kufika.

Usikazane kufuata mpango kama ulivyo kama hali haiendani na mpango ulivyokuwa. Kwa sababu mwanzo ulipanga utatumia kitu fulani na sasa umegundua hakipatikani, tumia mbadala wake. Usiishie hapo kwa sababu ulichopanga kutumia hakipatikani.

Ukiiona mipango yako kama mwongozo, utaweza kujiongoza vizuri kufika kule unakotaka kufika.

Kwenye kila hali unayopitia, lazima uifanyie tathmini na kuona kama mpango wako wa mwanzo unaendana na hali ilivyo. Kama unaendana basi endelea kuchukua hatua na kama hauendani na hali, badili mpango wako ili uweze kuendana na hali iliyopo.

Kumbuka kauli ya Martin Luther King Jr kwamba kama huwezi kuruka basi kimbia, kama huwezi kukimbia basi tembea na kama huwezi kutembea basi tambaa, chochote unachofanya, hakikisha unasonga mbele zaidi. Hii ndiyo maana halisi ya kutumia mpango kama mwongozo na kutokukubali kukwamishwa na chochote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha